Loading...

Monday, December 21, 2009

MATUNDA YA DHULUMA NA UNYANYASAJI WA JAMII YA WAFUGAJI HANANG'

Kwa mara nyingine wiki iliyopita Taifa la Tanzania limepata doa jingine katika kile tukiitacho amani na utulivu, hizi ni nyimbo tumezokuwa tukiaminishwa na kuimba kila uchao bila kujali kuwa katika uhalisia wa mambo hatuwezi kujidai kuwa kisiwa cha amani na utulivu katika mazingira ya unyanyasaji, dhuluma na ubinafsi uliopita kipimo wa baadhi miongoni mwetu. Katika kudhihirisha kuwa hali si shwari baada ya dhuluma ya miongo takribani mitatu jamii ya wafugaji wa Hanang katika nyanda za malisho za Bassotu wameamua kuvunja ukimya na kuionyesha Tanzania na dunia kuwa sasa wamefika ukomo wa subira na uvumilivu. Wazalendo wa Hanang’ baada ya kilio chao cha muda mrefu kwa serikali ili warejeshewe mashamba yao yaliyopokwa mwishoni mwa miaka ya 70 na serikali ili kuanzisha kilimo cha ngano tena kwa kutumia nguvu wameamua kuvunja ukimya.

Ili kuyaelewa matukio haya vyema ni bora kurejea nyuma na kuangalia historia ya eneo lenye mgogoro. Mashamba ya Gawal, Setchet, Murjanda, Gidagamowd, Mulbadaw, Bassotu na Warret yanapatikana katika iliyokuwa nyanda ya malisho ya Bassotu (Bassotu Plains), Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K Nyerere iliamua kuyachukua maeneo haya kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa ya ngano chini ya mradi uliokuwa ukiendeshwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO) kwa msaada wa Serikali ya Canada kupitia shirika lake la Msaada la Kimataifa CIDA, takribani ekari 100,000 zilichukuliwa kutoka kwa wakazi ili kutimiza lengo la kilimo cha ngano.

Kimsingi nyanda hizo za malisho zilikuwa zikikaliwa ama kutumiwa na jamii za wafugaji wa Ki Datoga na Ki Iraqw. Serikali iliwaondoa kwa nguvu wakazi wa maeneo haya ili kupisha utekelezwaji wa mradi huo, kijiji kama cha Mulbadaw kiliathirika kwa sehemu kubwa na wakazi wake ambao kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Shivji na Dk Tenga na ripoti yake kutoka katika Jarida la Africa Events la Disemba 1985 ikiitwa Ujamaa mahakamani, kijiji hicho kilichosajiliwa kama kijiji cha Ujamaa kwa mjibu wa sheria ya Vijiji na Vijiji vya Ujamaa ya mwaka wa 1975, ni mojawapo ya vijiji katika eneo hilo vilivyoathrika na upokaji huo. Wakionyesha kupinga unyang’anyi huo wakazi wa maeneo hayo walifungua kesi kupinga dhuluma hiyo, mojawapo ya kesi maarufu ni kesi ya Mulbadaw Village council and Others V National Agricultural and Food Corporation (NAFCO) na kesi nyingine ni kesi maarufu ya Mzee Yoke Gwaku na wenzie.

Mahakama kuu kanda ya Arusha katika uamuzi wake wa awali iliwapa ushindi wakazi wa maeneo hayo na kuamuru NAFCO kuwapisha waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali, NAFCO walikata rufaa Mahakama ya Rufaa ambayo iliamua kutengua maamuzi ya Mahakama Kuu na kuwapa ushindi NAFCO, na kilichofuata baada ya hapo ni kuondolewa kwa nguvu katika maeneo hayo chini ya usimamizi wa FFU na maboma na makazi yao yakichomwa moto. Wafugaji wa Ki Datoga (Wabarbaig) wengi waliondoka katika maeneo hayo na kuhamia maeneo mengine nchini ambayo mpaka leo bado wanasumbuliwa wakiambiwa warejee walikotoka. Bahati nzuri kwa wakazi hawa shirika la NAFCO kama yalivyokuwa mashirika mengineyo ya serikali kutokana na usimamizi mbovu yalishindwa kujiendesha na hivyo kufilisika, Wa Datoga na wakazi wengineo wa nyanda za Bassotu walichukulia hiyo kama ishara ya Mwenyezi Mungu kujibu sala zao dhidi ya dhuluma waliyokuwa wametendewa, mategemeo yao ilikuwa ni serikali kuwarejeshea rasmi maeneo yao waliyonyang’anywa bila ridhaa yao mwishoni mwa miaka ya 1970.

Kilichotokea ni kwamba zama za utandawazi zilikuwa zimeshapiga hodi na mawazo ya serikali katika awamu zilizofuatia hayakuwa tena yakilenga zaidi wananchi na hivyo wafugaji na wakulima katika maeneo haya wakajikuta wakiambiwa mashamba tumeshindwa kuyaendeleza wenyewe hivyo wawekezaji watatusaidia kuyaboresha vyema. Wanavijiji wanaozunguka mashamba hayo wakaamua kuanza harakati upya kushinikiza mashamba haya kurejeshwa kwao, serikali baada ya mvutano na mapambano marefu ikaridhia kurejesha mashamba mawili kati ya saba. Sasa hapa ndio hasa tunapaswa kuwa makini, mashamba haya baada ya kurejeshwa yalirejeshwa katika mamlaka gani? Kimsingi katika suala la usimamizi wa ardhi serikali za vijiji kwa maana ya halmashauri za vijiji ndio zenye jukumu la usimamizi na kwa ushirikiano na Mkutano mkuu wa kijiji waweza kupanga namna watakavyotumia ardhi yao. Lakini kinachoendelea ni ukiritimba ule ule wa siku zote kwa serikali kuu kupitia Mkuu wa Wilaya na mara nyingine Halmashauri kutaka kulazimisha matakwa yao yasikilizwe.

Kinachoonekana hapa ni serikali ya wilaya kutaka kushinikiza serikali za vijiji husika kufanya kile ambacho wilaya inataka, kwa upande mmoja inaonekana kiini cha tatizo ni uamuzi wa wilaya kuwahamisha wanaowaita wavamizi wa Mlima Hanang’ hawa ni wakazi waliokuwa wakiishi katika nyanda za miteremko ya Mlima Hanang’ ambayo serikali imeamua sasa ni sehemu ya hifadhi ya Mlima wa Hanang’ maeneo mbadala serikali ya wilaya iliamua kuwa ni katika haya mashamba mawili waliyorejeshewa wanavijiji wanaoyazunguka mashamba haya.

Lakini hii hasa si hoja ya msingi, kama serikali ina nia ya dhati ya kuwapatia maeneo wakazi waliohamishwa kupisha hifadhi ya Mlima wa Hanang’ suluhisho sio kuwapambanisha wao na wakazi wa vijiji vilivyorejeshewa sehemu ya maeneo yao bali ni serikali kuona sasa pana haja ya kuhawilisha shamba ama mashamba mengine na kuwapatia wakazi hawa, hii ndiyo bila shaka maslahi ya kweli ya Taifa. Kuna hoja ya kwamba viongozi wa siasa wapite kuhamasisha wanavijiji wakubaliane na hoja za wilaya, kwanini viongozi hawa wa kisiasa wasiishinikize serikali ama kuishauri serikali ihawilishe mashamba mengine zaidi na kuwakabidhi wanavijiji waliohamishwa toka mlimani ama wengineo wenye mahitaji ya ardhi katika eneo husika?

Mwisho kabisa, enzi za kutumia mabavu na nguvu nyingi zimepitwa na wakati, hizi ni zama za kukaa pamoja na kuyaongea matatizo yetu kwa uwazi, fukuto la Hanang’ ni mfano tu wa matatizo mengi katika suala zima la ardhi yanayotukabili na yatakayoendelea kutukabili kama tutakuwa hatujajipanga katika suala zima la namna tunavyotumia ardhi tuliyokuwa nayo na vipaumbele vyetu. Ni vyema sasa tukaanza kuwaona wanavijiji kama wakala wa mabadiliko na maendeleo badala ya vikwazo ama vizingiti, wakiwezeshwa nao wanaweza kufanya mabadiliko, wakulima na wafugaji ndio wanaoubeba msitakabali wa taifa letu kwasasa, kama tunashindwa kuwapa fursa na nafasi inavyositahili tusishangae kesho tukasikia katika maeneo mengine pia wameingia msituni, kwani ilianza na Arumeru, kisha Hanang’ kesho sijui itakuwa wapi lakini tunafahamu yapo maeneo mengi ambayo kero za kweli za ardhi za wananchi zinafunikwafunikwa na watawala katika ngazi hizo.

1 comments:

Mzee wa Changamoto December 25, 2009 at 5:18 AM  

Kwenu wana UDADISI
Kwa niaba ya familia yangu na wapenda mema wote nawatakia kila lililo jema wakati huu wa sikukuu na usalama kuelekea mwaka mpya
Baraka kwenu

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP