Loading...

Thursday, November 27, 2008

Yako wapi mapenzi?

Wazuoni nakuja, jamani nisikizani
Mwaweza kutoa hoja, mnitoe matatani
Wasomi mkidhi haja, ya kunitoa gizani
Yako wapi mapenzi?

Nimeenda kwa nyakanga, suluhu sikubaini
Nikapita kwa waganga, nafuu mie sioni
Kwa wanazuoni natinga, muwe langu tumaini
Yako wapi mapenzi?

Mume wangu mi wa kwanza, nilimpenda moyoni
Maisha tuliyaanza, kwa juhudi na imani
Japo shida zilikaza, tuliishi furahani,
Yako wapi mapenzi?

Wakamjia jirani, kumwambia anifuja
Nae akawaamini, uzee hauna tija
Akaniacha njiani, sikupajua kwa kuja
Yako wapi mapenzi?

Nikampata mi wa pili, tukaishi kifahari
Pilau kwa kachumbali, haikuwa na dhohari
Wageni kila mahali, waliuleta ururi
Yako wapi mapenzi?

Utamu wa raha zake, maumivu mwisho wake
Ikatoka hamu yake, kwa mabaya mambo yake
Nikapa sirudi kwake, nae akaenda zake
Yako wapi mapenzi?

Watatu huyu kiboko, japo anao mvuto
Kaniletea vituko, nyumba ikawaka moto
Watoa huko waliko, nyumba kajaza watoto
Yako wapi mapenzi?

Watoto wakawa nduli, mali wanazitafuna,
Kanambia nikubali, nibembeleze vijana
Nami sikuona dili, ndoa ikawa ndoana
Yako wapi mapenzi?

Huyu wanne ninae, nikajua nimepata
Ni mzuri mfanoe, hakuna anaepata
Nilifurahi namie, bingo nimeikamata
Yako wapi mapenzi?

Kumbe ni dalali hali, aso na utu moyoni
Wazee wangu si mali, awatusi hadharani
Wanangu kwake jabali, kulibeba hatamani
Ya wapi mapenzi?

Rafikize makuwadi, iweje na yeye sie
Wafanya ili mradi, ya kwao wayaendele
Hata tupigwe na radi,ngambo ataenda ye
Yako wapi wapenzi?

Talaka hataki nipa, eti anipenda sana
Upenyo tu mkinipa, wima nami namkana
Ila wapi nitapata, wakunipenda kwa sana
Yako wapi mapenzi?

Jamani niambieni, wapi nilipokosea
Au ni ulimbukeni, nambieni nipate jua
Nini sifa yakini, za mume kumtambua?
Yako wapi mapenzi?

© 2008 Mishy Singano

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP