Thursday, November 27, 2008

Yako wapi mapenzi?

Wazuoni nakuja, jamani nisikizani
Mwaweza kutoa hoja, mnitoe matatani
Wasomi mkidhi haja, ya kunitoa gizani
Yako wapi mapenzi?

Nimeenda kwa nyakanga, suluhu sikubaini
Nikapita kwa waganga, nafuu mie sioni
Kwa wanazuoni natinga, muwe langu tumaini
Yako wapi mapenzi?

Mume wangu mi wa kwanza, nilimpenda moyoni
Maisha tuliyaanza, kwa juhudi na imani
Japo shida zilikaza, tuliishi furahani,
Yako wapi mapenzi?

Wakamjia jirani, kumwambia anifuja
Nae akawaamini, uzee hauna tija
Akaniacha njiani, sikupajua kwa kuja
Yako wapi mapenzi?

Nikampata mi wa pili, tukaishi kifahari
Pilau kwa kachumbali, haikuwa na dhohari
Wageni kila mahali, waliuleta ururi
Yako wapi mapenzi?

Utamu wa raha zake, maumivu mwisho wake
Ikatoka hamu yake, kwa mabaya mambo yake
Nikapa sirudi kwake, nae akaenda zake
Yako wapi mapenzi?

Watatu huyu kiboko, japo anao mvuto
Kaniletea vituko, nyumba ikawaka moto
Watoa huko waliko, nyumba kajaza watoto
Yako wapi mapenzi?

Watoto wakawa nduli, mali wanazitafuna,
Kanambia nikubali, nibembeleze vijana
Nami sikuona dili, ndoa ikawa ndoana
Yako wapi mapenzi?

Huyu wanne ninae, nikajua nimepata
Ni mzuri mfanoe, hakuna anaepata
Nilifurahi namie, bingo nimeikamata
Yako wapi mapenzi?

Kumbe ni dalali hali, aso na utu moyoni
Wazee wangu si mali, awatusi hadharani
Wanangu kwake jabali, kulibeba hatamani
Ya wapi mapenzi?

Rafikize makuwadi, iweje na yeye sie
Wafanya ili mradi, ya kwao wayaendele
Hata tupigwe na radi,ngambo ataenda ye
Yako wapi wapenzi?

Talaka hataki nipa, eti anipenda sana
Upenyo tu mkinipa, wima nami namkana
Ila wapi nitapata, wakunipenda kwa sana
Yako wapi mapenzi?

Jamani niambieni, wapi nilipokosea
Au ni ulimbukeni, nambieni nipate jua
Nini sifa yakini, za mume kumtambua?
Yako wapi mapenzi?

© 2008 Mishy Singano

Sunday, November 23, 2008

Kuchukua Hatua Kitu Gani?

Naingia mtandaoni tena kuwadadisi
Naomba mnisikilizeni tena msinidisi
Nijibuni kiuanazuoni wala msinitusi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi

Nawauliza wanazuoni nijibuni basi
Napaswa kufanyani niweze kupasi
Niwaige manyani kupigapiga utosi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi

Nawahoji wakinzani mnaoleta uasi
Niende mahakamani hatua kuiposi
Niwafuate wapinzani kununua kesi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi

Nawadadisi maskini msojali ukwasi
Niingie matatani kuwapigania waasi
Nichukue hatuani kuwapiga mabosi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi

Natoka kilingeni nimejawa utusitusi
Najiona limbukeni aogopaye bisibisi
Niingizeni tanuruni nisiupate uyabisi
Niondoeni kizani unitoke wasiwasi
© Chambi Chachage


Lipi likusumbualo, kalamu kuirukia
Au umekosa mlo, sasa umechukia
Lipi hasa ulonalo, unalolisumbukia
Kama shida ni uhuru, tushapata 61

Amani tulonayo, ni tunu ilotufikia
Usitake mapambano, shimoni tatumbukia
Sijeichokoza leo, kesho hutoifikia,
Kama shida ni uhuru, tushapata 61

Jaribu kujipa moyo, manani takusikia
Kuwa mtu wa maono, lengo utalifikia
Siwachukie vigogo, nchi wameitumikia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Siwatafute wanono, waweza kukuchukia
Mwisho wakakutoa roho, bure kwa kujitakia
Ogopa sana vigogo, chini watakufukia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Wale uwapiganiao, kesho watakukimbia,
Hawatoshiriki mgomo, Wala kukuimbia,
Tena watakaa kando, huku wakijitambia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

We kula ugali wako, ukishiba tajitapikia,
Achana na nia yako, wengine kuhangaikia,
We jali maisha yako, wenye shida wajitakia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Chukua hatua zako, uone utapoangukia,
usitafute maneno, balaa likakufikia,
Mwombe sana Mola wako, 'mana' takushukia,
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Kama hawapendi jambo, hawawezistahimilia,
Madhari wanapata tango, shida wanavumilia,
Siku wakikabwa shingo, mabosi watasimulia
Kama shida ni uhuru, tushaupata 61

Shida zikiwakaba koo, watajua pa kukimbilia
Tena watafanya soo, mabosi watajililia,
Patakuwa ni padogo, mawe yatasimulia,
Kama shida ni 61, uhuru tushaupata?

© Ayub. R.

Sunday, November 16, 2008

Buriani Ben Mtobwa

Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha mwandishi maarufu, Ben Mtobwa ama 'Joram Kiango'. Taifa limepoteza kinara mwingine wa kutumia fasihi andishi kufichua masuala mazito yaliyoigubika jamii yetu. Hivi karibuni nilimwona gwiji Ben pale kwenye Mkahawa wa Vitabu wa Soma akipanga mikakati ya uandishi na uchapishaji.

Nilidhani huo ni mwendelezo wa kumwona mpiganaji huyu akiwa katika harakati za kutumia 'mtutu wa kalamu' kufichua uzandiki na ufisadi katika jamii. Lakini upeo wa mwanadamu una kikomo. Hivyo, sikujua kuwa hiyo ilikuwa mara ya pili na ya mwisho kumwona mwanaharakati huyo ambaye pia alijitosa katika fani ya uhariri wa gazeti la Heko na uchapishaji kupitia kampuni yake ya Heko Publishers.

Nawasihi tumpe mtunzi huyu 'Zawadi ya Ushindi' kwa kusoma kwa undani vitabu vyake ili tutambue ni nini hasa amejaribu kutufunulia 'Nyuma ya Mapazia' ya jamii yetu iliyozingirwa na 'Malaika wa Shetani' na mafisadi wenye 'Roho ya Paka' wanaomsulubisha 'Mhariri Msalabani' na kudiriki kusema 'Najisikia Kuua Tena' kupitia mikataba mibovu wanayoisaini 'Dar-es-Salaam Usiku' pasipo kumwambia mwekezaji uchwara 'Peza Zako Zinanuka' na tena bila kuogopa 'Salamu Kutoka Kuzimu' au kilio chetu cha 'Tutarudi na Roho Zetu?' Buriani Ben Mtobwa!

Saturday, November 15, 2008

Shambani Hanang Kunani Pale?Namshukuru sana Jalia,
Kurejea Darisalama;
Arusha mpaka Manyara,
Mtafiti sikukwama.

Nimejawa na bashasha,
Mrejesho kuutuma;
Wanazuoni wa Taifa,
Usikilizeni umma.

Ardhi yao Wadatoga,
Iligeuzwa chauma;
Nafko lo ikajitwalia,
Ngano kuilima.

Barbaig do akacharuka,
Kortini akasimama;
Dola ikajitetea kijanja,
Sheria ikazifuma.

Ikaleta Operesheni Sogeza,
Wananchi kuwasukuma;
Vijijini wakaswekwa kisasa,
Wakache kuhamahama.

Ujima uendeshwao kiusasa,
Kikaazimia chama;
Utumike kujenga Tanzania ,
Maendeleo kupima.

Mwalimu akauita Ujamaa,
Tukaukubali pima;
Ukahubiriwa kwa harara,
Tukatazamia mema.

Tukalima kwa ushirika,
Pato kulichuma;
Ranchini tukafuga pia,
Kujipatia nyama.

Hatamu chama kikashika,
Utawala ukauma;
Nacho kikaihodhi Katiba;
Watu kuwazima.

Wafugaji wao wakaswagwa,
Kama wanyama;
Mpaka leo wanatangatanga,
Kutafuta neema.

Uchumi nao ukayumbayumba,
Shilingi ikazama;
Wakalisaliti Azimio Zanzibara,
Likapata kiyama.

Hatimaye Nafko ikafilisiwa,
Ikaupoteza uzima;
Wafugaji ardhiyo wakaililia,
Msafara wakatuma.

Kwao Wakuu wakafikia,
Risala wakaisoma;
Wakasihi ardhi kupewa,
Iwahifadhi daima.

Baadhi yao mashamba,
Wakuu wakasema;
Tutawapa enyi wazawa;
Mgawane mazima.

Ila mengine watayawekeza,
Hao wachuma;
Bila ajizi yakabinafsishwa,
Tena himahima.

Wakayanadi pia matirekta,
Navyo vyuma;
Hata maji wakayabinafsisha,
Nao wakachuma.

Wawekezaji yote hawajaweza,
Mashamba kuyalima;
Heri Nafko walivyoyakwatua,
Wanateta wakulima.

Tambua we mwanasiasa,
Unaleta zahama;
Kama kanzu kuichuuza,
Rasilimali mama.

Warudishieni rasilimali wana,
Nao ndama;
Wananchi tuweze kujifugia,
Na kulima.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP