Loading...

Thursday, September 17, 2009

UNAPOKUWA MWANAMKE MCHONGAJI

UNAPOKUWA MCHONGAJI MWANAMKE

Imeandikwa na Mwandale Mwanyekwa na Bob Sankofa

Mara nyingi kila ninapokaa na marafiki ama hata wapita njia huwa hawaachi kuniuliza maswali mengi kuhusiana na kazi ninayofanya, uchongaji. Lakini wengine huwa wanakwenda mbali zaidi na kuniuliza najihisi vipi kuwa mwanamke mchongaji katika fani ambayo kwa kitambo sasa imekuwa ikitambulika zaidi kama fani ya wanaume. Mara nyingi huwa natamani kuwapa jibu la jumla, kwamba, “Kama wanawake tunaweza kuwazaa wanaume basi hakuna anachofanya mwanaume mwanamke akishindwe”.

Jibu la namna hii linaweza kuwa tata kwa rafiki zangu wengine, maana wapo marafiki wa kiume wasioamini kwamba kazi yeyote inayoweza kufanywa na mwanaume basi hata mwanamke anaweza, halafu mbaya zaidi wapo marafiki wa kike ambao wamelambishwa sumu ya kuamini kwamba yapo mambo ni kwa ajili ya wanaume pekee.

Sasa mara nyingi huwa nakumbana na changamoto hii, na mara karibu zote ili kuthibitisha imani yangu kwa watu wengine, imani ya kwamba anachoweza mwanaume na mwanamke anaweza, huwa inanilazimu kuzungumzia hisia juu ya kazi yangu kwa kumualika muuliza swali kuitalii historia yangu.

Kila ninapozungumzia historia ya kazi yangu, mimi binafsi hujihisi kama ndio ninaipitia mara ya kwanza. Kila wakati najifunza jambo jipya ninapotazama historia yangu. Hadithi yangu ni moja ya hadithi nyingi, tena zinazoshabihiana, za binti anayezaliwa katika nchi ya Tanzania, na pengine katika bara la Afrika. Ni hadithi ambayo mara nyingi huanza na Baraka nyingi lakini zisizokosa vikwazo njiani.

Baraka ya kwanza ni kwamba mama aliyenibeba tumboni kwa miezi tisa ni Mmakonde, kwa takwimu za haraka ni wazi kwamba kabila la Wamakonde, wenyeji wa kusini mwa Tanzania, ndio wachongaji wanaofahamika zaidi ndani ya nchi hii. Kwa hivyo, naweza kusema sikuchagua kuwa mchongaji, bali uchongaji ulinichagua. Nimekulia kijijini kabisa na katika utoto wangu nilizungukwa na familia nyingi za wachongaji, japo wengi kama si wote, walikuwa ni wanaume.

Baraka ya pili ni kwamba babu yangu mzaa mama yangu alikuwa ni fundi seremala na pia mchongaji wa vinyago, kwa hivyo nilianza kucheza na vifaa vya uchongaji nikingali binti mdogo kabisa, na kwa bahati nzuri babu yangu alifurahi nilipokwenda kucheza katika karakana yake.

Napenda kusema hapa kwamba kama babu yangu angekuwa akifanya kazi nyingine labda nisingekuwa mchongaji leo. Lakini si hivyo tu, iwapo nafsi ya babu yangu ingekuwa imetawaliwa na mfumo dume, pengine leo nisingekuwa mchongaji mwanamke, fursa niliyopewa na babu yangu ni mchango mkubwa uliosababisha niwe mwanamke ninayepambana katika fani inayosemekana kuwa ni ya wanaume.

Ni vigumu kujibu swali lililoulizwa bila ya kumuhusisha bibi yangu mzaa mama katika kufanikiwa kwangu kuwa mchongaji mwanamke, ama mwanamke mchongaji. Bibi yangu alikuwa mfinyanzi mzuri wa mitungi na vyungu. Kabla ya kufikia umri wa kwenda shule za serikali, tayari nilikuwa nimeshakwenda shule ya nyumbani. Kwa maana hiyo basi iwapo usingenikuta kwenye karakana ndogo ya babu yangu, ungenikuta pembeni ya bibi yangu nikitengeneza wanasesere wa udongo.

Nadhani ujuzi wangu wa kuchonga vinyago ulianzia hapa zaidi, na pengine nisingekuwa mchongaji basi lazima ningekuwa mfinyanzi. Ni kazi mbili nilizozipenda kuliko chochote kingine, ni kazi nilizoamini wazi kabisa kwamba ningependa kuzifanya katika maisha yangu hapa duniani.

Kazi ya uchongaji niliichagua mapema kwa sababu katika kijiji changu wakati watoto wote wa kike wa umri wangu tulipokuwa katika umri wa kutengeneza wanasesere ulipopita, wenzangu waliachana na mchezo huo lakini mimi niliendelea na sikuwahi kuacha. Baadae nikaanza kuchonga vijisanamu vidogo kwa kutumia miti ya mihogo na wakati mwingine hata mihogo mibichi, sikuwa nikichonga kwa ustadi sana lakini nilijuwa wazi kuwa ninaweza kuchonga hata kwenye mti mgumu kama nikiweka bidii.
Mapenzi yangu kwa sanaa hii yalinifanya kuoneka
na mwenye upungufu, tofauti na watoto wengine. Wengi waliona kama nimekataa kukua. Nilipoanza shule ya msingi sikuwa mwanafunzi mzuri sana darasani, sikuelewa kwa haraka kwa nini watu wanafundishwa vitu wasivyo na mapenzi navyo. Nina uhakika kama shuleni wangefundisha somo la kuchonga labda na mimi ningekuwa mmoja wa wanafunzi mahiri katika masomo. Ingekuwa rahisi kwangu kuelewa somo langu kwa sababu nilikuwa nalipenda.

Elimu yetu ya darasani, inatupima kwa maandishi, labda ingekuwa inatupima kwa matendo pia na mimi ningefanikiwa kwenda shule ya sekondari kama wenzangu, lakini kwa sababu akili yangu ilikuwa kwenye vinyago wakati wote, safari yangu ya darasani ikaishia hapo. Sikuwa na sifa za kwenda shule ya sekondari kwa sababu mtihani wangu wa nadharia pekee haukunipa nafasi.

Mara nyingi watu huniuliza iwapo ninasikitika kwa kutopata nafasi ya kwenda elimu ya juu. Huwa nasikitika kwa sababu ukweli ni kwamba sikukataa kwenda elimu ya juu lakini sikuweza kufikia vigezo vya watahini kwa wakati huo. Kwa upande wa pili sijutii kwa sababu labda ningeenda elimu ya juu na mimi ningekuwa kama wenzangu wengi wanaopenda kuvaa suti na kukaa kwenye kiti cha kuzunguka ofisini lakini wasifurahie kazi wanayofanya. Ofisi yangu ni chini ya mwembe, vazi la kazi yangu ni ovaroli, lakini ninayo furaha moyoni ya kufanya kile ninachokipenda. Nina imani hata siku Mungu atakapoamua kufanya hesabu ya namna nilivyotumia muda wangu kujiletea furaha moyoni, hatosikitika, ataona wazi kuwa nilifanya kile alichoniagiza kuja kukifanya hapa duniani.

Sikuamka siku moja na kujikuta nimekuwa mchongaji mwanamke, niliingia dunia hii nikitambua kuwa nataka kuwa mchongaji mwanamke. Tangu nilipofahamu nilichohitaji kwenye maisha yangu nimeweka akili, roho, mwili, muda, na moyo wangu kwenye tamanio langu. Si kwamba akili yangu inawaza uchongaji muda wote, la hasha, huwa nawaza kujipamba pia kama wanawake wengine wote, lakini ukweli ni kwamba hata ninapojipamba nusu ya mawazo yangu yapo kwenye kazi yangu.

Ni kwa kuwa na imani kama hii ndiko kulikorahisisha kazi yangu na kuyaweka mazingira ya kazi yangu katika hali ya mteremko. Umakini wangu kazini ndio ulionijengea heshima katikati ya wanaume, wananiheshimu na kunipenda, wananisaidia sana pia. Walimu wa kazi yangu ni wanaume na wanawake, kila mmoja kwa nafasi yake. Soko la kazi yangu ni la wanaume na wanawake, kila mmoja kwa nafasi na maono yake.

Hali hii inanifanya kila wakati nijiulize, “Kwa nini nisiwe mwanamke mchongaji au mchongaji mwanamke wakati uwanja uko wazi kwa ajili yangu?” Swali hili hunifanya kukamata gogo na patasi na kutengeneza kinyago. Huwezi kuitwa mchongaji mwanamke au mwanamke mchongaji bila kuchonga.

Kwa hivyo basi, mimi ni mwanamke mchongaji kwa sababu ninachonga na kuhusu ninajisikia vipi kuwa katika fani ya wanaume ukweli ni kwamba “Mara zote mtazamo wangu ni kwamba kazi yangu ni zaidi ya jinsia, kazi yangu ni sehemu ya uumbaji na katika uumbaji Mungu amemshirikisha kwa karibu zaidi mwanamke kwa kubeba mimba kwa miezi tisa. Lakini Mungu alifahamu pia kwamba uumbaji hautakamilika asipokuwepo mwanaume, na vivyo hivyo kinyume chake. Kwa hivyo najisikia vyema kukamilisha uumbaji kwa kujumuika katika FANI YA WACHONGAJI”

Afrika imekwishaamka, na mwanamke kama alivyo mwanaume amekwishaamka. Yanayotuunganisha ni makubwa kuliko yanayotutenganisha. Siku mwanamke na mwanaume watakapoamua kushikana mikono, na tayari kazi hii imekwishaanza, basi itakuwa neema kwa dunia hii maana hatutakuwa na wakati wa kupoteza tukimjadili ‘mchongaji mwanamke’ bali kama ilivyo kwa wanaume, mwanamke atatambulika kama “Mchongaji”.

Mwanamke asimame sasa na mwanaume asimame pamoja nae ili miaka michache tangu sasa mtu asihukumiwe kwa jinsia yake bali kwa ubora wa kazi au fani yake.

Najisikia huru kuwa mchongaji. UHURU SASA, UHURU MILELE!

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP