Loading...

Tuesday, August 3, 2010

MASLAHI YA WAKULIMA NA WAZALISHAJI WADOGO KATIKA MFUMO WA KISIASA WA VYAMA VINGI - NA PROFESA ISSA SHIVJI

Kama sehemu ya Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) unaoendelea hivi sasa hapa Morogoro, Profesa Issa Shivji amealikwa kutoa mada. Anaanza kwa kusisitiza kuwa ataongelea uzalishaji tofauti na wazungumzaji waliopita walioongelea soko. Anasisitiza kuwa 'soko ni matokeo - ni mahali ambapo unauza bidhaa. Lakini zile bidhaa lazima zizalishwe kwanza kabla hazijauzwa. Huwezi kuuza bidhaa hewa - japo kuna watu wanauza bidhaa hewa. Mfumo wa kuzalisha bidhaa ndio msingi wa mfumo wa kiuchumi, kijamii na hata kisiasa. Nani anayezalisha? Nani anayefaidika na uzalishaji ule? Nani anayetoa jasho na nani anakula matunda ya jasho hilo? Hayo ni maswali ya msingi na muhimu kabisa hasa katika jumuiya ya wazalishaji, na hasa wazalishaji wadogo - wakulima, wafugaji na wavuja jasho wengine!'

'Nchi yetu bado ni nchi ya vijiji. Sasa tuna vijiji zaidi ya 12,000. Takribani 80% ya watu wetu wanaishi vijijini. Ingawa takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa mchango wa sekta ya kilimo katika uzalishaji wa kitaifa (GDP) ni asilimia 26%. Tulizoea kuona mchango huo ukiwa ni nusu (50%) ila sasa takwimu zinasema zimeshuka mpaka 26%. Mchango wa kilimo ni 26% japo 80% ya watu wetu wanaishi vijijini - hii maana yake nini? Ina maana asilimia 80% ya watu wetu inazalisha pato kwa 26% tu? Hili ni suala la msingi tunaloposwa kujiuliza sababu zake!'

'Tuelewe mfumo wa vyama vingi kwa mtazamo na msimamo wa wazalishaji wadogo. Huwezi kuzungumzia wakulima wadogo kama hawapo wakulima wakubwa - hivyo hivyo huwezi kuzungumzia wakulima maskini kama hakuna wakulima matajiri. Huwezi kuongelea umaskini bila kuuelewa utajiri. Katika jamii hiyo hiyo kuna mgawanyiko. Katika jamii hiyo kutakuwa na mfarakano - hakutakuwa na mtazamo mmoja. Tunasikia hoja mbalimbali kuhusu wakulima - kuwa ni maskini kwa sababu hawafuati kanuni za kilimo cha kisasa na kuwa wavivu. Lakni wakulima sio wategemezi. Wao ndio wazalishaji. Katika jamii wasio wategemezi ndio maskini. Wale walio tegemezi ndio matajiri.'

'Kuna Tabaka la Wavuja Jasho na Wavuna Jasho!'

MADA HII INAENDELEA - YOTE ITAWEKWA MTANDAONI

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP