Thursday, July 9, 2009

Kumbukizi: Shule na Kweli Urithi wa Kweli


Sioni mito kauka, kwa miti ilosimama,
Soma soma acha soka, hakuna kama kusoma,
Nitafakari mi-kaka, mwingine hata sukuma,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.

Ewe Chachage makini, rafiki mweny fikra,
Hukusaidia nani, kuenenda kwa ubora,
Uliasa fikirini, elimu si biashara,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.

Inapendeza kutana, kukumbuka mashujaa,
Mwanazuoni mwanana, wewe kweli ushujaa,
Hakuna wa kufanana, kwa kweli ulienea,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.

Tazama haupo upo, twakiri wewe ni modo,
Tupo nawewe tulipo, kukumbuka yetu modo,
Fikrazo zingalipo, pambano lingali bado,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.

Hapa karibu simama, twakukumbuka milele,
Kwenye kweli ni salama, tuseme bila simile,
Wote tusimame wima, kwa kumuenzi milele,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.

Yale yako ni maisha, yaliyojaa mfano,
Maovu ulikomesha, penye kila mapambano,
Kalamu ilikutosha, kushinda lote pambano,
Shule ya kweli na kweli, ndio urithi wa Kweli.
----------------------------------------
"Nashukuru sana kwa taarifa ya usiku wa kumbukizi ya miaka mitatu toka mpendwa wetu Chachage atutoke. Ningependa kuwepo, lakini majukumu yamefanya niwe mbali na eneo la tukio hilo muhimu. Lakini napenda kufanya kitu ambacho nimekuwa nafanya kwa nadra sana toka nimalize shule ya msingi. Lakini pengine si kitu kigeni kabisa, kwa sababu, nakumbuka Chachage na Demere walipokuja Mtwango kwa mara ya kwanza pamoja na kujadili mimi kuhamishwa kutoka shule ya Sovi kwenda Mtwango Shule ya Msingi, Carbon Dioxide (CO2) iliyokuwepo pale tulipo na jinsi tulivyopishana na Oxygen (O2) tukifungua dirisha, pia tulijadili vitu ambavyo nilikuwa nafanya zaidi ya kusoma shule na kucheza soka. Kwa kifupi niliwaaambia huwa naandika mashairi pia. Kwa bahati mbaya sana siku ile hata baadaye sikufanikiwa kuwaonyesha mashairi niliyopata kuandika. Hata hivyo baada ya kusoma email yako leo asubuhi ihusuyo kumbukizi ya Chachage nikaamua moyoni mwangu kwamba ni lazima niandike shairi dogo kwa ajili hiyo. Ili nipate mtiririko wa fikra nilianza kwa kuandika neno SEITHY kwa kwenda chini ya karatasi yangu na kuanza kupanga vina na mizani yangu. Na mwisho nikamaliza na kichwa cha shairi lenyewe ambacho ni Shule na Kweli urithi ni wa Kweli. Naomba tafadhali kama hujali uniwasilishie beti zangu tano (5) kwenye usiku wa Chachage. Wape salamu tele ndugu na jamaa wote"

Zurich, Switzerland
8 July 2009

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP