Loading...

Tuesday, January 27, 2009

Vigogo ‘Wajinyonge’ ili 'Wasaidie' Wakulima

Katika Gazeti la HabariLeo la tarehe 15 January 2009, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, amekaririwa akisema kuwa “ninaposema kujinyonga nina maana tubadilike, tuache maneno na tudhamirie yale tunayosema, la sivyo kilimo hakitaweza kuwa uti wa mgongo wa Taifa hili.”

Haya maneno ya ‘Mtoto wa Mkulima’ sio mara ya kwanza nikimsikia akiyasema. Lakini najiuliza: Je, hao ‘vigogo’(maana siku hizi sio watumishi tena) wanaposikia haya maneno wanaukubali ujumbe huo?

Kwa kweli suala la kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida (Recurrent Expenditure) za wizara, tawala za mikoa, serikali za mitaa na mawakala wa serikali ni kubwa mno na zinatumiwa vibaya. Kwa sehemu kubwa ukilinganisha na bajeti za maendeleo (Development Expenditure) na utakuta uwiano ni mbaya.

Mtoto wa Mkulima anatoa mfano wa ununuzi wa magari ya kifahari, ‘mashangingi’, na gharama za semina. Nami naamini pia kuwa kuna matumizi ya kila siku yasiyo ya lazima.

Akiendelea kufafanua, Mwana wa Mkulima, anasema “kwangu mimi kilimo cha jembe la mkono ni tatizo na bila kulibadili hatutaweza kusonga mbele.” Hata mimi ninakubaliana naye, ila kauli hizi ni za miaka nenda rudi ila hakuna lolote linalofanyika kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kuliacha jembe la mkono na kwenda katika kilimo cha mashine.

Lakini tatizo la kilimo Tanzania, na bara zima la Afrika, ni suala la kutotumia trekta tu? Kuna haja ya matatizo mengine pia kuangaliwa kwa upana na urefu wake. Mfano masuala ya elimu ya kilimo, upatikanaji na matumizi ya mbolea, wataalamu wa kilimo vijijini, miundombinu, bei ya mazao(hasa ni kiasi gani mkulima anachopata katika bei ya mwisho ya mazao hayo).

Wakati Mtoto wa Mkulima akipiga panda kwamba Serikali iache, kama sio kupunguza, kununua magari ya kifahari, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete anasema “sasa hivi ukisema siasa ya Ujamaa na Kujitegemea unaonekana ni mwendawazimu.” Sijui ukisema hili la Trekta badala ya Shangingi unaonekana ni nani?

© Adam Jackson 2009

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP