Loading...

Tuesday, March 30, 2010

TAFAKURI TUNDUIZI: UWEKEZAJI NA UKOMBOZI

UWEKEZAJI NA UKOMBOZI WA MZALISHAJI MDOGO

Na Bernard Baha

Utwaaji mkubwa wa ardhi katika Afrika, Latini Amerika, Asia ya Kati na Kusini Mashariki umegonga vyombo vya habari kwa namna tofauti. Ardhi ambayo kimsingi haikuwa na thamani yoyote sasa inatwaliwa na wawekezaji wa kimataifa kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo ikihusisha utwaaji wa mamilioni ya hekta za ardhi. Kwa wakazi katika nchi ambako ardhi zinatwaliwa yaweza kuwa fursa ya kuboresha maisha lakini pia ukawa mwanzo wa kuingia katika lindi la umasikini na ufukara kwa wakazi kupoteza ardhi ambayo ndio msingi mkubwa wa maisha. Lakini kwa nchi za dunia ya tatu ardhi ndio utambulisho wa watu, maisha yao na uhakika wa chakula.

Wimbi hili halikuiacha Tanzania. Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuvutia wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta mbalimbali, kwa hiyo kimsingi uwekezaji ni sera ya taifa na kuna sheria zinazosimamia uwekezaji na vivutio aina aina vimewekwa kuandaa mazingira mazuri kwa wenye mitaji hasa kutoka nje kuwekeza. Uwekezaji toka nje hasa ndio unaonekana kama msingi wa maendeleo kwani wawekezaji hawa wanakuja kutoka mbali na mitaji yao na teknolojia ya kisasa, ujuzi na uzoefu ambao kimantiki ukitumika hapa nchi itafaidika kwa kupata teknolojia na wakazi katika maeneo husika ambako uwekezaji unafanyika kujifunza namna uzalishaji unavyofanyika.

Uwekezaji katika kilimo kwa mujibu wa viongozi wetu wa kitaifa pia unalenga katika kuwezesha maendeleo ya nchi lakini pia kwa wakazi kufaidika na fursa mbalimbali. Kuna aina mbalimbali za uwekezaji hasa katika sekta ya kilimo. Kuna wawekezaji ambao malengo yao ni kuwekeza katika mazao ya nishati uoto, kama vile mibono kaburi, miwa n.k, na kuna wale ambao wanalenga mazao ya chakula kama vile mpunga, mahindi na aina mbalimbali za nafaka.

Katika muktadha huu, je, ni kweli kuwa wanavijiji wanaotoa maeneo yao wanafaidika kwa lolote?

Kumekuwa na ripoti za malalamiko toka kwa wanavijiji juu ya kutwaliwa maeneo yao huku wakiachwa solemba, penginepo wakilipwa fidia kiduchu na kuahidiwa ahadi kemkem za maisha bora, ujenzi wa miundombinu kama barabara, zahanati, shule na ajira. Ahadi zote hizi kimsingi hutolewa ili kuwafanya wanavijiji waone umuhimu wa uwekezaji katika ardhi zao ingawa ukweli halisi kuwa wakiridhia utoaji wa ardhi ndio pia wamebariki mchakato wa uhawilishaji na ardhi kimsingi inakuwa katika kundi la ardhi ya jumla huwa hautajwi.

Jeuri ya wawekezaji wengi inakuja hapo hasa baada ya uhawilishaji kwani kimsingi mahusiano yao na wanavijiji waliotoa ardhi yanakuwa yameisha na hawawajibiki kwa lolote kwa serikali ya kijiji na hivyo basi hata wakiamua kujitolea kuchangia maendeleo inakuwa ni kile tukiitacho uwajibikaji wa kijamii kwa makampuni (Corporate Social responsibility) ambao ni hiyari ya kampuni kusaidia jamii iliyoko jirani na eneo la uwekezaji.

Katika nchi ambazo uwekezaji katika kilimo umewafaidisha wanavijiji serikali imekuwa msitari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wazalishaji wadogo katika vikundi wanajengewa uwezo wa kuendesha shughuli za kilimo kibiashara, hii ikiwa ni pamoja na kuongeza ubora wa mazao badala ya kuuza mazao ambayo hayajaongezwa thamani. Serikali inawajibika kujenga mazingira kwa makundi haya ya wakulima wadogo na wafugaji kuchangamkia fursa hizi badala ya kuelekeza jitihada kubwa katika uwekezaji kutoka nje.

Inawezekana tungefika mbali zaidi kama wawekezaji kutoka nje wangewekeza katika msingi wa ubia na wazalishaji wadogo, kwa maana kuwa wazalishaji wadogo - wakulima na wafugaji - katika vikundi vyao, msingi wao mkubwa ukiwa ni rasilimali ardhi, wanaweza kuingia katika ubia na wawekezaji toka nje kwa namna ambayo wanakuwa na sauti katika maamuzi na hivyo kuwezesha kile tukiitacho win win situation, yaani 'hali ya mafanikio kwa pande zote zinazohusika'.

Hakuna sababu ya Wachina, Wakorea na Wasaudia kuja kulima ilihali tuna makundi ya wakulima wadogo wadogo katika maeneo mbalimbali; ni kiasi cha kuelekeza jitihada katika kuwawezesha wazalishe kibiashara ili kupata ziada kwa ajili ya uhakika wa chakula lakini pia kuuza nje.

Hivi sasa pia kuna wimbi jipya la uwekezaji katika misitu, makampuni ya kigeni yanatwaa ardhi na kupanda miti kisha yanalipwa fedha katika utaratibu wa kupunguza gesi zinazochafua hewa ambao ni mkakati wa kimataifa dhidi ya uchafuzi wa mazingira na hasa tabaka la ozoni. Ni vijiji vingapi vimehamasishwa kutumia maeneo yao kupanda miti ili waweze kuvuna hizo carbon credits? Na je katika maeneo ambayo hili linafanyika ni namna gani suala la ardhi hasa inayofaa kwa mazao ya chakula linaangaliwa? Hii yaweza kuwa fursa lakini pia hatari kwa uhakika wa chakula.

Inawezekana tupo katika kipindi kigumu sana katika historia ya nchi yetu. Maslahi ya kitaifa na maslahi ya wananchi yapo katika majaribu. Je ,tumejipanga vipi kuhakikisha kuwa fursa hizi haziwi msiba kwetu, tukajikuta tukilaumu kama tunavyoendelea kulalamika jinsi tulivyoingizwa mjini katika sekta ya madini. Lengo letu katika michakato yote hii ni nini haswa? Kumkomboa mzalishaji mdogo ama kumwondoa kutoka kwenye rasilimali ardhi?

Huu ni wakati wa kujipanga na haswa kwa wazalishaji wadogo vijijini. Tusidanganyike na ahadi za mdomo. Ni vyema kuingia makubaliano ambayo yatawafaidisha makundi yote. 'Mkombozi wa Mkulima ni Mkulima Mwenyewe' ni kaulimbiu ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) na mkombozi wa mzalishaji mdogo, kwa mantiki hii, kwa maana ya wakulima, wafugaji, waokota matunda, wachimbaji wadogo wa madini na makundi mengineyo ni mzalishaji mdogo mwenyewe.

Shime tusisubiri mjomba wa kuja kutukomboa, hayupo. Ni jukumu letu kujipanga kwani siku za usoni zipo kwa ajili ya wale waliojipanga vinginevyo tutabakia kuwa watu wa kulalamika, huku tukishuhudia wachache miongoni mwetu wakifaidika na rasilimali ambazo kimsingi ni urithi wetu sote.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP