Loading...

Tuesday, August 3, 2010

CHANGAMOTO ZA MASOKO YA MAZAO YA KILIMO KWA WAKULIMA WADOGO - NINI KIFANYIKE?

Mpaka sasa mada zote katika Mkutano Mkuu wa 15 wa MVIWATA zimejikita katika kuhamasisha uzalishaji wa chakula kwa ajili ya biashara na si chakula tu. Hotuba ya ufunguzi ya Waziri Kiongozi, Philemon Luhanjo, kama ilivyosomwa na mwakilishi yake, ilifungua pazia na msisitizo wa uzalishaji mkubwa kwa kuzingatia Mwito wa Kilimo Kwanza. Hata fulana za mkutano walizovaa washiriki zina kaulimbiu hii 'KILIMO NI MASOKO.'

Na mada ya Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi (MUCCoBS), Profesa Faustine K. Bee, imeweka msisitizo katika uimarishaji wa masoko ya kilimo ili wanufaike na fursa za soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Ili hili liwezekane Profesa Bee anasema kuwa inabidi tuweke msisitizo katika: (1) Elimu na uhamasishaji mf. unaoepelekea wakulima na wananchi waelewe uwepo wa fursa hii muhimu ya kiuchumi; (2) Ujasiriamali na ujuzi/umahiri wa masoko - mf. katika kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika soko na wala siyo soko kwa ajili ya bidhaa; (3) Kuboresha upatikanaji wa fedha - mf. kuwa na taasisi mahsusi kwa ajili ya sekta ya kilimo; (4) Uimarishaji na uboreshaji wa taasisi/asasi wakulima - mf. kuhamasisha mikataba ya kilimo; (5) Upatikanaji wa taarifa na kufanya utafiti na masoko -mf'. kuongeza kasi na urahisi wa kuzipata; na (6) Uimarishaji wa miundombinu - mf. vituo vya masoko/minada ya mifugo, usafirishaji na mawasiliano, utunzaji wa bidhaa kwa kutumia maghala, ulinzi na usalama.

Licha ya mada hizi kuwa na mambo mengi ya umaendeleo (developmentalism) zimejikita katika mtazamo wa uliberali mamboleo (neoliberalism)/mfumo wa soko (market economy). Hazijaweza kuonesha undani wa mtazamo/mfumo huu athari zake kwa wakulima wadogo wanaoshauriwa waageuke na kuwa wakulima wakubwa wa kibiashara. Pengine mchana kutakuwa na mitazamo tofauti kidogo kutoka kwenye mada zitakazotolewa na Mwalimu Bashiru Ally na Profesa Issa Shivji.

1 comments:

Anonymous August 9, 2010 at 3:08 AM  

Safi sana! Hivi kuna vijana wanafuatilia hizi habari kweli?

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP