Loading...

Thursday, December 13, 2007

Wadadisi wa Nyamagana kutinga kortini!

Lile sakata la Nyamagana ambalo lidadisiwa jana katika blogu hii inasemekana limechukua sura mpya. Kwa mujibu wa The Citizen la leo wakazi wapatao 8 wa Mwanza watatinga kortini kesho ili kuzuia ujenzi wa hoteli ya 'nyota tano' inayotaka kujengwa na wawekezaji katika uwanja huu wa umma.

Kama ilivyokuwa enzi za mkoloni wa kale ambapo kwa namna moja au nyingine wananchi walipambana ili kulinda rasilimali zao hasa rasilimali 'mama', yaani ardhi, basi ndivyo ilivyo leo katika enzi za ukoloni mamboleo. Wakati wapo watu wanaoamini kuwa hakuna linalowezekana bado wapo wananchi ambao wanaamini kuwa hakuna lisilowezekana. Imani hii wameijenga kutokana na jinsi ambavyo historia ya kale na ya leo inavyoonesha kuwa inawezekana.

Kwa mfano kundi hili la wakazi wa Mwanza linanunukuliwa likisema kuwa licha ya kwenda kortini pia litatumia 'Nadharia ya Msitu wa Mabira' wakati wa mapambano ya kundi lao linalojiita 'Okoa Uwanja wa Nyamagana'. Kwa wale wafuatiliaji wa harakati za kulinda rasilimali basi watakumbuka kilichotokea mwaka huu huko Uganda ambapo wananchi wenye uchungu na nchi yao walisimama kidete kupinga jaribio la kuuza eneo la msitu wa Mabira kwa mwekezaji wa kigeni.

Wakati huohuo mahakama ya rufaa imeizuia kampuni ya simenti kuzihamisha familia 1,000 kutoka kwenye kijiji cha Chasimba. Hii nayo inathibitisha kuwa mapambano ya haki huzaa matunda. Hakika huu ni wakati wa wadadisi kuudadisi mfumo wa mgawanyo wa madaraka nchini na kupambana ili mahakama iwe na uhuru na nguvu ya kuhakikisha maamuzi yake yanatekelezwa bila kutoingiliwa na zile nguzo zingine' mbili za utawala, yaani 'Bunge' na 'Serikali'!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP