Loading...

Wednesday, May 6, 2009

Kiswanglishi kiwe Lugha Rasmi ya Taifa

Sikuplani kuandika makala hii wiki hii. Sikupanga kufanya hivyo hasa ukizingatia kuwa juma hili kuna ishu nyingi zinazochukua taimu yetu sana. Suala la mafisadi papa ni mojawapo ya hayo masuala yanayochukua muda wetu mwingi.

Nilichenji, yaani nilibadili, mawazo yangu baada kusikiliza kipindi cha Redio Wani. Katika programu hiyo watalaamu walikuwa wakidibeti, yaani wakijadiliana, kuhusu matumizi ya lugha ya kufundishia. Hoja iliyonitachi, yaani iliyonigusa, sana ni ile inayosema kuwa matumizi ya lugha ya Inglishi, yaani Kiingereza, kufundishia yanasababisha wanafunzi wengi wasipate elimu.

Hakika ni jambo lisilopingika kuwa maticha, yaani walimu, wengi hawajui kufundisha kwa lugha hii kwa namna inayowafanya madenti, yaani wanafunzi, waelewe wanachofundishwa. Risechi, yaani tafiti, nyingi zimefanywa na watafiti wa ndani na nje ya nchi yetu kuonesha kuwa kutumia lugha isiyoeleweka vizuri kufundishia kunasababisha wanafunzi wasielewe vizuri somo.

Lakini pamoja na ukweli huo bado tunang’ang’ania kutumia Kiingereza kufundishia kuanzia Skuli, yaani Shule, za Sekondari hadi kwenye Vyuo Vikuu. Wengine tumeamua kabisa kuwa na shule za msingi zinazotumia Kiingereza kufundishia. Eti hatutaki watoto wetu wakose chansi, yaani fursa, ya kujua lugha ya globalaizisheni, yaani utandawazi, kana kwamba lugha yetu ya Kiswahili yenye maneno lukuki ya Kiarabu, Kiingereza na Kireno nayo sio lugha ya utandawazi!

Ni kweli kabisa kuwa sisi na watoto wetu tunapaswa kuijua lugha ya Kiingereza. Lakini njia ya kujifunza Kiingereza kizuri cha kuongea na kuandika sio kwa kukitumia kama lugha ya kufundishia katika jamii ambayo haikijui vyema. Ndio maana watoto wetu na hata viongozi wetu wanachanganya sana Kiingereza na Kiswahili wanapozungumza. Sasa hicho ni Kiingereza gani?

Wapo wanaokiita Kiswanglishi. Lakini, je, ni Kiswanglishi kweli? Hapana! Hicho ni Kiswahili kinachobadilika ghafla katikati ya sentensi au mazungumzo na kuwa Kiingereza au Kiingereza kinachobadilika ghafla na kuwa Kiswahili. Naam ni ‘Kiswahili English’ au ‘English Kiswahili.’ Wataalamu wa lugha wanauita mtindo huo ‘code switching’ yaani kubadilibadili lugha katikati.

Kiswanglishi nachotaka kiwe lugha ya Taifa ni kipi basi? Ni hicho ambacho kimetumika katika sentensi za mwanzo za makala hii. Hiyo ni lugha ambayo Watanzania wengi, waliopo mijini na vijijini, wanakitumia. Kwa mfano, Bibi yangu amewahi kuniambia “ukifanya hivyo utadedi” akimaanisha ‘ukifanya hivyo utakufa.’ Hicho ndio Kiswanglishi halisi maana ni Kiswahili kilichokopa neno ‘dead’ kutoka kwenye ‘English’ na kulifanya liwe neno ‘dedi’ la Kiswahili.

Mifano ya jinsi tunavyotumia Kiswanglishi cha aina hii katika maandishi na mazungumzo yetu ya kila siku ni mingi. Hii ni baadhi tu: “nakwenda jobu kisha naenda shoping’ tauni”; “najiandaa na pepa kisha naenda kupata menu”; “yule sista/braza atakupa data zote unazohitaji.” Hiki ndicho Kiswanglishi kinachopaswa kuwa lugha ya Taifa maana ndicho Kiswahili chenyewe.

Hakika “Kiswahili sio Kreoli wala Pijini”. Sentensi hii imeganda kichwani kwangu toka Mwalimu wangu wa Kiswahili alipoitamka na kuiandika ubaoni nilipokuwa Sekondari. Kwa ufupi, alikuwa ana maana kuwa pamoja na kwamba Kiswahili kimeazima maneno kutoka lugha nyingine - kama vile Gari na Duka kutoka kwenye Kihindi, Mvinyo na Meza kutoka kwenye Kireno, Malaika na Shetani kutoka kwenye Kiarabu, Skuli na Hela kutoka kwenye Kijerumani - bado ni lugha kamili inayofuata mnyambuliko wake wenyewe wa maneno wa Kibantu.

Hivyo Kiswanglishi cha kweli ni Kiswahili cha Utandawazi - kinachokopa na kukopesha sana maneno. Ni Kiswahili kinachokubali kuchukua ama kukopa maneno mapya ya Kiingereza na kuyafanya yawe ya Kiswahili cha Kibantu na yaweze kutumika katika sentensi ya Kiswahili cha Kibantu. Kwa mfano, Kiingereza kikitumia ‘dead’ kinasema ‘s/he is dead’, ‘s/he will die’ na ‘s/he is dying’ lakini Kiswahili kikilikopa neno hilo kitasema ‘amededi’, ‘atadedi’ na ‘anadedi.’

Kwa kukonkludi, yaani kuhitimisha, napenda kutoa wito kuwa tuidhinishe Kiswanglishi, kama kilivyotafsiriwa katika makala hii, kitumike kama lugha rasmi hasa shuleni na vyuoni. Tukifanya hivyo tutashangaa kuona lugha yetu inakua, elimu yetu inapanuka na jamii yetu inapata maendeleo maana lugha ya mawasiliano ni chachu ya kuongeza ujuzi, maarifa na uelewa mpana.

Naam Kiswahili na kiendelee kutandawaa kwa kasi katika zama hizi za utandawazi kama kilivyotamalaki enzi zile tulipofanya biashara zenye tija na Waaajemi, Waarabu na Wachina bila kutegemea lugha zao. BAKITA na TUKI mpo? Kubalini yaishe: 'Kiswahili = Kiswanglishi'!
-----------------------------------------------------------------------------

Visawe Vipya Virasimishwe

Yuthi Visheni asante kwa kuendeleza dibeti hii. Hiyo hasa ndio misheni ya makala yangu ya wazi, yaani, kuendelea kuchochea mjadala wa kisera ila katika namna ambayo utaliangalia upya - kwa mtazamo wa Kiswanglishi - suala la lugha ya kufundishia ambalo linarudisha sana nyuma maendeleo yetu.

Kwenye Kiswahili kuna maneno yanaitwa 'Visawe'. Katika Kiingereza maneno haya yanaitwa 'Synonyms'. Kwa ufupi, visawe/synonyms ni maneno yenye maana sawa au maana zinazokaribiana sana. Lugha yoyote inayokua haijifungi kuwa na neno moja linalowakilisha kitu fulani. Hivyo unakuta lugha kama Kiingereza ina maneno kama (1) eat (2) consume (3) munch ambayo yote yana maana sawa au zinazokaribiana na yanaweza kutumika kuelezea tukio hilo hilo moja,yaani 'kula'. Kama unatumia Microsoft Word njia rahisi ya kuziona hizi synonyms ni kukliki/kubonyeza kitufe cha kulia cha mausi/mouse yako kwenye neno husika na utaona chaguo la 'synonyms' na ukilibofya hilo utapata hayo maneno mengine yenye maana sawa na hilo neno.

Matumizi haya ya visawe/synonyms utaona yanaonesha kuwa hoja yako hapo chini haikubaliani na hali halisi ya ukuaji wa lugha ya Kiswahili na matumizi yake la kila siku. Kiswahili unachokiongelea hapo chini, ambacho mimi nakiita 'Kiswanglishi' kinachochanganya maneno kukitofautisha na 'Kiswanglish' kinachochanganya lugha, kina visawe vingi tu. Hapa nina 'Kamusi ya Visawe: Swahili Dicitionary of Synonyms' iliyotungwa na Mohamed A. Mohamed & Said A. Mohamed na kuchapishwa hapa Afrika Mashariki na East African Educational Publishers. Kwa mujibu wa Dibaji yake, Kamusi hii ina visawe visivyopungua 71,000. Maneno ya Kiswahili yanayotupa hivi visawe ndio maneno hayo hayo tuliyochukua kwenye lugha za Kiarabu, Kiingereza, Kireno, Kijerumani, Kihindi na kwenye lugha mbalimbali za Kiafrika. Ila kama nilivyosisitiza kwenye makala yangu ya wazi, kwa sasa tunachukua maneno mengi zaidi kutoka kwenye Kiingereza. Hivyo basi, sioni kwa nini tusitumie maneno hayo, yakiwemo ambayo ni visawe kama hivyo ulivyovitaja hapo chini, na kuvirasimisha ili tuvitumie kama sehemu ya lugha yetu ambayo kwa sasa inazidi kuwa Kiswanglishi kuliko ilivyo 'Kiswarabu'.

Nahitimisha hoja yangu kwa kutoa mifano kadhaa ya visawe na tofauti kati ya 'Kiswanglishi = Kiswahili' na 'Kiswanglish = Anglo-Kiswahili':

- Kiswanglish: Nakwenda kula chakula then I'll go to town alafu nitarudi kazini, of course I will see you there (Sentensi hii imechanganya lugha mbili)
- Kiswanglishi: Nakwenda kupata menu kisha nitaenda tauni alafu nitarudi jobu, naam tutaonana hapo (Sentensi hii inanyambulika Kibantu/Kiswahili)
- Visawe vya Kiswarabu: salimu,amkia, amkua sabahi, lahiki (maneno yote haya yana maana sawa na hutumika kwa kubadilishana)
- Visawe vya Kiswanglishi: televisheni, runinga, tivii (maneno yote haya yana maana sawa na huweza kutumika kwa kubadilishana)

-------------------------------------------------------------------------

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP