Loading...

Wednesday, May 20, 2009

Wavumbuzi Wetu Wanapotelea Wapi?

Mtaalamu mmoja wa usomaji alikwenda kutafiti hali ilivyo katika Shule ya Msingi Keko Magurumbasi. Hapo alikuta maktaba nzuri iliyokuwa na vitabu vya Mradi wa Usomaji wa Watoto (CBP). Pia alikuta vitu mbalimbali ambavyo vilikuwa vimetengenezwa na wanafunzi.

Kilichomvutia sana mtafiti huyo ilikuwa ni modeli ya Jiji la Dar-es-Salaam na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Hakika modeli hii haikutofautiana kabisa na zile zinazotengenezwa na wanafunzi wa Chuo cha Ardhi au wa pale Kitivo cha Uhandisi. Lakini aliyeisanifu modeli hiyo hakuwa mwanafunzi au mhadhiri wa Chuo Kikuu. Alikuwa ni mwanafunzi wa Darasa la Saba!

Akiwa amejawa na hamasa, mtafiti huyo alimuuliza mwalimu aliyekuwa anasimamia maktaba hiyo kuhusu huyu mwanafunzi aliyekuwa na kipaji cha kusanifu majengo. ‘Ahh mazingira ya uswahilini hapa Keko sio mazuri kwa elimu’, mwalimu alisema kwa unyonge. ‘Sasa itakuwaje mwanafunzi huyu asipofaulu mtihani wa Darasa la Saba?’ aliuliza mtafiti kwa wasiwasi.

Jibu alilolitoa mwalimu linatoa mwanga kuhusu kile kinachowasibu wavumbuzi wengi hapa nchini. ‘Mhh ataishia kuwa sign writer mitaani’, alisema mwalimu kwa sauti ya kukata na kukatisha tamaa. Alisema hivyo baada ya kusisitiza kuwa wazazi wa eneo hilo lenye uhalifu sana aidha hawana uwezo wa kusomesha watoto wao sekondari au hawajali tu umuhimu wa elimu.

Sijui mwanafunzi huyo alifanikiwa kupata elimu ya sekondari. Wala sijui kama alifanikiwa kujiunga na elimu ya juu. Na kama hakujiunga na vyuo vikuu sijui kama alipata fursa ya kupata mafunzo ya ufundi kwenye vyuo vyetu vya ufundi stadi. Ninachojua ni kuwa katika mitaa ya jiji la Dar-es-Salaam kuna vijana wengi tu wenye vipaji kama hivyo na ambao hawana ajira rasmi.

Vijana hao huuza michoro yao ya usanifu majengo kwa staili ya kimachinga. Wengine naambiwa ni wahitimu wa vyuo vikuu. Lakini inawezekana kabisa kuwa wengine hawakubahatika kuyaona madarasa yanayotoa elimu ya juu. Kila ninapowaona vijana hawa huwa namkumbuka sana yule mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Msingi Keko Magurumbasi.

Huwa najiuliza kama naye ni miongoni mwa vijana hawa wanaouza michoro yao ya usanifu mitaani bila kuwa na soko la uhakika. Napowaona ‘sign writers’, yaani wasanii wanaochora alama na michoro mbalimbali, huwa najiuliza kama ule unabii hasi wa mwalimu ulitimia na kama ulitimia ni kwa kiasi gani kazi hii inamsaidia kutopoteza kipaji chake cha usanifu majengo.


Juma hili maswali haya yamezidi kunitatiza baada ya nusu mwaka kupita bila mhitimu wa shahada ya ‘honors’ ya sayansi ya biolojia ya kimolekyuli na teknolojia ya biolojia (‘molecular biology and biotechnology’) kupata ajira. Waajiri kadhaa wanamjibu kuwa teknolojia yetu iko chini sana hivyo hawana kazi anayoweza kuifanya au hakuna vifaa vya kutosha katika maabara.

Kilichonitatiza zaidi ni kile nilichokigundua baaada ya kumshauri aende Chuo Kikuu basi kusomea shahada ya juu ili akafundishe mpaka hapo kutakapokuwa na nafasi ya kutumia elimu yake kwenye mashirika ya utafiti wa tiba za kibiolojia. Niligundua hata shahada yao ya pili ni marudio tu ya yale aliyoyasoma na tena haigusii kwa kina masuala ya bioteknolojia. Kwa nini?

Lo nikajikuta nakubali kuwa ni kweli kuna wataalamu wetu ambao wanalazimika kutukimbia kwa kuwa hatuna nafasi kwa ajili yao. Siku zote nilikuwa nalaani kitu ambacho wanakiita ‘brain drain’, yaani, ile hali ya watalaamu wetu kwenda kutumia bongo zao kufanya kazi nchi za nje na kutufanya tupungukiwe na wataalamu. Lakini do kumbe huwa tunawapoteza humu humu nchini!

Sasa kuna wanaomshauri mhitimu huyu akafanye kazi yoyote na sio lazima ihusiane na utaalamu aliousomea. Lakini utamaduni huu ndio umesababisha tupoteze fursa ya kuendelea kisayansi na kiteknolojia. Hii ndio hali halisi ya Tanzania iliyomfanya Erasto Mpemba asiwe Mwanafizikia!

Alipokuwa mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari ya Magamba, Mpemba alivumbua kitu ambacho kilikuwa hakijulikani kabla. Aligundua kuwa katika hali fulani maji ya moto huganda haraka kabla ya maji ya baridi. Alipofika Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Mkwawa aliweza kuuelezea uvumbuzi huo kwa mtaalamu wa Fizikia ambaye aliuchapisha pamoja naye ambapo waliuita ‘Mpemba Effect’, yaani, ‘Taathira ya Mpemba’!

Na yule mwanafunzi wa Chuo Kikuu aliyegundua namna ya kupunguza maisha ya mbu wa malaria kwa kutumia mnyoo fulani ameishia wapi? Mara ya mwisho nilisikia akisifiwa kwenye vyombo vya habari ambapo Serikali ilisema itahakikisha uvumbuzi huo unaendelezwa na unatambuliwa kimataifa. Ila nilipoitembelea tovuti fulani niliona kuwa sehemu kubwa ya sifa hizo zimechukuliwa na taasisi fulani ya nje ya nchi ambayo inasemekana ilisimamia utafiti huo!

Baada ya Rais Kikwete kuhutubia wahandisi mnamo Septemba, 2008 ambapo alisisitiza tusomeshe wahandisi niliandika makala iliyohoji ‘wako wapi hao maelfu ya wahandisi tuliokwishawasomesha?’ Jibu lililopatikana ni kuwa wengi wameacha kazi ya uhandisi na wengine wameenda ughaibuni kwenye maslahi na tija zaidi. Mimi binafsi nawafahamu wengi tu.

Tufanye nini basi ili tusipoteze wataalamu wetu? Jibu ni rahisi. Tuwekeze katika rasilimali watu!

© Chambi Chachage – Mwananchi (19 Mei 2009)

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP