Loading...

Wednesday, December 10, 2008

Huu ndio uhuru kamili?

Picha za kumbukumbu ya uhuru huleta aina fulani ya msisimko wa kizalendo. Msisimko huo, kama zilivyo picha zenyewe, ni kielelezo tu cha jinsi tulivyojisikia tulipopata uhuru.

Hakika picha ya Kapteni Alexendar Nyirenda akisimika Mwenge wa Uhuru kwenye kilele kimojawapo cha Mlima Kilimanjaro ina mguso wa aina yake. Lakini, je, inaweza kuelezea hisia za watoto fulani waliojikusanya katika kilele fulani cha milima ya Upare kushuhudia tukio hilo? Je, inaweza kunasa hisia za mtoto mmojawapo aliyeamua kujiaminisha kuwa aliuona ukiwaka?

Msisimko ni hisia muhimu kwa mwanadamu. Lakini una ubaya na uzuri wake. Uzuri wake ni kwamba unaweza kuleta ari na nguvu mpya. Na ubaya wake ni kwamba unaweza kuleta matumaini hewa au kiini macho.

Kwa upande mmoja, watu wanaweza kusisimuliwa na tukio fulani la kisiasa au kihistoria na kudiriki kusema “ndio, twaweza” na kweli wakaweza kuleta mabadiliko. Lakini kwa upande mwingine, msisimko huo unaweza kufifia na watu wakakata tamaa kuwa kweli “inawezekana.”

Kuna picha ya kumbukizi ya uhuru ambayo inaonesha pande hizi mbili za msisimko. Picha hii inamuonesha Mwalimu Julius Nyerere akiwa amebebwa na wananchi. Uso wake umejaa tabasamu. Shingo yake imepambwa na mashada. Mikono yake imenyanyua juu bango zuri jeupe.

Bango hilo limenakshiwa na maneno fulani. Hatuna budi kusema ni maneno fulani kwa sababu kama mtu huijui lugha ya Malkia, yaani Kiingereza, huwezi kuyaelewa kwa undani. Utahitaji mtafsiri tu maana yanasema hivi: “COMPLETE INDEPENDENCE 1961.”

Shamrashamra za uhuru zilitusisimua sana mpaka tukanyanyua mabango hayo meupe yenye maandishi meusi yanayodai tumepata uhuru kamili. Tulifanya hivyo japo Malkia wa Uingereza aliendelea kuwa mtawala wa nchi yetu huku Mwalimu Nyerere akiwa chini yake kama Waziri Mkuu aliyechukua nafasi ya Gavana aliyekuwa akimwakilisha Malkia. Bado hatukuwa na Rais.

Nderemo, hoihoi na vifijo vya uhuru vilitugusa sana mpaka tukaendelea kuitukuza injili ya “tafuteni kwanza ufalme wa kisiasa na mengine yote mtaongezewa.” Tulifanya hivyo japo mhubiri wa injili hiyo, Osagefyo Kwame Nkrumah, alishaikana baada ya kuona athari za uhuru wa bendera na ukoloni mamboleo. Alishaanza kutuhubiri tuutafute kwanza ufalme wa kiuchumi.

Ni kweli kabisa msisimko huo wa uhuru ulileta mwamko mpya. Ni jambo lisilopingika kuwa kaulimbiu ya Mwalimu Nyerere ya “inawezekana wajibika kwa nafasi yako” ilitufanya tuwe na moyo wa kujenga taifa letu. Hakika kaulimbiu za “Uhuru na Umoja”, “Uhuru na Maendeleo”, “Uhuru na Ujamaa” na “Uhuru na Kazi” zilichochea nia ya kuleta mabadiliko chanya ya kijamii.

Lakini mfumo haubadilishwi na hisia au msisimko tu. Ndio maana mara baada ya huo uhuru ambao tulidhani ni uhuru kamili wananchi wengi tulianza kuyalilia matunda ya uhuru. Tulijiuliza kwa nini wakulima wanalima sana lakini bado nchi haina chakula cha kutosha. Tulishangaa kwa nini wafanyakazi wanafanya kazi sana lakini bado nchi haina tija ya kutosha.

Ilipofika mwaka 1967 hatimaye tukauona mwanga wa ile injili ya “tafuteni kwanza ufalme wa kiuchumi”. Tukalitangaza Azimio la Arusha. Tukatembea kutoka kila pembe ya nchi kuliunga mkono. Tukatoa Mwongozo wa kuziba mianya ya ubadhirifu. Serikali ikataifisha na kushika njia kuu za uchumi. Mafisadi wakaghafilika. Mabepari wakatahayari. Mabeberu wakataharuki.

Cherekochereko hizi za Azimio zilitusisimua sana mpaka tukatunga mashairi, majigambo na ngonjera za kudai kuwa tunatimua makupe na mabwanyenye wote na kukata mirija yote ya unyonyaji na ukandamizaji. Tulifanya hivyo japo tuliendelea kuwaachia waliokuwa makaburu wa kampuni ya Debeers waendelee kuchimba na kufaidika na madini yetu ya almasi za Mwadui.

Sherehe hizi za Azimio zilitugusa sana mpaka tukaendelea kuienzi miradi na misaada yenye masharti tuliyojiaminisha kuwa ni nafuu kutoka katika mashirika makubwa ya nchi za kibeberu. Tulifanya hivyo japo baadhi ya miradi hii ilisababisha tutumie nguvu za dola kuwanyang’anya wafugaji wetu ardhi yao ya malisho na hata kuwafanya wawe wakimbizi ndani ya nchi yao.

Haukupita muda mrefu tukaanza kuyalilia matunda ya Azimio. Tukawa na mijadala mikali kuhusu mafanikio na madhara yake. Mijadala hii ilimfanya Mwalimu Nyerere atuandikie kitabu cha ‘Azimio la Arusha Baada ya Miaka Kumi’ mnamo mwaka 1977. Muasisi wa Azimio akakiri kuwa ngoma ni nzito. Mafisadi wakapumua. Mabepari wakachekelea. Mabeberu wakashangilia.

Tukaupoteza ufalme wa uchumi kabla hata hatujautafuta. Eti ‘Muongo Uliopotea Afrika’ ukaanza 1980. Uchumi ukaporomoka. Uhujumu uchumi ukafanywa ajira. Uchumi bubu ukawa mfumo wa maisha. Benki ya Dunia na Fuko la Fedha la Kimataifa likatubana. Ule wimbo wetu wa “kama unataka mali utaipata shambani” ukageuka kuwa ‘kama unataka mali utaipata fukoni’.

Ila njia pekee ya kuingia huko fukoni ikawa ni kuzipa hizo taasisi beberu uhuru wa kutuamulia sera na mipango ya kitaifa. Zikatuletea ‘Programu ya Mageuzi ya Kimfumo’. Tukabadili mfumo wa Serikali kutoa huduma ya elimu na afya kwa umma bure. Tukakubali kila mtu aubebe mzigo wake mwenyewe. Walalaheri wakaweza. Walalahai wakajitutumia. Walalahoi wakazidiwa.

Watalaam kutoka nje wakaja na ‘TX’ kutufundisha namna ya kuwa na miradi bila kuitegemea Serikali. Ila miradi mingi ikafa. Muongo uliopotezwa ulipoisha hao wakaenda zao. Baada ya muda wakarudi na ‘DFP’ huku wakiwa na injili mpya isemayo kuwa ili mradi usife lazima uwe endelevu, yaani, ili mradi usife lazima uishi. Na ili uwe endelevu shurti tuwezeshwe kuumiliki.

Leo ni miaka 47 toka tupate uhuru baada ya kudai tunaweza kujitawala na kujiendeleza. Lakini bado tunawezeshwa kufanya hivyo. Eti tunawezeshwa kwa kuwa tunadai hatujiwezi. Na hata tunapodai twaweza tunasema hivyo ili tupate ufadhili wa kutujengea uwezo wa kuwezeshana.

Je, huu ndio uhuru kamili tulioubebea bango tarehe 9 Disemba 1961?

© Chambi Chachage - Mwananchi 10/12/2008

1 comments:

Mzee wa Changamoto December 23, 2008 at 5:14 PM  

Asante saaana Mkuu. Ni blog safi sana yenye uchambuzi wa kina. Nimesoma hapa na ninaloweza sema ni kuwa kuna maswali mengi yanayohitaji kujibiwa juu ya hisia na uhuru halisi. Nami nilijaribu kudadisi yale ambayo ningependa yawekwe bayana kwa kujibiwa na viongozi (bofya http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/11/kuelekea-miaka-3-ya-awamu-ya-4.html) ama pia kuangali ahali halisi ya maisha yetu tuelekeapo nusu karne kwa maisha ya mtu wa kijijini (bofya http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/12/them-i-them.html) na pia ulazima wa maadhimisho ya UHURU kwa namna yaadhimishwavyo (http://changamotoyetu.blogspot.com/2008/12/sherehe-za-miaka-47-ya-uhuru-wetu.html). Nimefurahi kuijua blog hii na nitaiweka kwenye BLOG SCROLL na kuitangaza kwa wadau wapate uelimishaji zaidi.
Blessings

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP