Loading...

Saturday, November 15, 2008

Shambani Hanang Kunani Pale?Namshukuru sana Jalia,
Kurejea Darisalama;
Arusha mpaka Manyara,
Mtafiti sikukwama.

Nimejawa na bashasha,
Mrejesho kuutuma;
Wanazuoni wa Taifa,
Usikilizeni umma.

Ardhi yao Wadatoga,
Iligeuzwa chauma;
Nafko lo ikajitwalia,
Ngano kuilima.

Barbaig do akacharuka,
Kortini akasimama;
Dola ikajitetea kijanja,
Sheria ikazifuma.

Ikaleta Operesheni Sogeza,
Wananchi kuwasukuma;
Vijijini wakaswekwa kisasa,
Wakache kuhamahama.

Ujima uendeshwao kiusasa,
Kikaazimia chama;
Utumike kujenga Tanzania ,
Maendeleo kupima.

Mwalimu akauita Ujamaa,
Tukaukubali pima;
Ukahubiriwa kwa harara,
Tukatazamia mema.

Tukalima kwa ushirika,
Pato kulichuma;
Ranchini tukafuga pia,
Kujipatia nyama.

Hatamu chama kikashika,
Utawala ukauma;
Nacho kikaihodhi Katiba;
Watu kuwazima.

Wafugaji wao wakaswagwa,
Kama wanyama;
Mpaka leo wanatangatanga,
Kutafuta neema.

Uchumi nao ukayumbayumba,
Shilingi ikazama;
Wakalisaliti Azimio Zanzibara,
Likapata kiyama.

Hatimaye Nafko ikafilisiwa,
Ikaupoteza uzima;
Wafugaji ardhiyo wakaililia,
Msafara wakatuma.

Kwao Wakuu wakafikia,
Risala wakaisoma;
Wakasihi ardhi kupewa,
Iwahifadhi daima.

Baadhi yao mashamba,
Wakuu wakasema;
Tutawapa enyi wazawa;
Mgawane mazima.

Ila mengine watayawekeza,
Hao wachuma;
Bila ajizi yakabinafsishwa,
Tena himahima.

Wakayanadi pia matirekta,
Navyo vyuma;
Hata maji wakayabinafsisha,
Nao wakachuma.

Wawekezaji yote hawajaweza,
Mashamba kuyalima;
Heri Nafko walivyoyakwatua,
Wanateta wakulima.

Tambua we mwanasiasa,
Unaleta zahama;
Kama kanzu kuichuuza,
Rasilimali mama.

Warudishieni rasilimali wana,
Nao ndama;
Wananchi tuweze kujifugia,
Na kulima.

2 comments:

Idda November 21, 2008 at 12:52 PM  

Umeonyesha umahiri katika ushairi, na uhodari katika kukusanya taarifa na kufikisha ujumbe stahilivu kwa manufaa ya umma na wenye chungu na nchi yao wanategemewa kuunyakua! Asante sana.

Amina Mcharo December 23, 2008 at 1:33 PM  

Like Chachage like Chambi.
Like father like son.
Safi sana brother...

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP