Loading...

Monday, July 14, 2008

Wasomi ni Makuwadi,Wakombozi au Wahuni?

Kwanza kabisa nimpongeze ndugu Halima Mkutambilu wa Kawe, Dar es Salaam kwa kuweka wazi hisia zake juu ya Wasomi wa Tanzania. Katika barua yake kwa Mhariri, Mtanzania la Alhamisi 12 Aprili 2007 yenye kichwa cha habari “MBEKI HAWA NI WASOMI WETU”. Ameweka wazi hisia na matamanio ya wananchi walio wengi kwa wasomi pamoja na mtazamo wao kwa hili kundi dogo ambalo kwa sehemu kubwa limefika hapo lilipo kwa kodi za wananchi.

Kwa ufupi, katika barua hiyo wasomi wanalaumiwa kwa kuifikisha nchi hii pabaya na kuisababishia matatizo makubwa. Sifa za kundi hili zimeainishwa kuwa ni ujivuni, kupenda kula, ufisadi na kuwa mihuri inayotumika kuwekwa hapa au pale na kuacha alama ambayo huja kuwa maumivu makubwa kwa wananchi. Sina budi kuunganisha uchambuzi huu na changamoto mbalimbali zilizotolewa na wachangiaji mbalimbali katika siku ya kumbukumbu ya Hayati Kamaradi Chachage, Usiku wa Chachage pale Chuo Kikuu Dar es Salaam tarehe 8 Julai 2008 juu ya nafasi ya wasomi katika kuleta mabadiliko.

Inawezekana hii ikachukuliwa kama mzaha fulani na labda wivu wa watu wenye mtizamo hasi dhidi ya wasomi. Lakini bila shaka ni wakati muafaka kwa wasomi kutafakari na kuangalia nafasi yao upya katika ujenzi wa Taifa. Labda tuchukulie mifano michache inayoweza kuwa imechukuliwa; ni nani aliyesaini mikataba mibovu iliyotufikisha hapa tulipo? Ni nani washauri wa Serikali katika mambo mbalimbali, ya siasa, uchumi, jamii n.k.? Pamoja na wanasiasa, ni viongozi wetu katika kada mbalimbali. Hawa wote kwa namna moja ama nyingine wanaunda kundi la watu wanaoitwa wasomi. Swali la kuongoza tafakari ni: Je, kazi zao na yote wayafanyayo ni kwa maslahi na manufaa ya nani?

Katika moja ya tahariri zake Mhariri wa jarida la Ardhi ni Uhai, linalotolewa na Taasisi ya HAKIARDHI Mhariri aliongelea kwa kirefu juu ya wasomi na nafasi zao mbalimbali katika jamii yetu sasa. Katika kujenga hoja yake alitoa mfano wa Susi na Chuma watumishi waaminifu wa Dk. David Livingstone, Raia wa Uingereza aliyekuwa na kazi kubwa tatu; kueneza injili ya Kikristo, kuifungua Afrika kwa ajili ya Wafanyabiashara na Mabepari wa Ulaya na kueneza Ustaarabu wa Kimagharibi miongoni mwa 'Washenzi'. Sote tunatambua madhara ya kazi zake, ukoloni na umaskini tunaoendelea nao mpaka sasa. Hawa ndugu Susi na Chuma uaminifu wao haukuwa na kipimo! Walimtumikia na kumbeba kila alikotaka kwenda akiwa hai au amekufa. Pengine wangebaini madhara yake bila shaka wasingeendelea kumbeba na kumzungusha.

Kama tulidhani akina Susi na Chuma wamekwisha twajidanganya! Kwani wapo akina Susi na Chuma mamboleo, kwa kujua ama kwa kuongozwa na tamaa na ubinafsi wanautumikia ubeberu katika mfumo wake wa utandawazi kwa njia na mbinu mbalimbali. Hawa wapo katika sekta binafsi na ya umma. Wamo serikalini wakibariki sera na sheria za kuuza nchi. Wanapatikana katika NGOs wakifanya harakati zenye kusaidia uhalalishaji wa sera na sheria zinazouza nchi na kudhalilisha utu na uhuru wetu. Pia wapo wale ambao wapo kwenye vyuo vya umma na binafsi, wasomi ambao wanashauri kwa sababu ya tamaa ya fedha wakijua madhara yake kwa jamii.

Akina Susi na Chuma wa kisasa ni changamoto kubwa sana katika jamii yetu leo hasa ukizingatia kuwa kwa lugha na mbinu mbalimbali wamejitambulisha kama wakombozi wa wanyonge. kwa sehemu kubwa pamoja na usaliti wao wananchi wengi bado wanawaamini hawa wanazuoni na wasomi na wana matumaini na kundi la pili linalojiita wanaharakati! Wengi wa wananchi kama ndugu yetu Halima Mkulambilu wanapobaini kusalitiwa hulalama na kusema “WASOMI MNATUANGUSHA’!

Ni kweli kwamba mchango wa wasomi katika kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii unatambulika na kuheshimika na watu wengi wa kawaida. Hata hivyo, ni vigumu kwa walio wengi kutofautisha kati ya wasomi, wanazuoni na wanaharakati wauza nchi na makuwadi (kama awaitavyo hayati Prof. Chachage) wa ubeberu na kundi la pili la Wasomi, Wanazuoni na wanaharakati wanaolinda na kuendeleza nchi na wananchi.

Njia rahisi ya kuyatofautisha makundi haya mawili ni kuangalia mchango wao katika ukombozi wa watu wanyonge. Je, wanashirikiana na watu ili wajikomboe wenyewe au wanataka kuteka harakati na kujinadi kuwa wao ndio wakombozi! Wanachukulia matatizo ya watu kama fursa za kijasiriamali kwa ajili ya maendeleo binafsi? Badala ya kusema samaki mmoja akioza tenga zima ni minyoo lafaa kutupwa nadhani ni vyema tukawa makini kuchambua ili tubaini waliooza na ambao bado wapo safi. Ukombozi wa kweli wa watu utaletwa na watu wenyewe, pale tunapowabaini wasaliti tuwaweke hadharani na tuwaumbue tusiogope.

Ni mara ngapi ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wasomi wetu umekataliwa na Serikali na ni wangapi wamesimama kuhoji maamuzi ya Serikali, kwa mfano katika mambo makubwa yafuatayo: Mikataba ya Richmond na IPTL; Ujenzi wa Maghorofa ya BOT; Ununuzi wa Rada; Uuzwaji wa NBC; Tuhuma za Manji NSSF; Ununuzi na Ulanguzi wa Korosho; Ununuaji wa ndege ya Rais na kejeli za Mramba; Pato duni kutoka katika sekta ya madini; Kunyanganywa uraia kwa baadhi ya wananchi na baadhi ya NGOs kufungiwa? Pamoja na mambo mengi kuwekwa wazi katika vyombo vya habari na baadhi ya wasomi kuongelea juu ya masuala hayo bado jamii kwa ujumla ama imekaa kimya kwa kuona mambo hayawahusu ama kwa sababu ya kulindana kichama ama kwa kuendeleza ile tabia ya kuwaona viongozi wezi ni wajanja wanaojua kutumia nafasi zao na kuwaona waaminifu na waadilifu ni watu wa ajabu.

Mwanazuoni mmoja aliwahi kusema kwamba mabadiliko ya kweli yataletwa na wananchi wenyewe kwa kuangalia kwa ukaribu matendo ya viongozi wanaowachagua na kuwawajibisha pale wanapotenda kinyume. Kama wasomi wamekuwa ni wasaliti basi hatuna haja ya kuwategemea. Kwa umoja wetu na wingi wetu tukiamua kuleta mabadiliko ya kweli tunaweza. Umoja ni nguvu wingi ni uwezo.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP