Loading...

Monday, July 21, 2014

Utamchumbia Binti Mpenda Vitabu?

CHUMBIA BINTI MPENDA VITABU

Hii ni kwa vijana wanaopenda kuoa! Ukitaka kuoa, chumbia Binti Mpenda Vitabu ( BMV) 

Kwa nini? Wa kazi gani? Utampata wapi?

Unaweza kumpata Maktaba akihangaika na vitabu vyenye vumbi na harufu kali ichomayo puani; vitabu ambavyo vimeuvaa uajuza na ushaibu kwa kutofunuliwa siku nyingi. Waweza pia kumkuta kwenye maduka ya vitabu akinunua vitabu. Ukisikia kuna uzinduzi wa kitabu sehemu au mjadala wa Kitabu Nilichosoma, Jongea maeneo hayo kwa vile BMV hawezi kukosa! Nenda tu hata kama hupendi vitabu! 

Ukibahatika kukutana naye kwenye daladala, yu nawe siti ya jirani, lazima atakuwa kashika kitabu. Usishangae kwa nini hakusemeshi; kitabu humtia mtu upofu asione cha jirani. Tafadhali, usimsemeshe mambo yasiyo na kichwa wala miguu; mara ‘dada habari’; ‘waitwa nani’? waenda wapi?. Hutopata mwitikio mzuri. Kama wataka kumnasa, msalimie kisha zungumza naye kuhusu kitabu; ’’Samahani, hii ni fiction au non-fiction?’ ‘’Yaelekea ni kizuri eeeh?’’ ‘’Kinahusu nini? ‘’ BMV hupenda kuulizwa mambo ya vitabu. Jitahidi kadiri ya uwezo wako mazungumzo yako yajikite kwenye vitabu. Tupa ndoano kwa kuazima kitabu; atakupa namba ya simu. BMV hupenda wapenda vitabu.

Endelea kuwasiliana naye. Nakusihi, kwenye mazungumzo yenu, habari ya vitabu iwe mbele. Mchunguze kuhusu vitabu avipendavyo. Aweza kuwa mpenzi wa fasihi. Naam, tuchukulie ni mpenzi wa fasihi. Basi jitahidi ujikite hapo.

Ni siku yake ya kuzaliwa. Unapanga kumfanyia nini? Keki? Kadi? Unasema unataka kumnunulia simu ya kisasa halafu umpeleke outing pale Samaki Samaki au Del Monte? Haya yote ni mazuri lakini hayataukosha vilivyo moyo wa BMV. Ngoja nikueleze. Unakifahamu kitabu kipya kilichotoka karibuni? Yaweza kuwa umekwisha msikia akikitaja kwamba kikiingia madukani atakinunua. BMV hutumia sehemu ya pesa yake kununua vitabu. Basi chunguza kama hajakinunua. Nenda kakinunue kisha kiweke kwenye bahasha nzuri.
 
Mwambie kwamba ungependa kutoka naye outing. BMV hupenda pahala tulivu. Mpeleke ufukweni au Soma Book Cafe kwa Demere Kitunga . Amini nakuambia, atafurahi mno kuliko unavyodhani. Zungumza naye. Kumbuka nilivyokuhusia, mazungumzo yenu yahusu vitabu. Kisha m-suprise kwa zawadi. Mweleze afumbe macho…eeh unataka kumvisha pete? Acha kabisa! Usifanye hivyo sasa; haraka haraka haina baraka. Toa kitabu ulichonunua kutoka kwenye mkoba wako kisha kiweke mezani. Mwambie kuna zawadi yake mezani na kwamba aotee ni zawadi gani. Usidhani ni mbashiri akipata; BMV ametawaliwa na vitabu kichwani. 

Mwambie afumbue macho kisha achukue zawadi yake kwenye bahasha. Akifungua na kukuta kitabu chenyewe ni kile akipendacho, tarajia maneno matamu toka kinywani mwake! Usishangae, BMV huthamini vitabu kuliko chochote.

Acha siku hiyo ipite. Siku nyingine, muombe msome kitabu pamoja au akusimulie kitabu chake pendwa. Fanyeni haya ufukweni. Siku hiyo, waweza kumueleza kiu yako; kiu ya kuwa naye maishani. Usidhani maneno yako matamu yatamduwaza; ameshasoma mengi. Ameshasoma vitabuni ahadi za wanaume wanaoahadi kutoa milima na mito wakikubaliwa au wale wanaoahidi magari huku wangali makapuku wa kutupwa. Ameshavisoma visa vya wanaume vinga’ng’anizi. Au umesahau kile kisa cha Mmbu king’anganizi alichowahi kusimulia Chinua Achebe? Ngoja nikukumbushe!

Hapo kale Mmbu alimpenda sana sikio (sikio hilihili lililo mwilini mwako). Basi Mmbu akamwendea sikio na kumweleza kuhusu pendo lake kwa sauti ibembelezayo kwa huba. Mrembo sikio kusikia maneno ya Mmbu akadondoka chini kwa kicheko. Kisha akarudi pahala pake na kumwambia Mmbu kwa dharau. ‘’Wewe mbu kiumbe unayeishi kwa wiki moja kisha ukaondoshwa na kifomithili ya mkulima ang'oavyo magugu ndiyo unipose mimi! Unataka kuniacha mjane halafu anioe nani?’’

Mmbu alijaribu kumbembeleza sikio bila mafanikio. Hoja ya sikio ilikuwa ile ile: kwamba Mbu ana maisha mafupi. Basi Mbu akasema kwa huzuni..’’Hao waliokuambia kuwa nina maisha mafupi wamekuongopea, nitakuthibitishia hili’’. Basi ikawa kila siku Mmbu anakuja sikioni kwa binadamu na kumweleza sikio kwamba bado yu hai. Hata sikioni mwako bila shaka hufika kuendeleza ushawishi wake kwa mnyange sikio. Ni kwa sababu hujui lugha ya Mmbu ndiyo maana unadhani amekuja kukupigia kelele tu! Akija kwa binadamu yoyote, iwe amelala au yu macho, lazima aje kwanza kwa binti sikio kumsalimu. ‘’Ewe sikio kipenzi, tazama nipo hai, nikubalie’’ Kweli Mbu king’ang’anizi!

Kwa hiyo ukiwa na BMV, jua visa vyote hivi amekwisha visoma! Habari ya kumuota mtu ndotoni au kumuona kwenye glasi achana nayo! Maneno haya yaseme ukiwa na wasichana wengine, si BMV! Mweleze kwamba unampenda. Akikuuliza kwa nini, mweleze unapenda kila kitu chake. Usisahau kusema pia unaipenda tabia yake hasa kupenda kwake kusoma vitabu. Hapa BMV atafurahi sana. Furaha yake ni vitabu.

Akikubali, anza uhusiano wa kimapenzi. Jitahidi nawe uanze kupenda vitabu taratibu. Akikuuliza unamjua Shaaban Robert usikimbilie kusema ni shule ya sekondari; sema ni nguli wa fasihi. Akisema kuhusu Andanenga usije dhani ni jina la mzizi fulani; huyo ni malenga mashuhuri almaarufu kama ‘’Sauti ya kiza’’. 

Muoe. Kama ndiyo kwanza mnaanza maisha, m-surprise kwa kumnunulia kabati jipya la vitabu. Mkijenga nyumba, usisahau study room, chumba cha kujisomea. Usishangae usiku akiwa kwenye usingizi mzito akagumia ndotoni ’’usimuuue usimuuee!’’. Hakuna haja ya kumwamsha; jua anaota ya vitabuni!
Ukirudi nyumbani halafu ukakuta bado hajapika chakula usimfokee wala kumpiga, hiyo ndiyo raha ya BMV. Nenda alipo, yaweza kuwa chumbani kajilaza na kitabu mkononi au nje kwenye bustani akisoma kitabu! Kwa BMV, vitabu ni popote! Msogelee karibu kisha soma naye hadithi, namaanisha kula naye hadithi kwa sababu huo ndiyo mlo mkuu wa BMV. 

Ukiishi na BMV jua haupo peke yako. Mpo waume wawili; wewe na vitabu. Usimuonee wivu mume mwenza kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumfisha BMV kwenye kilele,

Kilele kilojaa raha
Kilele kiso karaha
Kilele chenye furaha
Akawa hajitambui

Hajui yupo ndotoni
Au kapaa mbinguni
Ala raha za peponi
Mrembo hajitambui

Ado Shaibu ( Komredi wa Malenga )

………………………………………………..
NOTE: Tangu kuandikwa kwa mara ya kwanza kwa makala ya ‘’Don’t Date a Girl Who Reads’’ ya Charles Warnke, makala nyingi zaidi zimeandikwa kuchukua upande wa mwandishi au upande tofauti. Niliandika post hii baada ya kusoma makala ya Jennifer Souter iitwayo ''You Just Date a Girl who Reads’’.

Kwa wale wapendao kusoma makala zaidi kuhusu mjadala huu pitieni kwenye links zifuatazo:
Why You Simply Have to Date a Girl Who Reads | Jennifer Soutar 
Don't date a girl who reads — Charles Warnke - think thank thunk 
You Should Date An Illiterate Girl | Thought Catalog 
Angalizo: Unaposoma links hizo kumbuka, fasihi ndiyo iliyoutawala mjadala.

Wednesday, July 16, 2014

New Book on 'Religion & State in Tanzania Revisited'

Thursday, July 10, 2014

Ubidhaishaji wa Maumbile ya Binadamu

UBIDHAISHAJI WA MAUMBILE YA BINADAMU: Toka Sarah Baartman mpaka Agnes “Masogange”

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Tunaishi katika zama mpya. Zama za ubepari uliochukua sura ya uliberali mamboleo. Ipo tofauti kati ya ubepari halisi na uliberali-mamboleo. Ubepari halisi ulijikita katika kutengeneza faida kwa kuzalisha bidhaa viwandani. Uliberali mamboleo ni ubepari wa kikasino. Katika zama za uliberali-mamboleo uzalishaji bidhaa siyo tena msingi wa ubepari.

Upepari wa kikasino ni ule wa kutengeneza faida na kulimbikiza mtaji bila kujihusisha katika uzalishaji-mali. Uzalishaji-mali hufanyika mashambani na viwandani. Katika ubepari wa kikasino na kiporaji, mtu hutengeneza pesa kwa biashara za udalali, ununuaji na uuzaji hisa, ukopeshaji, kamari, ulanguzi/upaishaji wa bei za vitu, n.k.

Katika uliberali mamboleo, ambao ni awamu ya ubepari uliofilisika, kila kitu hugeuzwa bidhaa na kuuzwa au kununulika sokoni. Huduma za jamii (afya, elimu, makazi na maji) hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni kama itokeavyo kwa manukato, nguo au magari. Ubidhaishaji umevuka mipaka, kiasi kwamba hata viumbe vinabidhaishwa. Katika makala haya nitazungumzia ubidhaishaji wa muoneko wa viungo vya binadamu, hususan akina mama ufanyikao katika mfumo wa uliberali mamboleo.

Agnes Masogange
Jina la Agnes Gerald “Masogange” sio geni katika masikio ya Watanzania. Ni mwanadada mrembo. Lakini warembo wapo wengi. Masogange ni maarufu. Akina dada warembo na maarufu wapo wengi pia. Lakini umaarufu wa Masogange ni tofauti. Umaarufu wake umepatikana kutokana na anavyoonekana katika video za wanamuziki, na sehemu ya mwili wake inayompatia umaarufu ni makalio yake.

Mara kadhaa amekwishahojiwa naye akajisifia kuwa anajisikia raha kuwa na makalio makubwa: “Hakuna sehemu ninayoipenda kama makalio, yamekaa vizuri, nayapenda, najidai kupitia sehemu hiyo niliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Agnes katika moja ya mahojiano yake yaliyochapishwa Machi 29, 2014 katika blogu ya Global Publishers.

Ukiingia katika mtandao utaona picha na video za Masogange. Nyingi ya hizo zinaonyesha “sehemu hiyo aliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu”. Ameenda mbali hata kuweka picha na video zinazoonyesha utupu wake. Huko mtandaoni kuna wanaomlaani. Lakini hawa ni wachache. Wengi, hasa vijana, wanamsifia.

Lakini ole wako ewe msomaji mwema. Kama ulidhani kuwa makala haya yamelenga kumlaani ama kumsifia Masogange basi umekosea. Makala haya hayamzungumzii Masogange kama mtu bali yanazungumzia mfumo katili wa uliberali mamboleo.

 Nitatumia pia mfano wa “Masogange wa Kenya” aitwaye Vera Sidika. Afrika nzima kuna “akina Vera na Masogange” wanaoibuka na kujizolea umaarufu na pesa. Huko Ulaya na Marekani idadi ya mabinti wa aina hiyo imekithiri. Katika kona mbalimbali za dunia, wapo mabinti wanaotamani kuwa na umbile kama la Vera Sidika au Masogange ili wawe maarufu na kujizolea pesa. 

Je, ni nini chanzo cha wimbi hili la ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu? Nani mwenye maslahi katika wimbi hili? Makala haya yamelenga kujibu maswali hayo.

Sarah Baartman
Kwa kuanzia, ningependa kujadili kisa cha Sarah Baartman, binti wa kiafrika aliyezaliwa nchini Afrika Kusini mwaka 1789. Alifariki mwaka 1815, jijini Paris, Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 26. Je, alifikaje Paris?

Sarah alikuwa mtumwa huko Afrika Kusini. Mmiliki wake mwenye asili ya kikaburu aliamua kumuuza kwa daktari wa kiingereza aliyeitwa Alexander Dunlop. Dunlop alikuwa ameona ‘fursa za kiuchumi’ katika umbile la Sarah, na hasa makalio yake makubwa. Hivyo akamshawishi mmiliki wa Sarah amwuzie “bidhaa” hiyo adimu ili akaitumie kutengeneza pesa huko Ulaya.

Sarah alipelekwa katika nchi kadhaa za Ulaya, hasa Uingereza na Ufaransa. Huko alipelekwa katika kumbi za maonyesho akiwa uchi, na wazungu wakawa wanalipa viingilio kuja kushuhudia weusi wa ngozi yake na ukubwa wa makalio yake na sehemu zake za siri.

Ili kutengeneza pesa zaidi, mmiliki wa Sarah akawa akimuuza kwa wanaume wa kizungu waliotaka “kumvumbua” zaidi mwanadada huyo wa Kiafrika. Sarah akafariki kwa ugonjwa wa zinaa. Hata baada ya kufariki viungo vya mwili wake vilikatwa na kuwekwa katika makumbusho huko Paris ili wazungu wakajionee. Sarah aliendelea kuwa bidhaa na kivutio cha utalii hata baada ya kufa.

Tofauti ya Sarah na “ma-modo” wa sasa
Je, kuna tofauti kati ya Sarah na “mamodo” wa sasa?
Sarah aliishi katika kipindi ambacho biashara ya utumwa ilikuwa imeshika hatamu. Waafrika waligeuzwa bidhaa, wakauzwa na kununuliwa sokoni, kama vile mtu anunuavyo nyanya, nguo au kuku. Wakapelekwa huko Amerika kuzalisha mashambani na migodini. Nguvu-jasho ya Waafrika hawa ndiyo iliyozijenga na kuzistawisha nchi za Ulaya na Marekani ambazo leo tunakwenda kuomba misaada ya hali na mali.

Kwa hiyo, kama ilivyokuwa kwa babu na bibi zetu wengine waliopelekwa utumwani, Sarah hakwenda Ulaya kwa hiari yake. Alilazimishwa. Alikuwa ni bidhaa.
Usipofanya uchambuzi wa kina, unaweza kusema kuwa “ma-modo” wetu wa leo wanaotumia maumbo yao kama vivutio hufanya hivyo kwa hiyari yao. Lakini ukweli ni kwamba kuna nguvu ya kimfumo inayowalazimisha kufanya hivyo wafanyavyo. Nitajadili.

Maumbile ya Sarah yalikuwa ni ya asili. Mwili wake ni ule aliojaaliwa na Muumba. Katika zama zetu, wapo mamodo wenye maumbile ya asili. Lakini wapo wengi pia ambao wamelazimika kubadili maumbile yao. Ukuzaji wa makalio na matiti, uchubuaji wa ngozi, na hata ubadilishaji wa jinsia yamekuwa ni mambo ya kawaida.

Kiini macho na nguvu ya soko
Ukiingia mtandaoni, utakuta kampuni kadhaa zikitangaza bidhaa za kukuza makalio na matiti. Kwa wanaume, zipo dawa za kunenepesha na kurefusha uume, kukuza misuli, n.k. Kampuni hizi za kibepari ndizo kiini hasa cha ubidhaishaji wa viungo vya binadamu, na hasa makalio na matiti. Ili bidhaa zao zikubalike, kampuni hizi sharti zitengeneze soko la bidhaa zao.

Soko lenyewe hutengenezwa kwa kubadili mtazamo na fikra  za watu, na hasa vijana, juu ya dhana ya urembo, mapenzi na mahusiano ya kimwili. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na kampuni za utengenezaji wa filamu za ngono, kampuni za kurekodi video za muziki, wamiliki wa vilabu na makasino, magazeti na televisheni za udaku, hospitali za binafsi za upasuaji wa plastiki, kampuni za uzalishaji wa dawa hizi zimewezesha kukubalika kwamba makalio na matiti makubwa ni urembo, lakini pia ni hazina murua kwa shughuli za ujasiriamali.

Kwa hiyo, katika zama zetu hizi binti mrembo anasemekana kuwa ni yule aliye na makalio makubwa, matiti makubwa, na ngozi nyeupe. Ikitokea hukuzaliwa na vitu hivi basi usikonde: utavipata kwa kutumia dawa au kwa kufanyiwa upasuaji wa plastiki. Binti mwenye sifa hizi anaaminishwa kuwa ana “rasilimali” ambayo anaweza kuitumia kutengeneza pesa iwe ni kwa kujiuza sokoni ama kwa kuwa na mpenzi mwenye pesa.

Hivyo basi, wapo wanenepeshao viungo vyao ili kuwaridhisha wapenzi wao. Wapo wafanyao hivyo ili “kwenda na wakati”. Lakini wengi pia hufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya soko. Soko lenyewe sio lazima liwe la kujiuza kimwili. Ni soko la kuuza “makalio”, watu wakayaona iwe ni katika klabu za usiku, magazeti ya udaku au video za muziki, na mwenye nayo akatengeneza pesa.

Tarehe 10 Februari 2011, gazeti la MailOnline la nchini Uingereza liliripoti kifo cha Claudia Aderotimi, mwanafunzi wa nchini Uingereza, aliyefariki huko Marekani akiwa ameenda kufanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio. Claudia, ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mnenguaji katika video za wanamuziki wakubwa, aliwahi kukosa tenda kwa kutokuwa na makalio makubwa. Aliambiwa kuwa ili afanikiwe ni lazima awe na makalio yaliyobinuka kama ya mwanamuziki Beyonce. Hivyo, mfumo tulio nao unawatengenezea mabinti kiini-macho (illusion) cha “kuwa na umbo kama la Beyonce ili ufanikiwe”.

Hapa Afrika, wapo akina-dada wachache ambao kutokana na maumbile yao, yawe ya asili ama “yaliyokarabatiwa” kwa dawa au upasuaji, wamefanikiwa kujipatia pesa, Maisha yao ni ghali: toka nguo wavaazo, manukato wajifukizayo, magari waendeshayo na kumbi za starehe waingiazo. Wengi wao huenda kufanya “shopping” Dubai au Afrika Kusini.

Vera Sidika: “Mwili wangu ni dili”
Katika kipindi cha The Trend kirushwacho na kituo cha NTV nchini Kenya, Vera Sidika, ambaye amejizolea umaarufu nchini Kenya kutokana na umbile la makalio yake, alisema kuwa huenda kufanya “shopping” ya kati ya dola 10,000 hadi 50,000 (yaani kati ya Tshs. milioni 16 hadi milioni 80). Viatu alivyokuwa amevaa siku hiyo vinagharimu Tshs. milioni 5 na laki 6, na nywele zake za bandia ni Tshs. milioni 3 na laki 7.

Ngozi ya Vera sio ya asili. Ilichubuliwa kitaalamu na akawa mweupe. Vera anajitapa kuwa ubadilishaji wa rangi ya ngozi yake ulitumia zaidi ya shilingi milioni 15 za Kenya (takribani shilingi milioni 300 za Tanzania). Vera anasisitiza kuwa tangu apate ngozi nyeupe, kwake imekuwa “baraka”. Anatengeneza pesa zaidi, na anaalikwa nchi mbalimbali kwenda kusherehesha vilabu vya usiku (club hosting).

Vera anasema kwamba ukimwona klabu ujue amekwenda kutengeneza pesa. Hufanyaje hasa? “Huwa nasimama pale, na kutabasamu, na kupiga picha na mashabiki,” alifafanua. “Mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa,” Vera alijitapa.

Nyuma ya Vera, zipo kampuni za kurekodi video za muziki, wanamuziki, magazeti, redio, vituo vya televisheni, vilabu vya usiku, kampuni za kuzalisha kemikali za kubadili rangi ya ngozi, hospitali za binafsi zifanyazo uchubuaji wa ngozi, kampuni za vipodozi na mavazi ya kisasa, hoteli za kifahari, n.k. Wote hawa humtumia Vera kutengeneza faida.

Lakini tusisahau watu wa msingi wamfanyao binti huyu ajivune: hawa ni wale anaowaita “my fans”, yaani mashabiki wake. Kila siku Vera huweka picha za nusu uchi, zionyeshazo makalio yake, katika mtandao ili kukonga nyoyo za mashabiki wake. Aendapo Klabu hujiachia na kupiga nao picha za “ajabu” ili waendelee kumshabikia. Mashabiki hawa pia tayari wamekwishatekwa na mfumo, nao wakaamini juu ya urembo utokanao na kuwa na umbo kama la Vera.

Mtandao wa Kibiashara
Zipo nchi nyingi, mathalani Venezuela na Ufaransa, ambako ukuzaji-makalio na matiti vimetia fora kiasi cha wananchi kuzipigia serikali zao kelele ili zidhibiti vitendo hivyo. Lakini hii ni kazi bure kama tusipoelewa kiini cha tatizo lenyewe.

Gazeti la mtandaoni liitwalo “The Revolution” linalomilikiwa na Chama cha Kikomunisti cha Marekani liliwahi kufanya uchambuzi wa biashara ya upachikaji wa matiti ya bandia kwa wanawake. Nchini Uingereza pekee kati ya wanawake 20,000 hadi 30,000 hukuza matiti kwa njia hiyo kila mwaka, na biashara hiyo huingiza pato la zaidi ya dola milioni 150 (takribani shilingi bilioni 240 za kitanzania) kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa plastiki nchini Marekani, idadi ya watu wanaojihusisha na upasuaji wa plastiki iwe ni katika kukuza au kupunguza makalio, matiti, nyusi, nywele, kubadili sura au ngozi, imeongezeka kutoka watu milioni 7.5 mwaka 2000 na kufikia watu milioni 14 mwaka 2011.

Jarida la “The Revolution” linaripoti kuwa kampuni za utengenezaji kemikali za ukuzaji matiti hutumia kemikali bandia ili kutengeneza faida zaidi. Moja ya kampuni hizo ni Poly Implant Prothese (PIP) ya nchini Ufaransa. Kutokana na madhara makubwa ya kiafya yasababishwayo na kemikali za PIP, baadhi ya nchi zimejaribu kuzipiga marufuku bidhaa za kampuni hizo bila mafanikio.

Maslahi ya kibiashara hayaishii katika kampuni tu. Ubidhaishaji wa huduma za afya umezifanya hospitali nyingi za binafsi zijiingize katika kazi ya upasuaji wa plastiki ili kukuza au kupunguza viungo vya mwili. Wateja waliopata madhara ya kiafya kutokana na kemikali za kukuza matiti na makalio wamekataliwa na hospitali zilizowapa huduma hizo. Wamiliki wa hospitali hizo, kwa mujibu wa jarida la The Revolution, “wanadai kuwa hawapashwi kuwajibishwa kutokana na kununua bidhaa zilizokuwa sokoni.”

Ubepari: toka uzalishaji hadi ubidhaishaji
Pengine cha kufikirisha ni kauli ya Vera kuwa “mwili wangu ni biashara yangu na ninautumia kutengeneza pesa”. Suala la kujiuliza ni kuwa, je, tangu lini mwili wa binadamu uligeuka kuwa bidhaa, hata ukatumika kutengeneza pesa?

Katika kitabu chake cha Das Kapital (Capital au Mtaji) kilichochapishwa mwaka 1867, Karl Marx aliubainisha ubepari kama mfumo unaojitambulisha kupitia bidhaa. Lakini bidhaa hizo ni zile zinazozalishwa na nguvu ya binadamu na kupelekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa. Cha kushangaza ni kuwa watu hushikwa na wazimu wa bidhaa, wakazipenda na kuzithamini, lakini wasione kiini ndani ya bidhaa hizo. Kiini hicho ni nguvu-kazi ya binadamu iliyotumika kuzitengeneza. Marx alifariki mwaka 1883, yapata miongo saba baada ya Sarah kufariki. Kipindi alichoishi Marx kilikuwa ni kipindi cha ubepari wa uzalishaji bidhaa, viwandani na mashambani.

Takribani karne moja na nusu baada ya kuchapishwa kwa Das Kapital, Prof. Issa Shivji, mmoja wa wanazuoni wa Kimaksi, ameandika kuhusu ubepari wa karne ya 21, ambao umechukua sura ya uliberali mamboleo. Mfumo huu hautegemei tena uzalishaji, bali ubidhaishaji wa kila kitu.

Vitu ambavyo kwa asili yake haviwezi kuuzwa, hugeuzwa bidhaa na kuuzwa sokoni. “Utengenezaji wa bidhaa-sesere na zisizo za asili hauna mipaka katika mfumo wa uliberali-mamboleo,” anaandika Shivji katika kitabu chake kiitwacho Accumulation in an Afriacan Periphery. “Mazingira, ikolojia, na viumbe vingine wa asili (wanyama na mimea), viini vya kibaiolojia (ute wa mimea na viini-tete vya binadamu) hugeuzwa kuwa bidhaa, hali ambayo hutokea pia katika hisia na raha zihusishazo mahusiano ya kimwili. Juu ya vitu na mahusiano halisi hutengenezwa vitu-pepe na mahusiano-pepe, ambavyo pia hubidhaishwa. Katika ulimwengu wa mahusiano utaona mambo kama mabinti wa mtandaoni, vyumba vya faragha, na ufanyaji-mapenzi katika mtandao” (tafsiri yangu).

Kwa hiyo, tujifunzacho hapa ni kuwa mtandao wa watumiao miili ya vijana, na hasa wa kike, kutengeneza pesa ni mpana: vituo vya televisheni huwaalika katika mahojiano na kueneza udaku juu yao na kwa kufanya hivyo hutengeneza pesa, magazeti ya udaku hutengeneza pesa kwa kuchapisha picha na stori za mabinti hao, kampuni za utengenezaji wa kemikali za ukuzaji makalio/matiti na uchubuaji ngozi nazo hutengeza pesa, hospitali zijihusishazo na uchubuaji ngozi na upasuaji wa ukuzaji makalio hutengeneza pesa, na vilabu vya usiku viwaalikao mabinti hao navyo hutengeneza pesa, n.k. Huu ni mtandao mkubwa wa kutengeneza pesa katika zama hizi za utumwa mamboleo.

Kiini cha mtandao huu ni mfumo wa uliberali mamboleo, ambao ni aina ya ubepari uliofilisika na uliochukua sura ya kikatili ya ubidhaishaji wa kila kitu, yakiwemo maumbile ya binadamu! Mfumo huu hauwezi kuwekewa viraka kwa kuhubiri juu ya maadili kwa vijana. Ni ama tuubomoe, au tuuache uendelee kutubomoa kwa kugeuza hata miili yetu kuwa bidhaa. Kama wapigania uhuru wa bara la Afrika walipambana dhidi ya ukoloni, sisi wajukuu wao hatupashwi kusalimu amri. Hatuna chaguo mbadala, ni jukumu letu sote kupambana dhidi ya uliberalimamboleo.

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com

Launched: Kijiwe cha Watoto cha Usomaji


Thursday, June 26, 2014

Kupasuka kwa Vyama na Hatma ya Demokrasia

Tanzania na Afrika Kusini ni nchi zenye mambo mengi yanayofanana. Nyimbo zetu za taifa hazina tofauti sana. Hali kadhalika bendera zetu. Na hata baadhi ya lugha zetu.

Vyama tawala vya nchi hizi mbili navyo vinaendelea kushika hatamu licha ya kukua kwa vyama vya upinzani toka miaka ya 1990. Hata historia ya mipasuko ya vyama nayo inafanana kiasi.

Baada ya tofauti za kimtazamo na kimbinu katika miaka ya mwanzo ya 1960, mwanasiasa machachari Zuberi Mtemvu na baadhi ya wanachama wenzake wa Tanganyika African National Union (TANU) waliunda chama cha African National Congress (ANC).  Chama chenye jina kama hilo huko Afrika Kusini, yaani ANC, nacho kilikumbwa na tofauti katika miaka ya mwisho ya 1950 na kupelekea kuundwa kwa chama cha Pan Africanist Congress (PAC) chini ya mwanasiasa mahiri, Robert Sobukwe. 

Migawanyiko, ama mipasuko, ya vyama vya kisiasa inaweza kuwa chachu ya kukuza demokrasia au ya kudidimiza harakati za ukombozi. Ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani ANC ya kina Mtemvu ingetusaidia kwa lipi maana baada ya kumpa Mwalimu Julius Nyerere na TANU changamoto kwenye uchaguzi mkuu wa 1962 haikupata tena fursa hiyo mwaka 1965 kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa chama kimoja eti ili kudumisha umoja. 

Wenzetu wa Afrika Kusini wao wanajua kwa kiasi gani PAC iliwasaidia ama kutowasaidia katika harakati zao. Wapo wanaoona kuwa ilidhoofisha na kuchelewesha kupatikana kwa demokrasia kwa kuwa nchi za Afrika ziligawanyika kuhusu nani wa kumsaidia - ANC au PAC? Utata huu umegusiwa katika wasifu wa Nelson Mandela wa Long Walk to Freedom anapoelezea alivyogundua jinsi gani PAC ina mvuto Afrika na ambavyo imekuwa ikiifanyia majungu ANC alipozuru nchi yetu na nchi zingine na hivyo kuifanya kazi yake ya kutafuta ushirikiano wetu kuwa ngumu.

 Lakini ndio hao hao PAC waliosimamia, japo wengine wanadai kudakia, harakati za kupinga kulazimishwa kutembea na pasi za kibaguzi. Japo baadhi ya wanaharakati hao waliuliwa katika mauaji yanayojulikana kama Sharpville Massacre mwaka 1960, harakati zao zilikuwa chachu kubwa katika kuleta demokrasia nchini kwao.

Historia ya wenzetu kwa kiasi fulani sasa inajirudia. Mwaka 2008, kabla ya uchaguzi mkuu uliopita, wanasiasa kadhaa wa chama cha ANC walianzisha kwa makeke chama chao na kukibatiza jina la lililokuwa vuguvugu muhimu katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo kutokana na kupitishwa kwa kwa Freedom Charter (Azimio la Uhuru) huko Kliptown mwaka 1955, yaani Congress of the People (COPE). Wapo waliotegemea kitakipa chama tawala changamoto kubwa na kukifanya kisiweze kuhodhi maamuzi ya kibunge n.k. Lakini migongano ya kiwasifu pamoja na kugombania madaraka kati ya vinara wake wakuu wawili kati ya watatu, Mbhazima Shilowa na Mosiuoa Lekota, ilichangia kukidhoofisha chama hicho.

Kuibuka kwa chama kingine cha Economic Freedom Fighters (EFF) kilichoundwa na vijana matata waliojikuta hawana jinsi ila kutoka ANC nako kumechangia kufifia kwa COPE. Chama hicho kipya kinachoongozwa na mwanasiasa maarufu, Julius Malema, hakina hata zaidi ya mwaka 1 ila kimeweza kujizolea kura zipatazo milioni 1 katika uchaguzi mkuu wa 2014. Kwa lugha ya mtaani ya vijana, kinakipumulia kooni chama kikuu cha upinzani nchini humo, Democratic Alliance (DA) kinachoongozwa na mwanasiasa  mwerevu, Helen Zille, na huenda muda wowote kikawa chama kikuu cha upinzani na hata kuchukua dola kwenye chaguzi zijazo.

Chama hicho ambacho maana ya jina lake ni 'Wapigania Uhuru wa Kiuchumi' kimevuta hisia za vijana wengi wa hali ya chini na hata ya kati. Pamoja na kiongozi wake mkuu kuonekana ni mkaidi na mkwasi, anaendelea kujizolea wafuasi wakiwamo wasomi. Profesa mmoja katika chuo kikuu maarufu huko Johannseburgh aliwahi kusikika akisema kuwa ni jambo la kushangaza, na linalostahili kuchunguzwa, kuwa wanafunzi wake wengi makini wa shahada ya uzamivu ni wanachama wa chama hicho cha 'mtata' Malema.

Ni nini kinawavuta Dali Mpofu, mwanasheria msomi, na wenzake kujiunga na chama kinachozungumza lugha ya kijamaa/kisoshalisti japo inaonekana ni dhahiri kuwa kiongozi wake mkuu ana ukwasi wa kibepari/kifisadi? Ni nafasi rahisi ya kukuza demokrasia? Je, ni fursa ya kupata sifa na madaraka makubwa ya haraka haraka?

Au ni mvuto tu wa mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kuongea na wananchi wa kawaida na ushawishi mkubwa kwa umma? Kama ni mvuto huo wa halaiki ambao wataalamu wa sayansi ya siasa wanauita upopulisti, je, una nafasi gani katika kukuza demokrasia ndani ya chama hicho na nchi yao kwa ujumla?

Hapa kwetu Tanzania tuna nini cha kujifunza kutokana na migawanyiko/mipasuko ya vyama vya kisiasa huko Afrika Kusini? Katika makala ya Kutoka 1995 Kuelekea 2015 tulirejea kidogo historia ya mtafaruku wa NCCR uliopelekea kufunguliwa kwa kesi katika mahakama kuu ili kutatua ugomvi wa madaraka katika ya kundi la Augustine Mrema na kundi la Mabere Marando. Ni vyema tukaichambua kwa kina historia hii na ya mitandao ya CCM katika muktadha wa leo ili tujielewe badala ya kuwa bendera fuata upepo.

Kwa wale wanaoamini kuwa Mwalimu Nyerere alitabiri kuwa upinzani thabiti utatoka CCM basi pengine huu ndio wakati mwafaka wa kuhakikisha chama tawala kinapasuka katikati na ikiwezekana mpasuko huo uzae CCM-Safi na CCM-Fisadi. 

Na kwa wale wanaomini kuwa vyama vya upinzani ndio mwokozi wa demokrasia basi labda wakati ndio huu wa kuleta mipasuko mikubwa katika vyama vinavyoakisi ukiritimba/urasimu wa chama tawala ili kuzalisha vyama vyenye demokrasia na uwazi zaidi.

Lakini wale wanaomini kuwa demokrasia ya kweli haitokani na siasa za vyama bali mavuguvugu ya wananchi wakati ndio huu wa kutafakari na kuchukua hatua kuhusu hatma ya demokrasia yetu.

Africa

Loading...

Tanzania

Loading...

Dar es Salaam

Loading...
Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP