Loading...

Wednesday, February 13, 2008

Wasifu wa Waziri unaendana na Wizara?

Sifa kemkem zinazidi kumiminika kutoka kila kona baada ya Rais wa Tanzania kutangaza baraza jipya la mawaziri jana alasiri. Hata hivyo, wadadisi wa mambo nao wameanza kutoa tahadhari kuhusu baadhi ya mawaziri ambao wamebakia. Pale panapostahili sifa panahitaji ukarimu wa pongezi. Na pale panapohitaji ukosoaji panastahili ujasiri wa ukosoaji. Hii ndio kazi kuu ya Udadisi.

Hakika Rais anastahili pongezi kwa kuchagua baraza dogo ukilinganisha na lile alilokuwa nalo kabla ya sakata la Richmond kulipuka Bungeni. Pia anastahili pongezi kwa kuunganisha baadhi ya wizara na kudhamiria kuijenga ofisi ya Mwanasheria Mkuu iwe huru na yenye nguvu. Hata hivyo, pongezi hizo hazimaanisha kuwa tumeshafika huko tuendako. La hasha, ndio kwanza tumeanza. Na kama mdau mmoja anavyosema kwa lugha ya kigeni, "this is a step, but not a leap, forward" yaani 'tumepiga hatua tu ya kusonga mbele ila hatujaruka kwenda mbali.'

Naam bado tuna kazi nzito hasa ukizingatia kuwa wasifu wa baadhi ya mawaziri bado hauendani na wizara walizopewa. Nasema hivi kwa kuwa sikubaliani na kiongozi mmoja wa zamani wa Serikali aliyewahi kuniambia kuwa waziri ni kiongozi tu wa kisiasa hivyo haijalishi kuwa ana taaluma gani. Kwa kweli katika dunia ya leo ambapo taaluma, ufahamu na taarifa ndio nyenzo muhimu za kuleta maendeleo kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa mawaziri wetu wanajua kwa undani wa kitaaluma dhana kuu za wizara zao.

Mtazamo huu unamaanisha kuwa Rais amefanya vyema kuchagua naibu waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambaye ni Mhandisi mwenye utaalamu na uzoefu mkubwa wa kusimamia na kuendesha miradi ya maji na umwagiliaji. Hii pia inamaanisha kuwa anastahili pongezi kwa kumchagua Waziri wa Nishati na Madini ambaye amebobea katika masuala ya kisheria katika sekta ya biashara za makampuni ya kimataifa (multinationals) ambayo mpaka sasa ndio yananufaika sana na madini yetu kupitia mikataba mibovu.

Kwa upande mwingine, umuhimu huu wa kuhakikisha kuwa wasifu wa kitaaluma wa waziri unaendana na wizara una maana kuna walakini katika wizara ambazo zina dhana nyeti kama ya 'Decentralization by Devolution' (Upelekaji wa Madaraka katika Ngazi za Chini) na dhana ya 'Land and Resource Rights' (Haki za Matumizi ya Ardhi na Maliasili zake). Je, wasifu wa wawaziri wa wizara zinazosimamia utekelezaji wa dhana hizo, unaonadiwa katika tovuti ya Bunge, http://www.parliament.go.tz/, unaendana na wasifu wa wizara zao? Je, wataweza kusimamia kitaaluma masuala haya au watayasimamia kikamanda au kisiasa tu na pengine kuturudisha kwenye sakata kama lile la Richmond ambalo liligubikwa na 'Ujasiri wa Kifisadi' uliodharau ushauri wa kitaalam?

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP