Wednesday, October 15, 2008

Harakati za Migomo na Utawala wa Sheria

Kwa wale mnaofuatilia harakati za kudai haki kupitia migomo mtakubaliana nami kuwa sakata la walimu kuwapiga mawe viongozi wao jana baada ya viongozi hao kutoa tamko la kusitisha mgomo ni la aina yake. Tamko hilo la uongozi wa chama cha walimu lilifuatia tamko la mahakama kuzuia mgomo huo uliokuwa uanze leo. Walimu waliokuwa wamepandwa na hasira/jazba walichukua sheria mkononi na kuna kila dalili kuwa kama vyombo vya dola/sheria visingeingilia kati basi hata uhai ungeweza kutolewa. Ikumbukwe kuwa hivi karibuni wafanyakazi wa benki ijulikanayo kama NMB walilazimika kukubali kuwa sheria ni msumeno kwa kusitisha mgomo wao baada ya 'agizo' la mahakama.
Baadhi ya maswali ya kujiuliza katika kipindi hiki ni: Tunapaswa kufanya nini ili kuhakikisha kuwa harakati za kudai na kulinda haki zinafanikiwa bila kuvunja misingi ya utawala wa sheria? Ni kwa namna gani tunaweza kujenga mfumo wa utawala wa sheria usioipa nafasi dola kutumia kijanja mianya ya kisheria kupata 'mazuio' ya mahakama yanayorudisha nyuma harakati? Kama mahakama ndio chombo huru cha kutoa haki sawa tunatakiwa kufanya nini ili kuilinda Ibara ya 13 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema "Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria"?

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP