Loading...

Tuesday, July 27, 2010

WARAKA WA WAZI KWA RAIS JAKAYA KIKWETE

Waraka wa Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete

Dk. Barnabas A. Mbogo

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, kwa heshima na taadhima na kwa namna ya pekee kabisa, nakusalimu kiongozi wangu - amani iwe nawe. Nikiwa ni kijana mtanzania nina donge zito moyoni kuhusiana na uongozi wako, hasa unavyojitoa binafsi kusimamia na kuongoza nchi yetu pendwa ya Tanzania. Ni mwendawazimu tu anaweza kuthubutu kusema kuwa hujafanya jambo lolote la maendeleo katika kipindi cha takribani miaka mitano ya uongozi wako mpaka sasa. Umefanya mambo mengi mazuri ya kupongezwa katika nyanja za uchumi, siasa na hata katika ustawi wa jamii. Binafsi ninapenda kukushukuru kwa niaba ya wenzangu wanaokubaliana na namna unavyoongoza nchi yetu.

Mheshimiwa Rais, pamoja na mafanikio mengi mazuri ya kupendeza ambayo nitayachambua katika waraka huu, nitakuwa mnafiki sana nisipojadili kwa kina, marefu na mapana, maeneo ambayo ama umeshindwa binafsi ama baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali unayoiongoza wameshindwa kabisa kutimiza ahadi zao za uongozi bora na hivyo kuharibu kabisa ndoto nzuri yenye matumaini ya “maisha bora kwa kila mtanzania na Tanzania yenye neema inawezekana” hasa kwa kutimiza Kaulimbiu ya “ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya”.

Kusema ukweli, ndoto ya Tanzania yenye neema inawezekana ni ndoto ya ukweli kabisa Mheshimiwa Rais. Kuhusu Kaulimbiu ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya nathubutu kusema neno hili ni hamasa ya kutosha inayoibua moto wa kufanya kazi kwa ari zaidi, nguvu zaidi, juhudi na maarifa zaidi ili Watanzania tujiletee maendeleo yetu wenyewe kwa kasi zaidi. Binafsi naona dhima hii ni mwendelezo wa moja ya kauli za baba wa taifa - hayati Mwalimu J.K. Nyerere aliposema “watu hawawezi kuendelezwa na watu wengine wanatakiwa wajiendeleze wenyewe.”

Mheshimiwa Rais, katika kipindi chako cha uongozi wa takribani miaka mitano sasa tumeshuhudia mambo mengi mazito kuanzia bunge lenye msisimko wa hoja motomoto ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Waziri Mkuu aliondoshwa madarakani kwa hoja kali za wabunge. Pengine kulikuwa na udhaifu katika mjadala mzima wa kashfa ya Richmond, lakini bado jambo hili la kumuondoa Waziri Mkuu lilitokea katika awamu yako ya kwanza ya uongozi na kuweka historia Tanzania.

Tumeshuhudia ukiongoza mapambano dhidi ya rushwa katika ngazi tofauti tofauti, pia tumesikia namna ambavyo Taasisi ya Kuzuia na Kupamana Rushwa (TAKUKURU) ikilalamika kukosa meno ya kutafuna pale inapokutana na mifupa inayohusishwa na rushwa ama ufisadi - hii imekuwa changamoto sio tu kwa Serikali yako, bali kwa jamii nzima ya Watanzania na pengine ni fursa kwetu kutafakari namna ya kuboresha zaidi vyombo mbalimbali vya utendaji na maamuzi nchini mwetu.

Tanzania inatajwa kuwa ni taifa changa kwa maana ya umri wa Jamhuri na maendeleo ya uchumi, siasa na ustawi jamii hivyo Watanzania hatuna budi kuwa na subira kidogo ili tupate maendeleo. Ikiwa ni moja ya nchi za Afrika zilizoathirika na ubaguzi wa Kimagharibi uliodumu kwa zaidi ya miaka mia tano kwa mujibu wa historia, Tanzania pamoja na uchanga wake kama taifa nathubutu kusema ina raslimali za asili za kutosha sana ikiwamo watu makini wenye uwezo wa kubadilisha hali ya uchumi ulivyo sasa na kuwa uchumi wa kupigiwa mfano. Nashangaa namna Serikali yako inavyoweza kusimamia amani na utulivu nchini wakati huo huo inayumba sana kuhakikisha uchumi unakua sambamba na uwepo wa amani.

Mheshimiwa Rais, katika hali ya kushangaza sana na kinyume cha matarajio ya wengi kuwa, kwa kuwa wewe umekuwa ni mwanajeshi kwa kipindi kirefu sana kabla hujawa Rais, wengi wetu tulitarajia, pengine zile amri za kijeshi utazileta huku kwenye uongozi wa kiraia, wapi bwana, hujafanya hivyo, umeachia uhuru wa vyombo vya habari - baadhi ya waandishi wamekusema na kukukejeli wapendavyo, umekuwa mnyekevu kwao kwa vile umeamini katika demokrasia. Kuna kipindi watendaji wako walionyesha makucha ya Serikali na kutoa adhabu za mpito kwa baadhi ya vyombo vya habari vilivyodaiwa kuthubutu kuchafua hali ya amani Tanzania kwa kuchochea chuki na kujenga matabaka yasiyo na maslahi kwa taifa, ni wazi umejitahidi sana kuwa makini kuleta mlinganyo wa mambo muhimu.

Mheshimiwa Rais, donge lililonishika moyoni mpaka maji yanakuwa hayapiti kooni ni namna ambavyo baadhi ya wasaidizi wako wanavyoshindwa kukupa taarifa sahihi na kusababisha ufanye maamuzi yasiyo na maana kabisa kwa ustawi wa taifa letu changa. Nashangaa wanajiamini kitu gani mpaka kumpotosha Amiri Jeshi Mkuu? Ina maana hawajui ukweli wa taarifa wanazokuletea ama wanajua hata kama wakikudanganya hautowaadhibu kwa mujibu wa sheria?

Udhaifu uko wapi?

Napata mashaka sana juu ya mustakabali wa taifa ikiwa utaendelea kupewa taarifa zisizo sahihi nawe ukazifanyia maamuzi ambayo unaamini ni maamuzi makini. Hauyumkini mimi sio mtanzania wa kwanza wala wa mwisho kukuarifu juu ya jambo hili; kwa mujibu wa kanuni za uchumi, raslimali ni “kiduchu-scarce” sana hivyo maamuzi ya kutumia hizi raslimali lazima yawe ni maamuzi makini yanayotokana na utafiti wa kutosha ili tufaidike zaidi na hizi raslimali. Najua inachefua kiasi gani unapopewa taarifa potofu ili ufanye maamuzi - hawa viongozi waandamizi wanaokupa hizi taarifa potofu lengo lao ni lipi hasa? Ama wao sio Watanzania na hivyo hawaoni sababu ya kuendeleza Tanzania kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya? Ama ndio kusema hawataki maisha bora kwa kila mtanzania?

Nimesoma kwenye vyombo vya habari namna ulivyopotoshwa kwenye lile gari la wagonjwa, majuzi tena nimesikia ulivyopotoshwa juu ya kituo hewa cha mawasiliano ulichofungua, haya ni baadhi tu ya matukio uliyopotoshwa, vipi kuhusu mambo mengine unayoarifiwa mkiwa kwenye vikao vya ndani, kwa mwendo huu Tanzania yenye neema inawezekana kweli? Nakupa pole sana Mheshimiwa Rais.

Waraka huu nauandika ilhali machozi yananitoka. Kazi ya kuimarisha uchumi, siasa na ustawi wa jamii ya Tanzania sio yako peke yako Mheshimiwa Rais. Kwa ridhaa yetu tumekupa mamlaka utuongoze, uwe msemaji wetu tukiamini kuwa sisi watendaji tupo nyuma yako tukiunga mkono maazimio mbalimbali ya bunge letu tukufu na tukishirikiana na serikali yetu kujiletea maendeleo yetu wenyewe.

Kinachoniliza ni “genge” la watu wachache waliokuzunguka ambao wako radhi kukata mawasiliano na maridhiano yako na sisi wanyonge -hapa ndipo najiuliza, watu hawa wana lengo gani na Tanzania? Kama wanaweza kukupotosha, watashindwa kuchukua rushwa nzito nzito ili kujinufaisha binafsi? Jitihada kubwa sana ulizofanya za kuunganisha Watanzania na Serikali kujitahidi kutoa huduma kila kona zinaonekana ni kazi bure kwa vile baadhi ya watendaji waandamizi ni wanafiki - hawatekelezi kama unavyovyaagiza- matokeo yake unaonekana eti wewe unapenda sifa kwa maana ya kuwaahidi Watanzania maendeleo, kisha wanakupigia makofi kuonyesha wamefurahishwa na hotuba zako nzuri zisizotekelezeka. Naamini tatizo kubwa linasababishwa na baadhi ya watendaji wako Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani mwaka 2005/06 jamii ya Watanzania ilikuwa na imani kubwa sana kwako. Kadri muda ulivyokuwa unapita jamii hasa ya wasomi wakaanza kupoteza imani kwako, sio kwa vile huwezi kuongoza, la hasha, ni kwa vile baadhi ya watendaji wako walilegea sana na kuonekana kama wametumwa kuchukua rushwa kama sio kuchelewesha utoaji wa huduma bora kwa wakati. Kulipotokea mabadiliko ya Waziri Mkuu kundi kubwa sana la wasomi lilirejesha imani kwako, lakini lilianza kupoteza imani yao kwako kwa vile wasomi wengi hawakuridhishwa na utendaji wa baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali yako.

Nimekuwa mmoja wa watu waliokubali sana kauli yako, nainukuu: “siasa na biashara haviwezi kwenda pamoja" ukiwa na maana kuwa ikiwa mtanzania anataka kuwa mwanasiasa hana budi kuacha biashara. Ukweli wa hili jambo uko wazi sana. Kuyumba kwa imani ya wasomi Watanzania juu ya uongozi wako kunatokana na namna ambavyo Serikali inatoa maelekezo na kisha yenyewe inashindwa kuyatekeleza. Jambo hili linaudhi sana Mheshimiwa Rais, halina tofauti na kupotoshwa.

Mheshimiwa Rais, nimeshikwa na uchungu sana mpaka nashindwa kuandika kila nilichokusudia kuandika, naomba uniruhusu nikuandikie tena mara nyingine kuhusiana na ufanisi wa Serikali yako na mtazamo wa Watanzania kwenye ufanisi wa Serikali yako. Lengo langu sio kukulaumu ama kukushambulia kuwa umeshindwa ama umefanikiwa kutimiza ndoto yako ya Tanzania yenye neema inawezekana, bali ni kujadili nawe maeneo yanayochangia tushindwe kutekeleza ndoto yako ambayo ni yetu Watanzania wote kwa vile imetoka kwa kiongozi wetu tuliyemchagua wenyewe - naamini viongozi tulionao hutoka kwa Mungu ,yatokanayo na uongozi wao ni udhaifu wa kibinadamu ama hekima waliyopokea kutoka kwa Mungu aliyewapa nafasi walizonazo.

Mheshimiwa Rais, baba wa taifa Mwalimu Nyerere alilisitiza sana suala la kukusanya kodi. Sisemi eti Tanzania hatukusanyi kodi, tatizo ni Watanzania wenzetu wenye dhamana ya kukusanya kodi badala ya kuipeleka kwenye mfuko wa Serikali , baadhi yao wanapeleka kwenye mifuko yao binafsi. Naamini kufanya hivi ni kinyume kabisa cha taratibu za kazi lakini ndivyo wanavyofanya. UInashangaza wanavyokuja kukupa taarifa potofu kuhusiana na mapato ya Serikali, wanategemea ndoto yetu ya maisha bora kwa kila mtanzania itatekelezeka? Kwa nini basi wanafanya hivi?

Kwa haraka tu nipitie Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025. Kwa vile hii dira ina kila kitu ambacho Tanzania changa inahitaji nimejikuta naipenda sana dira hii, lakini sioni namna tutakavyotekeleza miongozo ya dira na kufikia malengo tuliyojiwekea kwenye hii dira ya maendeleo ya 2025. Natamani Serikali yako ingewekeza nguvu zaidi kwanza kutoa elimu endelevu na shirikishi kwa Watanzania kuhusu hii dira, na kuainisha mchango wa kila mtanzania kwenye kufikia malengo tuliyojiwekea wenyewe kama nilivyoyasoma kwenye dira.

Nionavyo Serikali inatekeleza sehemu kidogo sana ya malengo yaliyomo kwenye dira, mbaya zaidi jitihada za Watanzania kujiletea maendeleo zinaendana na dira kwa kiasi kidogo sana. Kama tutashikamana kama taifa katika kutekeleza hii dira, ni wazi Serikali yako haitopotoshwa na rushwa itapungua sana kwa vile kila mmoja atawajibika katika eneo fulani, hivyo kulegea kwa eneo lake itakuwa ni tiketi yake kupoteza nafasi yake ya kazi kwa kuzingatia kuwa kila mmoja atapimwa kwa ufanisi wa kazi yake katika kufikia malengo tuliyonayo kwenye dira ya maendeleo 2025.

Mheshimiwa Rais, nashukuru sana kwa kutumia muda wako kusoma waraka huu ambao nimejitahidi kuutumia kutoa donge lililopo moyoni mwangu kwa kadri ninavyoiona nchi yangu Tanzania isivyotendewa haki na watu wake yenyewe.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Barnabas Mbogo
P.O.Box 6243
Mwanza
Tanzania

drbmbogo@gmail.com
00-267-73-265-295

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP