Loading...

Thursday, October 14, 2010

Uhuru Waliopigania Mwalimu Nyerere na Bibi Titi Enzi za Ujana Wao una Maana Gani kwa Vijana?

Si rahisi sana kuuelewa uhuru pasipo kuukosa ama kutokuwa nao. Inawezekana kabisa ikawa vigumu kwetu vijana wa leo kujua maana ya uhuru tulioupata mwaka 1961. Pengine mimi binafsi siwezi kuelewa maana yake mpaka nizielewe simulizi za Bibi yangu. Kwa mujibu wa Bibi yangu, waliishi katika kipindi ambacho mtu aliweza kuchapwa viboko kisa yuko shambani kwake siku ambayo Bwana/Bosi/Mtawala wake hataki kabisa alime.

Lakini lazima tukubali kuwa vijana wa leo tunahitaji uhuru zaidi ya ule tulioupata mwaka 1961. Kama nilivyouliza katika makala yangu katika gazeti la Mwananchi (10/12/2008): Huu ndio uhuru kamili? Je, huo uhuru tuliodai ni kamili mwaka 1961 ulikuwa kamili kweli? Ama ulikuwa 'uhuru wa bendera'? Haya ndio maswali yanayotufanya vijana wengi tusielewe maana ya uhuru ule kwa kuwa bado tunajisikia hatuna uhuru kamili mpaka leo.

Mimi kama kijana wa leo nataka niwe na uhuru wa kwenda popote kama Katiba ya Nchi inavyosema. Lakini, je, naweza kufanya hivyo kama sina ujuzi na uwezo wa kufanikisha hilo? Pia nataka kupata elimu bora inayoweza kunipa maarifa na mbinu za kufanikiwa maishani. Ila, je, hilo linawezekana kama sera ya elimu, ikiwamo ya lugha ya kufundishia, inaninyima fursa hiyo? Hilo litawezekana vipi kama bajeti ya elimu ni duni na fedha zinaliwa!

Kijana wa karne ya 21 nahitaji uhuru wa kufikiri na kuvumbua. Lakini, je, hilo linawezekana kama miundombinu ya sayansi na teknolojia haipo ama ni mibovu? Litawezekana vipi kama vyuo vyetu havina nafasi wala wahadhiri wa kutosha tena wenye uwezo wa kufundisha achilia mbali kufunda? Nitawezaje kushindana na vijana wenzangu walio katika nchi ambazo zinajali uhuru kamili wa watu wake kupata fursa za kujiendeleza?

Pamoja na hayo yote nakubaliana na Mwalimu Nyerere kuwa uhuru ni haki ya msingi. Hivyo hatuwezi kujadili utayari wa mtu kuwa huru au la. Kila mtu anapaswa kuwa huru kwa kuwa ni mwanadamu. Hivyo sisi kama vijana wa leo tunapaswa kutambua kuwa mwaka 1961 ulikuwa ni mwanzo tu wa kudai uhuru ambao tuliporwa na wakoloni. Hivi leo uhuru huo unapokwa na wakoloni mamboleo na vibaraka wao. Tuupiganie uhuru kamili.

Ndio, tupiganie uhuru kamili kwa kuwawajibisha viongozi ambao wameamua kuwa vibaraka wa ukoloni mamboleo. Naam, tufuatilie matumizi ya fedha zetu walipa kodi ili tupate huduma bora za afya, maji, elimu – na miundombinu. Na tuzibe mianya yote ya ufisadi ndani yetu na ya nchi yetu.

Kwetu vijana ambao walau tumepata fursa ya kusoma na kuelimika tukumbuke wosia wa Mwalimu Nyerere kuwa sisi ni kama mtu aliyetumwa na Kijiji chenye kiu akalete maji. Basi na tuyachote hayo maji na kuyarudisha katika Vijiji zaidi ya 10,000 vya nchi yetu ya Tanzania ili vikate kiu hii!

* Sehemu ya Wasilisho Hili Imetoka katika Gazeti La Mwananchi (13 Oktoba 2010)

1 comments:

Temu, A.B.S October 16, 2010 at 3:44 PM  

Kizazi cha Baba wa Taifa, hii ikijumuisha waliopigania "Self Rule", kama tulivyoita "Uhuru", kinatupa mengi ya kujifunza.

Sio tuu vijana wa leo wanataka nini, yaani wapatiwe nini ili kukamilisha lengo la awali kabisa la uhuru, naamini kabisa kuwa swali la msingi ni kuwa vijana wa leo wafanye matendo gani na wawe na mafikara gani ili kujenga jamii yenye uhuru wa kweli.

Uhuru ni aghali mno. Ila ni swala la msingi kabisa kwa maendeleo ya mtu na jumuiya yake. Hivyo basi, ni kijiuliza na kujipangilia wakati ukiweka manufaa yako yenye kuoana na manufaa ya umma. Hivi viwili lazima vioane. These are not mutually exclusive. Kuvuruga umizani huu, ni kuleta matatizo yale yale ya kutokuwa huru, na kutokuwa na maendeleo ya kifikra. Na huu ndio ubatili mbaya zaidi.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP