Loading...

Tuesday, September 2, 2008

Kicheko cha JK funzo la uvumilivu!


Hakika vichekesho na vicheko vinahitajika sana katika jamii. Huleta furaha na faraja. Pia hupunguza makali na masaibu ya maisha.

Hata wanasaikolojia wamedhihirisha kuwa hali ya kufurahishwa hutusaidia tuwe na mzunguko mzuri wa damu. Pia husaidia kuzalisha chachu ya kuchochea bongo zetu. Hali hii hutufanya tuweze kuwa wepesi wa kufikiri, kukumbuka na kutenda.

Hali kadhalika misahafu mbalimbali husisitiza umuhimu wa kufurahi na kufurahishana. Kwa mfano msahafu wa Kikristo unanena waziwazi kuwa “moyo uliochangamka ni dawa nzuri; bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.” Pia unatuhimiza tuwape cha kuwafurahisha wale walio na uchungu nafsini ili wausahau umaskini wao na taabu yao.

Hivyo, basi, hatuna budi kumshukuru Jalia kwa kutupatia Rais mwenye uwezo wa kucheka na kutuchekesha. Naam si viongozi wetu wa dini wametuhakikishia kuwa Rais wetu ni chagua la Mungu. Tena na msahafu mmojawapo unasisitiza kuwa kila mamlaka hutoka kwa Maulana.

Hotuba ya Rais aliyoitoa Bungeni hivi karibuni imezua mjadala mkali. Wapo waliokerwa sana na kile ambacho Rais alikisema au kutokisema. Hawa hawakucheka hata kidogo wakati wote wa hotuba. Pia wapo waliofurahishwa sana. Hawa wamelazimika kuandamana kumpongeza Rais.

Hapo katikati tupo tuliocheka huku tunalia. Sisi ndio wale ambao ule msahafu unatusema kuwa hata “ wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.” Hisia zetu ni tete tena ni tata. Ni vigumu kwetu kucheka bila kulia hata tunapotazama Ze Komedi.

Hulka na haiba ya Rais wetu hakika imefanya awe na umaarufu wa ajabu. Umaarufu wake umefanya watu wambatize majina kedekede, likiwamo la JK. Yeye mwenyewe, kwa utani uliotuchekesha wenye vicheko vilivyo karibu, ameongeza orodha ya majina yake pale aliposema ‘Mabilioni ya Bwana Fulani’, akimaanisha ‘Mabilioni ya JK’, wakati wa hotuba yake.

Hapa alikuwa anaongelea zile fedha – ama tuziite vijisenti – ambazo zinatolewa kwa kila mkoa kwa ajili ya kuwawezesha wakazi wa mikoa hiyo. Ilibidi Bwana Fulani atenge dakika kadhaa kutoka kwenye takribani dakika 180 za hotuba yake ili azungumzie fedha hizi ambazo zimekuwa gumzo hasa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa vifisadi vimezigeuza kuwa vijisenti vyao.

Huyu ndiye Rais tuliye naye. Ni Rais mwenye ujasiri wa kutuchekesha kuhusu masuala mazito yanayoikabili nchi yetu ili kutupunguzia mzigo tulio nao. ‘Usione majentlomeni wametinga tai mtaani hali yao ngumu’ na ‘liwa ule’ ni ‘sharbati’ aliyotuonjesha ili kutuliza kiu yetu ya haki.

Hasira hasara. Ndivyo walivyonena wahenga. Naye Rais ametilia sana maanani wosia huu tena kama ulivyo. Ndio maana amesisitiza kuwa ‘tukienda kichwakichwa’ na kuwakamata mafisadi (au ni watuhumiwa tu?) basi Serikali inaweza kuishia kupelekwa mahakamani na kupoteza mamilioni ya fedha. Hasira za mkizi furaha ya mvuvi. Je, hasira za mvuvi furaha ya mkizi?

Huko zamani tuliambiwa Serikali inakwenda hatua kwa hatua. Hata leo bado Serikali inakwenda hatua kwa hatua. Kwetu sisi wenye ‘haraka kuliko upesi’ ni vigumu sana kuwa wavumilivu.

Hebu tutafakari upya ombi alilolitoa JK ‘Tanga Kunani Pale!’ Alituomba tuwe wavumilivu tunapopitia wakati huu mgumu. Lakini uvumilivu hauji hivi hivi tu. Ndio maana vichekesho vya Rais vinajaribu kutuwezesha sisi wananchi tucheke na hivyo kuvumilia ugumu wa wakati huu.

Huu ni wakati ambapo kuna upungufu mkubwa wa chakula duniani. Ni wakati wa bei ya mafuta kupanda hovyo. Naam ni wakati ambapo hata Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta) unakiri kuwa wananchi wengi wanaona kuwa hali yao ni mbaya kuliko Mkukuta ulipoanza 2005 – mwaka wa ule uliokuwa utatu mpya! ‘Choka mbaya’ au sio?

Hizi ni zama za ujasiri wa kifisadi. Lakini hizi pia ni zama za ubwege wa kifisadi. Ni zama ambazo hata kicheko cha fisi mla mizoga kinaweza kumtetemesha simba mla nyama mpaka atapike mzoga. Naam ni zama za kuucheka ufisadi na si kuwachekelea mafisadi.

Hatuna budi kukaza mikanda yetu. Kweli tumelizwa sana na mafisadi. Tukiendelea kulia na kulalama tu hatutaweza kufanya lolote. Tuungane na JK kuchekesha, kucheka na kujichekesha.

Heko JK! Hakika vichekesho vyako vinatufunza mengi. Inahitaji uvumilivu kujicheka. Hahaa!
-------------------

1 comments:

Anonymous September 15, 2008 at 5:31 PM  

JK anachekea mpaka vyura... hana jipya

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP