Loading...

Friday, September 4, 2009

WARSHA YA WASIFU WA WANAWAKE KAMA WAZALISHAJI, WATUNZAJI NA WATOAJI WA MAARIFA NA WAENDELEZAJI WA UTAMADUNI


WARSHA YA 4 YA TAMASHA LA 9 LA JINSIA

ALHAMISI 10 SEPTEMBA 2009

SAA 5 ASUBUHI – SAA 11 ALASIRI

VIWANJA VYA MTANDAO WA JINSIA TANZANIA (TGNP)

MABIBO, DAR –ES- SALAAM

Wasifu wa Wanawake kama Wazalishaji, Watunzaji na Watoaji wa Maarifa na Waendelezaji wa Utamaduni na Historia Mbadala ya Jamii

Utangulizi
Warsha hii inaangalia umuhimu wa mwanamke katika kuvumbua, kuhifadhi na kusambaza maarifa, ufahamu au ujuzi wa masuala mbalimbali katika jamii. Katika jamii mbalimbali mwanamke amekuwa kiungo na msingi mkuu katika kuzalisha, kutunza na kukuza utamaduni na historia ya jamii husika. Lakini kutokana na mfumo dume kuota mizizi katika jamii hizi, nafasi hiyo ya mwanamke ama imekuwa haitambuliwi ipasavyo na kusahauliwa sana au kwa makusudi kabisa imewekwa pembezoni kana kwamba wanaume pekee ndio wanajishughulisha na uzalishaji na umiliki wa rasilimali ya maarifa.

Kwa kuzingatia mada kuu ya Tamasha la Tisa la Jinsia -2009 lenye Kaulimbiu ya ‘Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walio Pembezoni’, washiriki wa Warsha ya Nne watamtambua na kumbainisha na kumrudisha mwanamke aliyeko pembezoni katika nafasi yake muhimu kama mmoja wa wazalishaji, watunzaji na watoaji wa maarifa yanayohusiana na matumizi na hifadhi ya rasilimali hizi ambazo zinapaswa kumnufaisha kama zinavyowanufaisha watu wengine ambao hawako pembezoni.

Maarifa na Utamaduni kama Nyenzo za Vuguvugu la Ukombozi wa Wanawake
Tunapozungumzia maarifa na utamaduni ambao mwanamke ni mshiriki mkuu wa uzalishaji, utoaji na usambazaji wake tunamaanisha nini hasa? Tunamaanisha kuwa maarifa ni yale mambo yote ambayo jamii au watu fulani katika jamii wanayajua na kuyatumia kama mbinu au nyenzo ya kutumia rasilimali zao ili kujikimu na kujiletea maendeleo yao. Hali kadhalika tunamaanisha kuwa kwa ujumla wake maarifa hayo yote ndio utamaduni wenyewe wa jamii hiyo na wanajamii wake.

Kwa mfano, rasilimali kuu ya ardhi imekuwa ikitunzwa na kutumiwa kwa namna tofauti katika jamii mbalimbali. Maarifa kuhusu matumizi hayo ya ardhi ni kama vile kupumzisha ardhi katika kipindi fulani ili ipate rutuba kwa ajili ya msimu mwingine wa kilimo katika jamii za wakulima au malisho katika jamii za wafugaji. Kwenye jamii husika maarifa haya yamekuwa yakirithishwa kutoka kwenye kizazi kimoja hadi kingine na hivyo kuendelea karne hadi karne na kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii hiyo. Jamii za wafugaji wa Kimaasai na Kibarabaig, kwa mfano, zimekuwa na utamaduni wa ufugaji wa kuhamahama ambapo wakati wa msimu wa kiangazi zinaliaacha kwa muda eneo fulani lenye rutuba lipate muda wa kuchipusha majani zaidi na kurutubisha vyanzo vya maji. Katika kipindi hicho jamii hiyo itakwenda kwenye maeneo mengine na baada ya msimu huo kuisha itarudi tena kwenye eneo la awali ambalo sasa litakuwa na uwezo wa ziada wa kustahimili wingi wa mifugo yao bila kuchoka na kupoteza rutuba yake hadi msimu ujao wa kuhama utakapoanza. Mwanamke katika jamii hizi amekuwa ni mshiriki muhimu katika kukuza na kuhifadhi maarifa haya hasa ukizingatia kuwa katika jamii za Kimaasai amekuwa mstari wa mbele katika maarifa ya ujenzi wa maboma ya kudumu na yale ya muda kwa ajili ya uhamaji.

Warsha hii inampa changamoto kila mshiriki kujiangalia kwa undani yeye mwenyewe na jamii inayomzunguka kuona ni ujuzi na maarifa gani ambayo yeye au wanawake walio pembezoni wanayavumbua, wanayakuza na wanayasambaza kama sehemu ya utamaduni wao. Je, yule mwanamke anayechota maji kwenye kisima kile cha maji kilicho mbali na pale anapoishi ana maarifa gani kuhusu namna ya kupata rasilimali hiyo ambayo imekuwa adimu bila sababu ya msingi na, je, maarifa hayo yanamsaidiaje yeye na wenzake katika kupata, kuhifadhi na kutumia maji hayo katika namna endelevu? Harakati za mwanamke huyu na wenzake kupata maji zinafanikiwa kwa kiasi gani na,je, mafanikio hayo yanasambazwa kwa wanajamii wengine ambao nao wana changamoto ya upatikanaji wa maji?

Je, maarifa ya Bibi yule katika Kijiji kile aliyekuwa anatumia chungu cha asili kuyafanya maji yawe ya baridi pamoja na kuwa safi na salama , yamehifadhiwa na kurithishwa kwa kizazi kinachofuata au yamesahauliwa kwa kuwa baadhi ya watu katika jamii wana majokofu? Na ule ujuzi wa Dada yule kwenye Mtaa ule katika kutambua ni wapi panafaa kuchimba kisima chenye maji ambayo siyo ya chumvi au magadi umehifadhiwa na kusambazwa kwa wengine ambao wanahitaji maji ya aina hiyo kwa muda wakati wanaendelea na harakati za kuhakikisha maji ya bomba yanapatikana kwa kila kaya nchini?

Mifano hiyo ya maarifa kuhusu ardhi na maji ambazo zinahesabika kama rasilimali muhimu sana ni sehemu ndogo tu ya maarifa ambayo wanawake, wakiwamo wale walio pembezoni, wameyazalisha na wanaendelea kuyazalisha. Changamoto kubwa inayotokana na mfumo dume ni, je, maarifa haya yanahifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo kama sehemu ya utamaduni wa jamii husika na kama mchango muhimu wa wanawake katika kuiendeleza jamii hiyo. Kama utamaduni ni jumla yote ya masuala ya jamii kama wasomi wetu wanavyotukumbusha, je, mwanamke aliyeko pembezoni anatambuliwa kama mshiriki muhimu katika jumla yote ya masuala hayo ya jamii yetu/zetu?

Warsha hii pia inaangalia upande wa pili wa shilingi ambao mwanamke anashiriki katika kuzalisha na kuhifadhi maarifa yanayoishia kuwa nyenzo za kumkandamiza na kuikandamiza jamii yake pamoja na kujenga utamaduni wa kukubali ukandamizwaji. Lakini warsha hii haiishii hapo tu bali inaangalia ni jinsi gani maarifa hayo hayo yanatumiwa au yanaweza kutumiwa na wanawake kama nyenzo ya harakati za kupinga utamaduni/maarifa kandamizi na kujikomboa dhidi ya mawazo na mifumo ya mahusiano inayoelekezwa na taasisi na itikadi ya mfumo dume na mifumo kandamizi mingine kama vile ile ya ubaguzi wa rangi na ubepari wa kibeberu.

Kuwatambua na Kuwabainisha Wanawake kama Wadau Muhimu wa Maarifa
Ili kutimiza lengo lake kuu la kumrudisha mwanamke aliyeko pembezoni mwa jamii kwenye nafasi yake halisi, yaani awe ‘katikati ya jamii’, warsha hii itatumia mbinu ya ‘Vunja Ukimya – Sema Usikike!’ Hii mbinu itahusisha kuwapa nafasi washiriki kuelezea wasifu wao na kutoa visa mkasa au shuhuda ya kile wanachokifahamu, namna walivyokifahamu na jinsi ambavyo wanawafahamisha wengine. Warsha hii itakuwa uwanja wa kupashana habari na kubadilishana uzoefu kuhusu maarifa mbalimbali ambayo ni zao la wanawake hasa wale walio pembezoni. Maarifa haya yatakusanywa na kusambazwa kwa jamii na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo kama sehemu muhimu ya jamii hii. Hivyo, warsha hii itakuwa na matukio haya:

1.Maelezo kutoka kwa Washiriki kuhusu Maarifa yatokanayo na Mchango wa Wanawake
2. Maonyesho ya Magazeti na Vitabu vyenye Wasifu wa Wanawake Mbalimbali Tanzania
3. Mada kuhusu Kumbukumbu kutoka kwa Mwangalizi wa Nyaraka na Maktaba (Mkutubi)
4. Mahojiano ya Wazi na Wanawake Walioandika au Walioandikiwa Wasifu katika Magazeti
5. Mafunzo kuhusu kujiandikia kwa urahisi Kitabu cha Kumbukumbu za kila Siku (Shajara)
6. Majadiliano kuhusu ‘Maarifa Simulizi’ na Changamoto ya kutojua Kusoma na Kuandika
7. Mkanda wa Video kuhusu Harakati za Wanawake kupata na kutoa Taarifa na Maarifa
8. Maswali na Majibu kati ya Washiriki na Wataalamu wa Maarifa Asilia na Tiba za Jadi


Washiriki wafuatao na wengineo wanatazamiwa kujumuika na Wanatamasha katika warsha hii:

(i) Wahariri wa Kijarida cha Woman (Mwanamke) wa Gazeti la Daily News
(ii) Wahariri wa Kijarida cha Woman (Mwanamke) wa Gazeti la The Citizen
(iii) Waandishi wa Wasifu na Maarifa ya Wanawake katika gazeti la Mwananchi
(iv) Waandishi wa Gazeti la Si Mchezo! la Femina HIP na waliotoa Stori Yangu
(v) Wanawake 2 waliohojiwa na kuandikiwa wasifu kwenye Gazeti la Lucky!
(vi) Wachapishaji wa Andika Afrika na Wadau wa Gazeti la Startup Biashara
(vii) Wakutubi 2 kutoka Maktaba Kuu na ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
(viii) Wakunga wa Jadi na Waganga Rasmi wa Tiba Asilia na Mitishamba

Hitimisho
Baada ya kupata Uhuru na kuwa Jamhuri Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitukumbusha kuwa katika makosa yote ya ukoloni hakuna lililo baya kupita jaribio lao la kutufanya Watanzania tuamini kuwa hatukuwa na utamaduni wetu au kile tulichokuwa nacho hakikuwa na thamani yoyote. Warsha hii ni sehemu ya jitihada za kutambua kuwa kile tulicho nacho – yaani maarifa yetu na utamaduni wetu – kina thamani na umuhimu na kuwa wale wote wanaozalisha maarifa hayo wanapaswa kutambuliwa. Na kama alivyosema mwanamaarifa mmoja, kuna nafasi kwa kila mtu kwenye uwanja wa ushindi dhidi ya ukandamizaji. Ndio, kuna nafasi kwa kila mtu – mwanamke na mwanaume aliye pembezoni na asiye pembezoni – kwenye ulingo wa kuzalisha na kukuza maarifa ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP