Loading...

Sunday, May 25, 2008

Mkahawa wa Vitabu wa Soma


Kampuni ya uchapishaji ya E & D LTD iko mbioni kuzindua shirika la kukuza usomaji na maendeleo mnamo tarehe 6 - 13 Juni 2008. Tukio hilo litakalochukua juma zima litafanyika katika 'mkahawa wa vitabu' (book cafe) wa Soma ambao nao utazinduliwa rasmi wakati huo mara tu baada ya ujenzi wake kukamilika rasmi. Mkahawa huo upo Mikocheni Reagent sehemu ya Mlingotini Closure.

Usomaji unaoongelewa hapa sio usomaji wa vitabu na ripoti tu, bali ni usomaji wa fasihi (literature), sanaa (art) na utamaduni(culture) wa jamii kwa ujumla katika namna iliyo pana zaidi. Usomaji wa aina hii unaichukulia jamii kama kitabu ambacho wanajamii wanashirikiana katika kukiandika na kukisoma kwa njia mbalimbali kama vile kwa kutunga au kusikiliza hadithi, mashairi, nyimbo na ngoma; kuandaa au kutazama vipindi kwenye runinga (television) na jukwaani (theatre); kuumba au kupitia maandishi na vielelezo kama vile picha na vinyago (sculptors).

Ni dhahiri kuwa usomaji huu mpana utachochea vuguvugu (movement) la kuibua, kukuza, kuhamasisha na kuenzi aina zote za fasihi, yaani fasihi andishi na simulizi. Historia inadhihirisha kuwa kuna uhusiano wa kina kati ya vuguvugu la aina hii na maendeleo ya jamii husika kwa ujumla. Hivyo basi itakuwa vyema kama tutatumia fursa hii kwa namna moja au nyingine ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya jamii yetu.

Soma inakaribisha mtu yoyote ambaye anajisikia kujitolea kushiriki katika kuwezesha au/na kuandaa baadhi ya programu za vuguvugu hilo. Programu mojawapo itakuwa ni ya kuandaa wasifu (profiles) wa wanafasihi kama vile waandishi wa vitabu, wasimulizi, waigizaji na waimbaji. Kila juma kutakuwa na tukio katika 'mkahawa wa vitabu wa soma' ambalo litakuwa limejikita katika wasifu wa mwanafasihi wa juma hilo. Wigo wa namna ya kuandaa wasifu ni mpana na unategemea mawazo na ubunifu (creativity) wa mtu atakayejitolea kuandaa wasifu huo. Hivyo, unaweza kuwa nia makala gazeti, kipindi katika runinga na kadhalika. Inatazamiwa kuwa katika kila juma angalau kutakuwa na wasifu mmoja katika gazeti la Kiswahili au/na la Kiingereza.


"Tunakaribisha vikundi mbalimbali vyenye nia ya kuvinjari nyanja zote za kijamii na kiutamaduni na umuhimu wake kwetu kihistoria pamoja na kwa mstakabali wa jamii yetu; ikiwa ni pamoja na maisha na mahusiano yetu ya kijamii yalivyo hivi sasa. Tungependa kupata tarehe na andiko fupi—aya moja au mbili zinazoelezea mada pamoja na majina ya wawezeshaji wakuu/watoa mada na anuani zao kwa ajili ya ufuatiliaji—sababu nyngine ni kutuwezesha kuandaa na kusambaza ratiba kila mwezi. Karibuni sana." - Demere Kitunga, Mkurugenzi Mtendaji wa E & D Ltd na mratibu wa Soma Book Cafe

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP