Loading...

Wednesday, August 12, 2009

Blogu zinachochea au zinafifisha uandishi?

Hizi ni ‘Zama za Utandawazi.’ Hivyo ndivyo wasomi fulani wanavyotuambia. Hakika mtandao wa mawasiliano umepanuka. Hata mizunguko imeongezeka na wanamtandao wamekuwa wengi.

Hali hii ya kuongezeka kwa mwingiliano na kukua kwa mawasiliano ulimwenguni inajulikana kama kutandawaa. Huko kusambaa kumeikuza kwa kasi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo sasa inajulikana kwa kifupi kama Teknohama. Hata hivyo, Utandawazi – ambao wanaharakati na wanamapinduzi fulani wanauona kuwa ni Ubeberu uliojigeuza jina tu –haujaifanya Teknohama iwafikie watu wa nasaba na matabaka yote duniani kwa usawa.

Blogu ni aina mojawapo ya Teknohama ambazo zimeibuka hivi karibuni kutokana na kutandawaa huku. Kama lilivyo gazeti, redio au runinga/televisheni, Blogu ni chombo cha habari kinachotumika kufikisha taarifa au habari fulani kwa kutumia maandishi, maneno, picha na kadhalika. Hata hivyo, chombo hiki cha habari kinatumia kinakilishi/kompyuta au simu iliyounganishwa kwenye mtandao maalumu wa mawasiliano ili kufikisha ujumbe.

Baadhi ya Blogu maarufu zinazohusu Tanzania ni ‘Blogu ya Jamii’ inayomilikiwa na Muhiddin Issa Michuzi, Swahili Time’ inayoendeshwa na Chemi Che Mponda, ‘Nukta77’ inayosimamiwa na Subi Sabato, na BongoCelebrity’ inayohaririwa na Jeff Msangi.

Japokuwa Blogu ni aina ya chombo cha habari ambacho bado hakijatimiza mwongo mmoja – yaani miaka kumi – hapa Tanzania, hivi sasa kuna wanablogu wengi sana. Utitiri huu wa Blogu unatokana na ukweli kuwa kwa kiasi fulani hiki ni chombo huria ambacho mtu yoyote mwenye fursa au uwezo wa kutumia mtandao anaweza kukimiliki bila gharama zozote mbali na zile za kulipia mtandao wenyewe na kompyuta au simu. Hivi sasa kuna tafiti zinaendelea kuhusu wingi wa Blogu nchini na matumizi yake.

Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa kuna aina nyingi za Blogu zinazohusu Tanzania na kwa namna moja au nyingine zinahusiana na fani ya uandishi. Maswali muhimu ya kujiuliza kuhusiana na suala hilo ni: Je, hizi Blogu zinachochea au kufifisha fani uandishi na usomaji? Ni kwa namna gani Blogu zinakuza au kudumaza sanaa na stadi za uandishi na usomaji?

Tuanze na Blogu ya Jamii ambayo pengine ndiyo maarufu kuliko zote hapa nchini. Ukiitembelea utaona kuwa inajaribu kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali kama vile: wanaopenda burudani hasa za picha, vikaragosi na video; wanaopenda taarifa mbalimbali za kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi; na wale ambao wanapenda mijadala, midahalo na maswali.

Tukiutafsiri uandishi kama aina yoyote ya matumizi ya maandishi kufikisha ujumbe, hakika Blogu ya Jamii inauchochea na kuukuza. Ukiifuatilia Blogu hii utaona jinsi ambavyo waandishi mbalimbali wanatuma maandishi yao humo na jinsi wasomaji mbalimbali wanavyotoa maoni yao kuhusu maandishi hayo humo humo kwenye Blogu. Kuna baadhi ya maandishi yanapata maoni kutoka kwa watu hata zaidi ya mia moja kwa siku!

Lakini tukiamua kuutafsiri uandishi kama fani inayozingatia misingi fulani ya kisanii, kiufundi na kitaaluma basi kuna uwezekano mkubwa kuwa Blogu ya Jamii haichangii sana katika kukuza fani hii. Hii inatokana na ukweli kuwa maandishi mengi yanayowekwa humo yamejikita zaidi katika kufikisha ujumbe mfupi na kwa haraka ambapo nia kuu inakuwa ni kupasha habari, kuuliza maswali, kujibu hoja au kutoa burudani. Mara moja moja kunakuwa na maandishi ya kisanii kama vile mashairi, ya kiufundi kama vile insha, na ya kitaaluma kama vila ripoti ila kwa ujumla uandishi katika Blogu hii unazingatia zaidi maudhui kuliko fani.

Licha ya hayo Blogu ya Jamii inachochea fani ya picha/taswira pengine kwa sababu mmiliki wake ni mpiga picha mahiri na mzoefu. Blogu hii pia imeunganishwa na Blogu zingine zikiwamo zile ambazo zimejikita zaidi katika uandishi kama fani (yenye maudhui). Mojawapo ya Blogu hizo ni ile ya mwandishi maarufu Majjid Mjengwa.

Mjengwa kwa kiasi kikubwa amekuwa akiitumia Blogu yake kama chombo cha kusambaza makala zake alizokuwa akiziandika katika magazeti mbalimbali kabla ya kuanzisha jarida la Kwanza Jamii. Japokuwa makala hizo zimejikita zaidi katika uchambuzi wa kisiasa, uandishi wake unajaribu kuwa na vionjo vyenye uwiano wa kisanii na kiufundi. Mizania hii inajidhihirisha hasa pale mwandishi anapotumia riwaya na hekaya mbalimbali katika uchambuzi wa matukio halisi.

Mwanablogu mwingine anayetumia Blogu kwa namna hii ni Mwandishi wa Habari na Mtunzi Mkongwe, Ndimara Tegambwage. Blogu yake inajitambulisha kwa Kauli Mbiu: ‘Uhuru Hauna Kikomo. Kikomo Kinawekwa na Maadui wa Uhuru.’ Maandishi mengi yaliyomo humo yanatokana na safu yake ya ‘Sitaki’ katika gazeti la Tanzania Daima.

Dondoo hii kutoka katika Blogu ya Tegambwage inaonesha mfano wa matumizi ya fani ya uandishi yenye usanii unaowiana na ufundi: “Kwa hiyo, kwa kusoma ndani ya ‘habari chakupewa,’ mwandishi mzuri huweza kuanza kufuatilia habari yenyewe, isiyovalishwa vilemba au vitenge; isiyopakwa mafuta na kupuliziwa pafyumu. Isiyolenga kusifia na kutukuza watawala, bali yenye nguvu ya kutoa ujumbe sahihi kwa watawala na wataliwa”!

Dalili zinaonesha kuwa watu wengi wataendelea kuanzisha Blogu zao ilhali wanablogu wengi watashindwa kuendesha Blogu zao. Tayari kuna Blogu nyingi ambazo hazijatumika kwa muda mrefu kutokana na wanablogu wake kukosa muda au kutopata cha kuandika. Pia inaonekana kuwa Blogu zinazowavutia wengi ni zenye maandishi machache, picha nyingi na vichekesho vingi.

Inaonekana kuwa, kwa sasa kuna ushindani mkubwa, wa kupata wasomaji, kati ya Blogu mbalimbali ambapo zile za burudani na wasifu zinaelekea kupata wachangiaji wengi zaidi, zikifuatiwa kwa mbali kiasi na zile za siasa na harakati. Inaonekana pia kuwa Blogu na Teknohama kwa ujumla zinafifisha utamaduni wa kuandika na kujisomea vitabu. Katika Jimbo moja huko Marekani inasemekana kuwa maandishi yaliyowekwa mtandaoni yataanza kutumika kufundishia mashuleni badala ya vitabu vya kiada. Je, Blogu zitatokomeza vitabu?

Ili kuziwezesha Blogu kuwa kichocheo cha uandishi ni lazima kuwe na uwiano kati ya maandishi na taswira. Pia ni muhimu kukuza vipaji vya uandishi wenye mvuto. Kwa mtaji huo, chombo huria kama hiki kikitandawaa sawia na kuwafikia watu wengi kitaondoa urasimu na ukiritimba wa wachapishaji wa magazeti na majarida. Na Blogu zitazalisha vitabu!

© Chambi Chachage - Imechapishwa kwenye Toleo la 3 la Soma

1 comments:

Tandasi August 17, 2009 at 1:05 PM  

ni hakika blogu zaweza kutia mashaka flani kwa magazeti na vitabu, lakini hii sana kwani kitabu au gazeti huweza kufika blogu zisikoweza kufika vitabu, vinaweza kufichwa blogu zisikofichika ni mimi Tandasi wa ndotoyangu-harakati.blogspot.com nakualike unisome pia

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP