Loading...

Tuesday, December 23, 2008

Mwaka unaishia tumejifunza ujasiri au ubwege?

Mwaka 2008 ndio huo unazidi kututupa mkono. Maandalizi ya kuuaga mwaka yameshaanza kwa kishindo. Pilikapilika za kufunga haraka mahesabu ya mwaka nazo zinaendelea kwa kasi mpya.

Kabla shamrashamra za kuukaribisha mwaka 2009 hazijaanza ni vyema tukajikumbusha yale yaliyojiri mwaka huu. Na si kujikumbusha tu bali pia kutathmini ni nini hasa tumejifunza katika kipindi hiki. Katika kufanya hivyo tuzingatie kuwa maarifa ni yale mafunzo tunayoyakumbuka.

Tuanzie Bungeni. Pengine funzo kubwa kuliko yote tulilolipata ni kuwa sisi Watanzania sio mabwege tena. Funzo hili linatokana na kauli ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge ya Kuchunguza Sakata la Richmond, Mheshimiwa Dakta Harrison Mwakyembe (MB).

Kwa mbwembwe nyingi, Mbunge huyo wa Kyela aliisoma ripoti hiyo mbele ya halaiki iliyojumuisha wabunge na wananchi tuliokuwa tukimsikiliza kupitia runinga na redio. Siku hiyo vilabu vya pombe viligeuka kumbi za kusikiliza Bunge. Inasemekana hata kipindi maarufu cha Ze Komedi kilishuka chati kwa jinsi Watanzania tulivyopania kujua sababu hasa ya kuwa gizani.

Hakika ripoti hiyo ilitutoa matongotongo. Kwa mara ya kwanza tulijiona sote tuko nyuma ya mapazia tukishuhudia tulivyoingizwa mjini. Tukaambiwa huo tuliousikia ndio ujasiri wa kifisadi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu akalazimika kujiuzulu. Nchi ikatikisika. Rais wetu akalazimika kulivunja baraza lake la mawaziri kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu. Kimya kikakataa kutanda.

Mjadala mkali ukazuka kuhusu kilichojiri. Wapo waliosema kuwa wizi wa Richmond ulikuwa ni wa kitoto. Alaa kumbe kuna wizi wa kikubwa! Wapo pia waliosema kuwa huo wizi ni wa Kidato cha Nne. Lo kumbe wizi wa mitihani ndio kiwango cha chini kabisa cha utaalamu wa kifisadi!

Tukajadili hadi tukagundua kuwa tulijiachia sana mpaka mafisadi wakawa na ujasiri wa kufanya wizi ambao haujaenda shule. Kwa kuwa hakukuwa na wa kumfunga paka kengele basi mafisadi waliweza kuingia mpaka jikoni na kufanya wanachotaka bila kizuizi chochote. Kumbe upole na ubwege ulitukolea wee mpaka mafisadi wakawa hawaogopi kuvunja sheria zetu kirahisirahisi tu.

Kwa ujasiri wa kizalendo, tukaungana na wanakamati wateule kuapa kuwa hakutatokea tena skendo ya kifisadi kama ya Richmond. Tukasubiria kwa hamu sana utekelezaji wa mapendekezo ya kamati. Kwa utulivu,Waziri Mkuu mpya akatuelezea Bungeni kuhusu utekelezaji ulipofikia.

Wapo walioridhika na jinsi ripoti yake ilivyoonesha jinsi utekelezaji unavyokwenda hatua kwa hatua. Lakini wapo walioiona kuwa ni kiinimacho tu cha kuvuta muda. Pia wapo walioona kuwa utekelezaji huo ni sehemu tu ya utamaduni wa kulindana, kutowajibika na kutupiana majukumu.
Pamoja na kuwa na maoni tofauti, kwa ujumla tunaendelea kusubiri mpaka tuone hatma ya utekelezaji wa mapendekezo ya kamati hiyo ya aina yake. Tumejiaminisha kuwa sisi Watanzania sio mabwege tena japo bado tu wavumilivu. Ndio maana safari hii tumeshtukia mapema dili la kutaka kununua mitambo ya umeme ya yule aliyekuwa mrithi wa Richmond, yaani, Dowans.

Naam tunajiaminisha kuwa sisi Watanzania sio mabwege tena ndio maana tumezuia dili la kutorosha mitambo ya umeme ya Aggreko ambayo inasemekana haijatulipa kodi ya shilingi bilioni 10. Hakika tunaamini tumeupa talaka uvumilivu wa kibwege ndio maana tunahoji huyu Kagoda huyu hivi ni mnyama gani na sasa tunaanza kupata majibu kutoka hapa, pale na kule.

Lakini mazoea hujenga tabia. Na tabia za muda mrefu hazifi kirahisi. Hivyo, bado chembechembe za woga wa kibwege bado zinatusongasonga Watanzania. Bado tuna uwili wa popo. Tuna ujasiri wa kuhoji kilichofanyika ila bado tuna ubwege wa kutohoji kinachofanyika.

Tuna ujasiri wa kuhoji kwa nini imechukua miaka mingi kuchunguza matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu ili kufungua mashtaka fulani. Lakini tuna ubwege wa kutohakikisha kuwa taarifa za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusiana na udhibiti wa matumizi hayahaya mabaya ya madaraka na ubadhirifu zinafanyiwa kazi vilivyo leo, kesho na keshokutwa.

Ndio, tuna ujasiri wa kuhoji kama fedha ilizochota Kagoda kwenye EPA pale BOT kweli zilitumiwa na chama fulani cha kisiasa. Lakini tuna ubwege wa kutohakikisha kuwa maagizo ya taarifa za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu Msajili wa Vyama vya Siasa inayojumuisha rekodi za vyama hivyo yanatekelezwa mwaka huu, mwaka kesho na mwaka keshokutwa.

Undumilakuwili huu wa kuchanganya ujasiri na ubwege ndio unatufanya tusite kufanya mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa na sheria zinazohusu uhuru wa habari. Uwili huo popo ndio unatufanya tusuesue kuleta mabadiliko ya kikatiba. Tunaogopa sana. Hatuogopi kidogo.

Kwaheri mwaka 2008. Asante kwa kutufundisha a be che de za ujasiri wa kibwege. Karibu mwaka 2009. Njoo utufunde a b c za ubwege wa kijasiri.

Mwandishi: Chambi Chachage
Chanzo: Mwananchi 23/12/08

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP