Loading...

Wednesday, March 4, 2009

Kwa kuwa tumeamua kufa na wawekezaji

Mwaka jana kipindi hiki nchi ilitikisika. Kamati teule ya Bunge ya kuchunguza utoaji wa zabuni ya kuzalisha umeme kwa kampuni ya Richmond ilitikisa wenyenchi. Ripoti yake ikatufanya wananchi tutikise vichwa.

Kwa mbwembwe nyingi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dakta Harrison Mwakyembe (MB), aliisoma ripoti hiyo mbele ya wawakilishi wa wananchi. Miongoni mwa sentensi alizotumia kwa umahiri kuelezea kwa nini tuliingia kwenye mkataba huo tete ni ile ya “kwa kuwa Watanzania tulishaamua kufa na Richmond, tukasonga mbele!”

Naam, ni kweli kabisa tuliamua kufa na Richmond kama ambavyo tuliamua, tumeamua na –
Mungu apishilie mbali – tutaamua kufa na mambo mengi tu. Moja ya masuala ambayo tuliamua na pengine bado tumeamua kufa nayo ni suala la uwekezaji. Kwa hilo tumeamua kusonga mbele.

Wataalamu wetu hutuambia bila kutafiti huna haki ya kunena. Hivyo, hatuna budi kunukuu takwimu zao. Ni dhahiri kuwa kiwango cha uwekezaji kimeongezeka sana toka tulipofungua milango na madirisha ya sera na sheria zetu. Taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinathibitisha hilo – mwaka 2008 kiwango hiki kilikua kwa karibia asilimia 25 zaidi ya cha 2007.

Hakika kazi ya kubinafsisha mashirika na mali za umma kwa wawekezaji inafanyika. Kazi hii ni nzito sana ndio maana iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) iliomba iongezewe muda mwishoni mwa mwaka 2007 ili imalizie kazi hiyo. Ila haikuongezewa.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, hadi kufikia 30 Juni 2007 ilikuwa imeshamaliza shughuli 1,002 za kubinafsisha au kuhamisha umiliki – ama kwa uuzaji, ubia, ugawaji, ukodishaji au ufilisi – wa mashirika 336 kati ya 361 yaliyoorodheshwa, na mali 666. Kazi yote hiyo iliifanya toka mwaka 1993. Hiyo ilikuwa ni mara tu baada ya kutungwa kwa sera ya uwekezaji mnamo mwaka 1992.

Haya yote yalianza kufanyika licha ya muasisi mkuu wa mashirika hayo ya umma, Mwalimu Julius Nyerere, kulaani ubinafsishaji wa kila kitu. Mwalimu alisisitiza kuwa tunachohangaika kukibinafsha ni kitu, ni kitu fulani tulichokijenga. Na akatukumbusha kuwa tunaota tunapodhani kuwa tukibinafsisha kila kitu, mpaka jela zetu, basi wawekezaji wa nje watatukimbilia kwa kasi.

Kwa uchungu Mwalimu akatusihi kuwa “sasa tusikubali tusikubali tuwacheke wajinga wale nani anataka anataka mashirika yetu yafe ndiyo kataeni kabisa kabisa ndiyo ya kwao hayafi mbona hala kuja kuua mashirika yetu bwana?” Lakini wapi tukakubali. Tukaamua kufa na wawekezaji.

Hivyo basi, tukajikuta kwa nguvu nyingi tunatumia zaidi ya miaka 17 kutafuta wawekezaji huko, pale na kule. Tukawa kama wavu wa kutega panya. Lo, tukavua waliomo na wasiokuwemo.

Kwa mfano, ilituchukua miaka 12 kutafuta na kupata mwekezaji wa kilichokuwa Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo (SPM). Na hata baada ya kumpata tukajikuta tuna mjadala mkali Bungeni kuhusu kama huyo mwekezaji ndiye mwekezaji halisi au anatumiwa tu. Hilo tukaliundia kamati.

Hizi juhudi zetu za kufa na wawekezaji zikamfanya Waziri anayehusika na Viwanda kujitutumua Bungeni kueleza kuwa huyo mwekezaji baada ya kununua SPM ndio akampata mwenzake wa kufufua naye kiwanda. Akadai hivyo ndivyo zile hisa 100 alizokuwa nazo mwekezaji akapewa huyo mwenza. Akasisitiza kuwa hili ni suala la kawaida katika biashara na BRELA ina taarifa.

Kuhusu wasifu wa huyo mwenza, Waziri akasema “na bahati nzuri tumehangaika kueleweshana, tumepiga simu Registrar of Companies, British Virgin Island na kuongea na Afisa anayeitwa Benedin Smith na kupata taarifa zifuatazo…wanayo kwenye rekodi zao kampuni inayoitwa Angel Hurst Industries Limited, yenye namba za usajili 395195, taarifa anazotoa ni jina na namba za usajili tu, ukitaka anything more ni lazima ufanye official search na kulipa dola 25. Kwa hiyo, tumejitahidi na katika kupata ukweli tutafanya wote, ukweli wa Watanzania wote.”

Hapo ndipo wadadisi wa mambo wanapojiuliza: Inakuwaje mali iwe yetu wenyewe na bado tupate shida hivyo kupata taarifa za tunaowabinafsishia mali yetu? Au ndio mambo ya mteja ni mfalme? Kama mteja kweli ni mfalme ina maana muuzaji ni mtumwa?

Katika ziara yake katika mashamba yaliyobinafsishwa kwa wawekezaji huko Hanang, Rais naye akaombwa na waanchi awarudishie mashamba hayo. Kilichowafanya watoe ombi hilo ni uhaba wa ardhi ya kulima na kuchunga na ukweli kuwa wawekezaji hawawezi kulima ardhi yote.

Hata hivyo, Rais akanukuliwa na HabariLeo (17/09/2008) akiwajibu: “Hilo la mashamba mimi siwezi kuwapatia, yale ni mashamba ya watu siwezi kuwagawia ninyi…Hayo mashamba ni sisi wenyewe tumeshindwa kuyaendesha, tumeamua kuwapatia wawekezaji ambao wameanza kuyafufua polepole, tutakachofanya sisi serikali ni kuwataka waongeze kasi ili na nyinyi muweze kupata ajira…Pale hakukuwa na meneja ambaye ni Mzungu au Mhindi. Ni sisi wenyewe Waswahili ndio ambao tumeyaua…Acheni maneno maneno, tusiwe mafundi wa kusema mameneja tulikuwa sisi wenyewe, miluzi mingi humpoteza mbwa…”

Hii ndio halisi. Tafiti na tathmini mbalimbali za taasisi za Serikali na zisizo za Serikali zinaonesha kuna wawekezaji ambao uwezo wao wa kulima ardhi ya umma waliyobinafsishiwa ni mdogo. Wengine wanadiriki hata kukodisha vipande vya mashamba husika kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi na ambao wanaililia Serikali iwagawie mashamba hayo wayalime ili tule.

Kwa nini tunawakumbatia wawekezaji uchwara? Je, ni kwa sababu tumeamua kufa na wawekezaji au kuna sababu zingine zilizojificha? Nini kinatufanya tuukate mkono unaotulisha?

Hivi ni takwimu gani zinaonesha kuwa wanaolilisha taifa hili ni wawekezaji waliowekeza katika kilimo? Ni lini tutaachana na biashara ya kuzalisha njaa kwa kutowapa wakulima wanaotulisha kipaumbele? Au tunasubiri wawekezaji wageuze mashamba yetu yote yawe ya mibono kaburi?

Mwandishi: Chambi Chachage

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP