Loading...

Friday, January 30, 2009

Kuinuka na Kuanguka kwa UDSM!

Kwa aliyewahi kusoma, kukipenda, kufundisha na kufanya kazi maeneo ya chuo, na yote kabisa Mtanzania mzalendo!

Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, palikuwa mahala pa cheche ya fikra na mbubujiko wa mijadala makini na ya huru kwa maslahi ya Taifa na Afrika kwa ujumla.

Palikuwa mahala pa ndoto ya kila kijana kuweza kufika na kupata fursa ya kusoma hapo. Ilikuwa ndoto na fahari ya kila mzazi kuweza kumfikisha mtoto wake hadi ngazi hiyo. Ilikuwa ndoto kwa wanataaluma (wa ndani na nje ya Tanzania) kupata fursa kufundisha katika chuo hicho. Mlimani palikuwa kizio cha kupima taaluma ya juu nchini!

Hakika waswahili walisema “hakuna marefu yasiyo na ncha”! na kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho! Kama kilivyoanza kwa juhudi za dhati ndivyo kinavyomalizwa kwa juhudi za dhati na kundi la watu wachache wasiotaka kusikia la mwazini wala mnadi swala wakiwa na kiburi cha nguvu ya vyombo vya dola na ushosti wa wakuu wa nchi.

Kwa sasa ni chuo ambacho kinasifika kwa kuongozana kwa migogoro na hata migomo na kusimamishwa mara kwa mara kwa wanafunzi wake! Hii ni historia nyingine inajengwa katika chuo hiki makini.

Historia inayojengwa sasa ya kukithiri kwa migogoro na kusimamishwa kwa wanafunzi inapelekea kwa watu makini kuhoji uwezekano wa kufinywa mianya ya majadiliano na uibukaji mpya wa fikra hasa kama hazifurahishi tabaka tawala.

Hii ni ishara ya mlipuko! Mlipuko unaotokana na kukandamizwa kwa muda mrefu sana kwa fikra pevu za wanazuoni(hususan chipukizi), bongo huru, na hamasa ya mabadiliko. Hali hii inakuwa ishara mpya ya machweo ya chuo hiki adhimu, chuo hiki kilichojengwa kwa nguvu za Hayati Mwl. Nyerere kuelekea anguko ambalo haliwezi zuilika mpaka sasa kutokana na ukosefu wa utashi wa kulizuia anguko hilo.

Kukithiri kwa matumizi ya nguvu na ubabe zaidi ya busara na umakini wa kisomi na kustaarabika, kukithiri kwa uongozwaji wa kisiasa zaidi ya kiweledi “professionalism”, kukithiri kwa umimi na kiburi cha kutosikiliza wanaokuzunguka wala wananchi dhidi ya kuwa mtumishi na msikivu na kutenda kwa maslahi ya umma!!

Hii inadhihirishwa na ufinyu wa miundo mbinu kama vyumba vya mihadhara dhidi ya wanafunzi, kuchakaa kwa vyumba vya mihadhara hivyo na haswa makazi ya wanafunzi, ukosefu wa vitabu na vifaa vingine muhimu kwa kitaaluma, kutokwenda na mabadiliko mathalani ukosefu wa vitabu vipya vinavyozinduliwa kila pembe duniani ama matumizi ya TEKNOHAMA, ufinyu wa wahadhiri na walimu kwa ujumla ambao unachochewa sana na urasimu! Kukithiri kwa roho za kiroho na kifisadi zinazopelekea kurudisha nyuma utendaji hususan ufundishwaji na kujikita katika kusaka “madili na fedha”. Ni baadhi tu ya ishara za dhati kuelekea anguko la chuo hiki isipochukuliwa juhudi za dhati.

Hapo nimeamua kutoyajadili shutuma za kukithiri kwa rushwa haswa ya mapenzi, uvunjwaji wa mitihani, kukithiri kwa kufeli kwa wanafunzi, mrundikano katika vyumba vya kulala na hadi katika madarasa, kutokuwepo tena kwa wakaguzi kipindi cha mafunzo ya vitendo “practical training-PT” (ati sababu hakuna fedha)!!

Ufinyu wa wahadhiri wa ngazi zote, na kukimbiwa na wahadhiri wa chache waliopo kwenda katika vyuo hivi vinavyoanzishwa nchini na nje ya nchi ni ishara hasi kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.

Kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa shahada ya pili “uzamili” na ya “uzamifu” katika chuo cha Dar-es-Salaam mwaka hadi mwaka inatoa ishara mbaya sana kwa chuo cha Mlimani. Kasi kubwa ya vijana wabichi wahadhiri kujiunga na taasisi za vyuo vya juu nchini tofauti za Chuo Kikuu Mlimani (ambacho bado kinalia ukosefu wa wahadhiri) kinaimarisha kifo cha Chuo hiki nchini.

Kuibuka kwa vyuo vingi mbadala nchini vya umma na binafsi inakuwa ahueni kwa wazazi ambao hawana uwezo wa kuwakimbiza watoto wao ng’ambo. Vyuo hivi ambavyo vilipoanza vimekuwa vikidharauliwa na kupata kebehi sasa vimeanza kuimarika siku hata siku na kuwa “jiwe kuu la pembeni baada ya kukataliwa na “mwashi”(Mlimani)”!!

Kufutika fikra na mtazamo wa wazazi na wanafunzi kuwa chuo kikuu bora ni “Mlimani” pekee nayo ni fursa mpya ya mapinduzi katika sekta ya elimu ya juu nchini. Ingawa kwa upande wa Chuo cha Dar-es-Salaam kuongeza msumari katika jeneza la kuelekea kaburini kwa chuo hicho nchini.

Hiki ndicho Chuo cha Dar-es-Salaam, chuo ambacho kilishasimama na kuimarika si tu nchini katika taaluma ya elimu ya juu bali hata Afrika. Licha ya takwimu za kuporomoka toka nafasi ya 13 Afrika iliyowahi kufikiwa!

Inasikitisha sana, lakini ni kutokana na kuchanganya “urafiki” wa kinafiki, ukabila, siasa mahala penye kuhitaji ufanisi na utaalamu. Hakika anguko la chuo hiki ni anguko kubwa sana nchini, na sikitiko kwa kila ambaye amepitia katika chuo hiki.

Wenu,

Asha Miguubaja.

1 comments:

Idda Hadjivayanis Paul February 3, 2009 at 4:04 PM  

Nimeguswa sana na kipande hiki cha habari, mimi kama mdau wa chuo kikuu mlimani ambaye nilisoma hapo miaka 11 iliyopita nasikitika sana kushuhudia kinavyoanguka kama mtoto anayejifunza kutembea.Hata ndoto za mwanangu kutamani amalize elimu yake ya chini na kuendelea mpaka mlimani kupata elimu yake ya juu imeanza kuvunjika pia.Kwa kweli kunahitajika juhudi za pamoja za ziada na kiada kukirudisha mahali pake; la sivyo tutabakiza kuwa eneo la kihistoria tu.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP