Loading...

Thursday, July 3, 2008

Rais ni Kilongola!


Tazama ni jinsi gani inavyopendeza kuona Rais wetu akisoma kwa makini, tena mbele ya kadamnasi, ripoti ya Afrika kuhusu namna ya kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia kabla ya 2015. Picha hii iliyopigwa huko Misri kwenye mkutano wa AU iliupamba ukurasa wa mbele wa gazeti la Majira la jana na Tovuti ya Magazeti ya Serikali. Picha hii imenikumbusha mahojiano/taarifa ya Dk. Asha-Rose Migiro (pichani) wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuhusu moja ya ziara za Rais kule USA. Mama Migiro aligusia kuwa pamoja na kubanwa sana na ratiba ya ziara, Rais alitafuta upenyo na kwenda katika mitaa ya huko ughaibuni kununua vitabu.

Tukio hili pia limenikumbusha ila dhana ya 'Kilongola' ambayo iliingizwa katika misamiati yetu pale Bungeni na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla kulazimika kujiuzulu Kutokana na lile sakata la Richmondgate, Dk. Ibrahim Msabaha. Kwa ufupi, Kilongola ni mtu anayewaongoza wenzake katika jambo fulani muhimu. Tena kama anavyosisitiza Jenerali Ulimwengu katika makala yake ya Kazi ya 'Kilongola' kuonyesha njia, huwa inakuwa vyema mtu huyo akiwaongoza wenzake kwa vitendo na sio kwa maneno tu.

Tanzania yenye utamaduni wa kusoma inawezekana. Rais wetu anaonyesha njia. Risala zake zinadhihirisha ni kiasi gani Rais na wasaidizi wake wana utamaduni wa kusoma. Rais ndiye Kilongola wa kuivunjilia mbali ile dhana mgando ya kwamba ukitaka kumficha Mwafrika jambo fulani basi liweke katikati ya kitabu, yaani, kwenye maandishi. Tumuunge mkono. Na kama vitabu tulivyovitumia darasa la kwanza enzi zile vinavyotukumbusha, tusome kwa furaha!

2 comments:

Anonymous July 3, 2008 at 10:51 AM  

asante chambi kwa kutuletea matukio mbalimbali yanayotufanya tutoe maoni yetu.
Kwangu mimi ninavyomchukulia rais wetu ni mtu asiyependa kujisomea. mara nyingi katika mahojiano ya papo kwa papo huwa hana majibu yanayoridhisha- hana details, hujibu kisiasa saana. Hivyo siwezi kusema kama ni mfano bora sana wa mtu anayependa kujisomea. Pamoja na ya yote, awe anapenda ama hapendi kujisomea bado anawajibu wa kutuongoza sawa sawa na matumaini yetu, na hiyo ndiyo Changamoto kubwa iliyopo mbele yake.

aidanmmari@yahoo.com
Mwanaharakati.

Freddy Macha July 7, 2008 at 2:38 AM  

Chochote kinachoonyesha mambo ya kusoma,vitabu, maandishi badala ya magari, majumba na vitu visivyopatikana kwa mtu wa kawaida kinafaa kutukuzwa.
Mada ambayo ndugu Chachage anaongelea (nahisi) inahusu saikolojia. Kuwa taswira inayotolewa na picha ya viongozi hawa wawili (Rais Kikwete na Mama Migiro) ni ipi: Taswira. Picha. Maana. Mambo yanayoelemisha bila kusema.
Pia si vibaya kutaja kuwa Bongo tungekuwa na tuzo za zawadi kwa picha bora za waandishi wa habari hii ingekuwa miongoni na kilingoni.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP