Loading...

Tuesday, February 8, 2011

MTOTO WA BIBI - GRANDMA'S CHILD

Mtoto wa Bibi

Chambi Chachage

“Ukimgusa Mwanamke Umegonga Mwamba” – Wanawake Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini

Bibi yangu mzaa mama anaitwa Mkunde. Bibi yake mzaa mama alijulikana kama Shode. Hivyo huyu Bibi yangu aweza kuitwa Mkunde Binti Orupa Mwana Shode.

Kisa cha maisha ya wanawake hawa ni kiungo muhimu katika historia ya familia yetu. Kwa kiasi kikubwa wamekuwa mwamba ama msingi ambao mama yangu, Demere, amejijenga. Kile walichokifanya wote hawa ni mhimili mkubwa katika maisha yetu.

Orupa Mchikirwa alimlea Mkunde katika kipindi ambacho Wakoloni na Wamishionari walikuwa wameingia katika Milima ya Upare ama Vuasu kama ijulikanavyo katika lugha ya Chasu. Kilikuwa ni kipindi kigumu katika jamii za Kiafrika. Sina hakika kwa nini walimuita Mchikirwa yaani aliyezirwa. Ila ni hakika jina la Orupa lilitokana na yule Orpa aliyekataa kwenda nchi ya ugenini pamoja na mkwewe Naomi kwenye kile Kitabu cha Biblia cha Ruth. Mkulu Orupa hayupo nasi kimwili leo ila bado ni nguzo yetu. Kumbukumbu yake hutusaidia kudumisha udugu.

Sijawahi kujumuika katika kusanyiko lolote la wajukuu, vitukuu , vining’ina au vilembwe vya Mlala Orupa Mchikirwa ambapo hatajwi. Kwa kiasi kikubwa yeye ndiye aliyekuwa mama wa mama yangu, dada na kaka zake pamoja na binamu zao. Pamoja na shida kubwa zilizokuwa zikimkabili bibi huyu mjane bado alihakikisha kuwa walio wake hawalali na njaa. Hata wageni wake alihakikisha wanashiba pia.

Inasemekana wakati hali ya ukame ilipozidi na ugumu wa maisha kumuelemea alifunga ‘mshanga’, yaani kamba, kiunoni ili apunguze makali ya njaa na aweze kulima kwa ‘kikumbu’, yaani, kijembe chake, ili kuwe na chakula nyumbani kwake.

Chakula kichache alichokuwa nacho hakukila bali aliwaachia wanawe na wajukuu zake. Yeye alibaki na mshanga na kikumbu tu mchana kutwa. Wale wajukuu wamekuwa madaktari, marubani, walimu na kadhalika. Mchango wake wanautambua.

Katika udogo wangu nililelewa na Bibi yangu Mkunde. Maisha yake hunifanya nitambue urithi alioachiwa na Orupa Mchikirwa. Ustahimilivu. Upendo. Utu.

Ninapowaangalia dada zangu, Mkunde na Rehema, bado nauona urithi huo. Japo tu kizazi cha nne kutoka kwa Koko Orupa Mwana Shode bado hatujapoteza mizizi yake.

Dunia inapozidi kujikita kwenye unyama nitauenzi urithi huu wa ‘Ujamaa ni Utu’.

5 comments:

annet February 8, 2011 at 11:59 PM  

Hi binamu, nakubaliana na maneno yako, maana juhudi za koko Orupa ndiyo matunda tunayaonayo sasa katika kizazi kilichobaki. Hatuna budi kudumisha Upendo na juhudi kwa kile alichokianzisha koko Orupa. Barikiwa kwa kukumbuka hilo.

Anonymous February 9, 2011 at 8:35 AM  

Chambi kusema kweli leo umenitoa machozi yaani hii picha ya mwisho nimemkumbuka sana koko Orupa. Nashukuru Mungu niliweza kukaa nae na kujifunza mengi kutoka kwake, Koko alikua akilima kuanzia asubuhi hadi jioni hata chakula cha mchana mumpelekee shamba, na alinihadithia alivyosoma kwa shida akitoka shamba na mtoto mgongoni ili arudi apike na awahi shuleni, kwani walikua wakichapwa viboko.

Yaani nina mengi ya kuandika kuhusu huyu bibi ila kikubwa ni kwamba alikua na Upendo, Uvumilivu na usiemsikia akilalamika matatizo yake, akiwa na hela hujui na akiwa hana hujui. kwani kila jumamosi asubuhi alitupa sadaka senti tano wote tukatoe kanisani.

Dorah

Anonymous February 11, 2011 at 10:36 AM  

Kutokana na wasifu wa Mkulu Orupa mwana Shode, kipare angeitwa "KIKOLOLO" yaani mzizi mkuu ambao ndio unalisha familia mema yote kimwili, kiroho, kiakili, kijamii na kiuchumi. KUDOS Mkulu Orupa.

Gureni

SN February 11, 2011 at 1:05 PM  

Dah! Nikiandika yote ulioyaamsha kwenye fikra zangu baada ya kusoma maneno yako, nadhani nitajaza ukurasa...

Kwa sasa hivi nitakushukuru tu kwa hii historia fupi!

Ijumaa njema.

Aaron Mruma July 19, 2012 at 10:32 AM  

Nakubaliana na wewe Chambi,nafikiri tuko mahali hatujui tumefikaje na tutaweleza nini wanaokuja.Mbaya zaidi ule ukoo umeanza kutoweka na baada ya muda mfupi hatutakuwa na kumbukumbu tena ni vyema tupate hiyo historia ilipotekea,

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP