Loading...

Saturday, September 18, 2010

Akiwa Hoi Aomba Mahakama Dakika 20 Ili Ajibu Mashtaka - Ajali Iliosababisha Kifo Cha Dr Simon Eliezer Temu - YMCA 19 March 2010

----------
Na Mwandishi Maalum, Moshi 17/09/2010

Mshtakiwa Bryan Alphonce Tawete mkazi wa Moshi leo alifikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya, Moshi mjini Mheshimiwa Kasebele ambapo alisomewa mashtaka katika maelezo ya awali tayari kuanza kusikilizwa.

Katika taratibu za mahakama, Bryan akiwa anapitishwa katika taratibu za maswali ya uhakiki wa jumla ya mashtaka matatu, ambapo aliyakana yote alianza kuonekana na wasiwasi mkubwa huku akitetemeka na kutokwa na jasho pindi alipohojiwa iwapo aliwahi kufikishwa kwa polisi wa onyo na mlinzi wa amani na kukiri makosa kwa maandishi , ambapo  pia alizidi kukana, lakini alianza kuomba apewe kiti, na kuanza kuuuma uma maneno huku akiomba apewe muda wa kupumzika na kuwa alikuwa akijiskia vibaya.

Awali akiwakilisha mashtaka hayo matatu pamoja na vielelezo, wakili wa serikali Mheshimiwa Mjalula alisema kuwa mnamo April 2010, mshtakiwa Bryan alikiri makosa yote matatu   katika kituo kikuu cha polisi mjini Moshi na pia kwa mlinzi wa amani, jambo lililomfanya hakimu amuulize mshtakiwa kama ana uhakika na majibu anayoyatoa ya kukana taarifa za polisi. Swali lililompa taabu sana kujibu na kuonekana akiweweseka. Hakimu alimruhusu apumzike kwa dakika 20.

Haikupita muda ilisikika sauti ya ndugu na dada zake Bryan kutoka chumba cha mahakama, kama alivyosema mmoja wa mashuhuda, "ghafla  tukasikia kelele za dada wa Bryan Alphonce Tawete akiita Bryan!!! Jamani Bryan!!! -  Bryan  alikuwa amelegea hoi, ndunguze wakambeba wakamtoa nje ya chumba cha mahakama alionekana akipepesa macho, wakamlaza kwenye upepo".

Wakati haya yakitokea, mjane Mrs Elisia Simon Temu alikuwepo mahakamani pamoja na mwanae Dr. Florence Temu na ndugu na jamaa wa karibu na familia. Mmoja wa watoto wa marehemu alionekana amevaa T-Shirt yenye picha ya Baba yake Mzazi Dr Simon Eliezer Temu. Dr Simon Eliezer Temu alifariki kufuatia kugongwa na gari alilokuwa akiliendesha mshtakiwa Bryan siku ya tarehe 19 Machi 2010, katika barabara ipitayo eneo laYMCA- Moshi. Pia wakili wa kujitegemea  wa familia ya Dr Simon Elizer Temu,  Advocate Jonathan Peter  na vijana wake walikuwa miongoni mwa waliokuwepo mahakamani hapo.

Dr Simon Eliezer Temu (77), akiwa mmoja wa Madaktari 12 wa kwanza wa Tanganyika huru, na mtaalam katika magonjwa ya Malaria na mmoja wa waasisi wa National Institute for Medical Research - NIMR, alifariki dunia tarehe 24-Machi 2010, takriban baada ya siku tano katika hospitali ya KCMC Moshi akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi yaani ICU.

Baada ya muda walionekana ndugu wa familia ya mshtakiwa wakishauriana na kurudi  tena mahakamani baada ya dakika kama 20 hivi, na ndipo walipomuhakikishia Mheshimiwa Hakimu Kasebele kuwa  Bryan yuko tayari kuendelea. Hakimu akauliza tena maswali yote, na mshtakiwa akayakana yote na kusema kuwa hajawahi kuandika maelezo yoyote polisi ya kukiri kosa.

Mnamo Machi 19, 2010, kwenye majira ya saa kumi na moja na nusu jioni, Dr Simon Eliezer Temu, akitokea kwenye matembezi yake ya siku, alikuwa akivuka barabara ipitayo eneo la YMCA Moshi, aligongwa na gari aina ya Suzuki Escudo T220 AYC - yenye nembo ya Chama Cha Waalimu Tanzania – kitendo kilichosababisha daktari huyo kuanguka na kuumia sana sehemu za kichwani, na kupoteza fahamu baada ya muda mfupi. Gari hilo  lililomgonga  lilirudishwa nyuma mara moja na kuonekana likimkwepa mwili wa majeruhi aliekuwa amelala kwenye barabara hiyo ya lami huku damu zikimchuruzika kutoka kichwani. Baada ya muda, Dr Temu alisaidiwa kupelekwa KCMC na raia wema akiwemo Kiongozi wa CCM Moshi Vijini Mh. Kingazi na Dereva wake na pia mtoto wa Katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro.

Hapo awali April 2010, kufuatilia tukio hili la kugonga na kukimbia yaani 'hit and run', na baada ya mazishi ya Dr Temu nyumbani kwake Mamba Komakundi - yaliohudhuriwa na mamia ya watu, Polisi wa Usalama Barabarani na Upelelezi Moshi, chini ya uongozi wa Mkuu wa  Polisi wa mkoa Kilimanjaro Bwana Lucas Lifa Ng'hoboko, waliendesha msako mkali na upelelezi kwa kushirikiana na  familia ya Dr Temu na jamii waliweza kufika nyumbani kwa Bryan ambaye ndiye mshtakiwa, na kumchukuwa kwa mahojiano kituo cha polisi cha mjini Moshi kabla ya kumfikisha mahakamani hapo. Gari aina ya Suzuki Escudo yenye namba za usajili T220 AYC, mali ya Chama Cha Waalimu, lililokuwa limeegeshwa katika hotel maarufu mjini Moshi ijulikanayo kama Keys Hotel, lilichukuliwa na kupelekwa katika kituo cha polisi kwa uchunguzi zaidi.

Marehemu, Daktari Mstaafu (77), ameacha mjane, watoto wanne, na wajukuu 4.

Kesi itasikilizwa tena tarehe 19/10/2010 mjini Moshi.
----------
Picha Kuanzia Juu

1. Gari Linalohusika na ajali
2. Picha ya Marehemu
3. Picha ya Marehemu
4. Picha ya Mjane na Binti wakati wa Mazishi

4 comments:

Subi September 18, 2010 at 1:58 PM  

Asante kaka Chambi kwa Taarifa hii. Nilikuwa namfahamu Dk. kwa kumwona tu mara kwa mara, kumbe alifariki, basi Mungu na ampumzishe pema. Nimesikitishwa sana na kifo chake, alikuwa mtu mwema na mkarimu sana.

Anonymous November 3, 2010 at 6:21 PM  

INASIKITISHA! Hii tetemeka na fainting ilikuwa ya kweli au usanii? kama ni ya kweli inaashiria mtu huyu alihusika hata kama atakana mara zote maana sasa akikumbuka tukio na unyama wa kuondoka bila kutoa msaada wala kuripoti polisi, kisha kujificha na kuibuliwa huko alikojificha...DAMU YA MZEE TEMU INAMLILIA MUNGU! EBU HAKI ITENDEKE TANZANIA IPONE! HUYU NI MMOJA ILA WAKO WENGI HASA WAZEE WALIOTENDEWA HAYA NA HAKUNA MTU WA KUMFUATILIA MHUSIKA...THERE IS A GREAT NEED OF STOPPING SUCH CARELESSNESS INCIDENCES!

Anonymous February 5, 2011 at 4:32 PM  

@ Anonymous - ni kweli kabisa na hizi ndio nguvu kazi zetu, watu wetu wenye mawaidha, watu wetu wenye pilika pilika za kijamii na uchumi ndio wanakuwa njiani katika harakati za kifamilia na uchumi na ndio wanauliwa ovyo ovyo tuu na wahusika hawachukui hatua zozote za maana!

Hadi leo hii kesi kwa mfano maamuzi nasikia ni bado mahakama wanasuasua na polisi wanarudisha nyuma upelelezi - kama mchezo wa kuchelewesha na mtu yoyote anajua mambo ya Tanzania ni wazi rushwa zinatembea tayari. Huu ni UJINGA juu ya UJINGA na ni kweli lazima tupinge haya mambo. Familia nyingi sana zinaathirika.

Anonymous October 20, 2011 at 12:09 PM  

Dana dana za kesi mmh sijui zitaisha lini hapa Tz. Sytems zetu zinahitaji kurekebika san aili haki iweze kutendeka tena kwa muda muafaka.

sasa walau kuna ufuatiliaji ju ya ajali ila kama ni sustainable au nguvu ya soda bado ni kitendawili.

Pasipo haki tutaendelea na umasikini wetu , pamoja na kuzidi kupumbaza watu kiufahamu hata kufikia kuona hamna haja ya kufuatilia haki zao au kwa upande mwingine ulio mbaya kudai haki kwa nguvu ... MUNGU TUPONYE TZ. AMEN.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP