SIFA KWA MUNGU!

1. Ee Mola ninakujia
Kwako ninasujudia
Sifa nakurudishia
Utukufu enzi pia

2. Ewe uliye Jalia
Mmiliki wa Dunia
Hukumu ni zako pia
Na adhabu ya Jehania

UTANGULIZI

3. Kalamu naishikia
Naandika beti mia
Kwa tungo nazipangia
Zinasifu Tanzania

4. Ni tungo za historia
Ni wapi tulianzia,
Na wapi tumefikia,
Lengo ni kukumbushia

5. Nataka kusimulia
Kwa hizi tungo mia
Huku nawahisabia
Mpaka zitapotimia

6. Tangu walipoingia
Wageni toka Asia
Na wale wa Yuropia
Makabila yalohamia

7. Ishirini na mia,
Makabila ya Tanzania,
Makubwa madogo pia
Hapa nawasimulia

8. Na beti zikitimia
Zikifika hizo mia
Kalamu nitaachia
Lengo nitalifikia.

9. Ujumbe nauanzia
Wa hizi beti mia
Kwa kina nitagusia
Ni wapi tulianzia

...

FUNGUA LINKI HIZI UENDELEE KUUSOMA:


au

MTUNZI:

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Disemba 5, 2011
Email: mwanakijiji@jamiiforums.com
Facebook: "mimi mwanakijiji"

Ω

USULI:

Nilipata wazo la kuandika utenzi huu* kuanzia mwaka jana. Nilikuwa nimekusudia kuandika Utenzi wenye beti 1000 kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania. Lakini katika uvivu wangu na mihangaiko ya dunia nimejikuta nimeishia kwenye hizi beti 100 za utenzi huu wa Tanzania. Maadhimisho ya miaka hamsini ya Uhuru ni maadhimisho siyo ya mipaka ya nchi, siyo ya jina na kwa hakika kabisa siyo maadhimisho ya kupita kwa muda. Ni maadhimisho – naamini- ya utu wetu.

Kwamba, katika miaka hamsini iliyopita tumeweza kufanya kile ambacho hakikuwahi kufanywa kwa miaka 2000 iliyopita katika eneo letu. Yaani, kuwaunganisha watu watu wetu wote, chini ya mipaka ile ile, wakiwa huru na haki sawa. Katika utenzi huu nimeelezea jinsi eneo letu lilivyojulikana kama Azania katika masimulizi ya Wagiriki au kama Zenji kwa Waarabu na wakati mwingine kuhusiana na majina ya maeneo ya Kushi na Nubia katika Biblia. Kama jamii ya watu tumepitia mambo karibu yote ambayo yamepitiwa na jamii nyingine za dunia. Kuanzia maisha ya ujima, utumwa, vita, mapigano, na hatimaye uhuru.

Kumbe basi historia yetu haina tofauti sana na historia ya jamii nyingine za watu ambazo zimesimama katika pande za dunia. Unaposoma utenzi huu ni matumaini yangu utakufanya ujisikie fahari kuwa wewe kama vile mimi ni zao la historia hii. Tumefungamanishwa na historia kiasi kwamba haiwezi kufunguka. Mbele yetu wametutangulia wengi katika historia ambao nao walisimama kutambua utu wao na kuudai mbele ya watawala wa zama zao. Ni hiki ndicho tunachokifurahia kwamba leo tuko huru kuwa watu sawa na wengine – kwa kila hali.

Ni utu wetu ndio ulikuwa msingi wa kupigania uhuru wetu na unatakiwa kuwa ndio kiini cha kushangilia uhuru huo. Ni vipi tumetumia uhuru huo kuinua utu wetu hili ni swali jingine ambalo kizazi chetu kama kizazi kinachokuja kitahiji kujibu. Je, mambo tunayoyafanya na kufanyiana yanalingana na utu huo? Je, tunatendeana kama watu wenye utu katika sera, sharia, mipango, na mambo tunayoyafanya? Utenzi huu basi ni kukumbushia utu wetu.

MMM Disemba 5, 2011