Loading...

Thursday, March 17, 2011

ANA KWA ANA NA MABABU WA LOLIONDO

Ana kwa Ana na Mababu wa Loliondo

Hatimaye nimefika kijijini Samunge huko Loliondo wilayani Ngorongoro. Nimekutana na Ambilikile Mwasapile maarufu kama ‘Babu’. Pia nimeonana na kuzungumza na wazee wengine.

Mababu hawa watano ni sehemu ya wazee nane wanaojulikana kama ‘Wazee wa Mji’ hapo kijijini. Kwa mujibu wa mmoja wao, huchaguliwa na wazee wa rika lao kushikilia uongozi wa kimila wa jamii yao ijulikanayo sasa kama Wasonjo japo kwa asili kabisa wanaitwa Wabatemi.

Kilichotuleta hapo Samunge ni kitu kimoja tu: Kujua asili na nguvu ya dawa inayotolewa na Babu Mchungaji kwa maelfu ya watu wanaozidi kufurika kijijini hapo kutoka katika kila kona ya nchi na hata nchi za mbali. Babu tulipoonana naye kabla yao jibu lake lilikuwa ni fupi tu: “Asili ya dawa ni Mungu mwenyewe, mti ni wa kawaida; ni mti wa kawaida kama miti mingine ila Mungu ameweka Neno lake ndani ya mti hivyo Neno ndilo linaloponya.” Na tena akasisitiza kuwa Mungu akitoa Neno lake ndani ya mti huo basi mti hautakuwa na nguvu hiyo ya uponyaji.

Tulipomdadisi Babu kuhusu matumizi ya zamani ya mti huo alisema kuwa wenyeji walikuwa wanautumia kama supu/mchuzi ila hajui la zaidi. Jibu la ziada ndilo tulilolipata kutoka kwa wazee wa mji na bado tunatafakari jibu lao katika muktadha wa imani za asili za tiba za Kiafrika katika kipindi hichi ambapo vuguvuvugu la uasilia linazidi kupamba moto sehemu mbali mbali.

Mti hii, wazee hawa wa Samunge wanadai, una majina mawili: Mgamryaga na Mbaghayo. Lakini hawajui kwa nini una majina mawili. Ila wanasema unapatikana kwa wingi katika Mlima Mwegaro hapo kijijini. Eneo hilo la mlima ndilo Babu Mchungaji alituonesha kwa kidole alipokuwa anaeleza kuwa ameoneshwa na Mungu kuwa huko ndipo huduma yake itakapohamishiwa kwa ajili ya kutibu watu wengi zaidi ambao wataendelea kuja kutoka mbali.

Kwa mujibu wa wazee hao, dawa hiyo ilikuwa inatumika kama “kinga ya kansa”. “Inapokuwa katika mnyama ni kimeta ila inapokuwa katika mwanadamu ni kansa”, anasisitiza mzee mmoja anapokuwa anajaribu kutuelezea huo ugonjwa ambao walikuwa wanaamini unapatiwa kinga pale wanapokunywa supu iliyochemshwa kutokana na mti huo. Mzee mwingine ananichorea kwenye udongo kabisa jinsi gani hicho kidonda cha ‘kansa’ kinavyojitokeza mwilini mwa mwanadamu.

Walikuwa wanaamini na inaonesha bado wanaaamini kuwa mnyama akifa kwa ugonjwa huo basi nyama yake ikichemshwa pamoja na mizizi ya mti huo na kuliwa ama kunywewa basi wanapata kinga ya kansa. Lakini mlijuaje, nawadadisi? Tulikuwa tunagundua kibahati bahati anajibu mmoja ila kabla hajamaliza mwingine anadakia: ‘Sisi tulirithi kutoka kwa mababu zetu.”

Pia kulikuwa na tiba ya ugonjwa huo, wanasisitiza wazee hao, ambayo ilitokana na kuchoma mti mwingine na kutumia masizi ya moshi wake yanayoganda kwenye dari la nyumba. Wanasisitiza kuwa kinga na tiba hizi bado zinafanya kazi. Lakini inapokuja kwenye suala la dawa ya babu wote wanakiri kuwa ni suala la kiroho/kiimani. Tena wanakiri kuwa na wao wameshainywa na wanaelezea sehemu ambazo imeshawaponya – mmoja mgongo, mwingine mguu na kadhalika.

Wazee wa mji wanne kati ya watano tulioongea nao wana majina ya Kikristo. Tena wote wanakiri kuwa ni waumini wa dhehebu la Kikristo la Kilutheri. Lakini wanasema mila zao hazigongani na imani hiyo ndio maana wao kama wazee wa mji bado wanazisimamia na kuziongoza. Kwa mfano, wanasema Jumapili ya 13 Machi 2001 walifanya tambiko dogo linalojulikana kama Ghorou kwa lugha yao ambapo waliombea huduma ya Babu na masuala mengine ya Kijiji. Mmoja wao anasema mvua iliyonyesha Jumatatu ni matokeo ya tambiko hilo.

Je, walimjulisha babu kuhusu hilo tambiko? La hasha! Wanasisitiza kuwa lilikuwa ni tambiko la wao wazee tu ambalo watu wengine hawakuwa na haja ya kuambiwa kama yalivyo matambiko mengine. Matambiko hayo ni pamoja na lile la kupeleka utumbo wa kondoo na asali kwenye chanzo cha maji katika Mlima Mwegaro kwa ajili ya kuomba kupitia kwa mizimu ya mababu.

Lakini wanatoa angalizo kuwa hapo kwao hakuna “waganga wa kienyeji” pengine katika jitihada ya kusititiza kwamba yanatokea huko sio masuala ya ‘kichawi’ ama ‘kishirikina’. Wanaendelea kusisitiza kuwa ujuzi wa dawa wanao mababu. Hivyo, wagonjwa kijijini wanawaona wazee hao.

Kwao hakuna hili suala la uwili au upacha unaopingana katika kuendeleza imani yao ya kimila na imani yao kikristo. Wanachoona ni kuwa imani hizi hazipingani. Kwa mfano, huduma yao katika chanzo cha maji hayo imejikita katika kuhakikisha wanalinda chanzo hicho cha uhai wa jamii yao. Moja ya taratibu hizi inamkumbusha mwanafunzi wa Biblia kuhusu taratibu za wana wa Israeli walipokuwa wanatoka utumwani katika Nchi ya Misri na kukaa jangwani kwa muda.

Wakiwa huko jangwani walipewa maagizo mbalimbali ya kujitunza na kuitunza jamii ikiwa ni pamoja na kudhibiti hali ya mwanamke aliye katika hedhi isiathiri vitu vinavyotumiwa kwa pamoja katika jamii hizo. Wazee hawa wa Samunge nao wanadai kuwa si ruhusa kwa mwanamke aliye katika siku zake kugusa maji achilia mbali kuoga huko kwenye chanzo hicho.

Tena mwanamke akiwa katika hali hiyo hata akiteleza katika maji hayo basi inabidi alete faini ya kondoo na asali kwa ajili ya tambiko hapo katika chanzo cha maji. Msisitizo wa hili tuliushuhudia pale mzee mmoja alipoondoka na kwenda kuwaonesha wasafiri wenzetu waliokuja kupata dawa ya Babu mahali pa kuoga. Ni suala ambalo mwanaharakati yoyote wa usawa wa kijinsia anaweza kulivalia njuga. Ila kama navyosisitiza, ni muhimu kwanza kujua mantiki yake.

Mjadala huu mfupi na wazee hawa wa mji unaniacha na maswali mengi: Je, kuna uwezekano wowote kuwa hii dawa ina nguvu za kikemikali za tiba ndani yake ndio maana walikuwa wanaitumia kama kinga? Na kama ni kweli, je, suala la kiimani analolisisitiza babu na wazee hawa lina nafasi gani katika hili? Bado naendelea kutafakari hasa ukizingatia kuwa nimeambiwa eti maana ya neno mojawapo kati ya maneno hayo hapo juu ya asili linamaanisha ‘kutafakari.’

Ama kweli wazee hawa wa mji wanatafakari. Kisiasa hii pia ni fursa ya kuendeleza kijiji chao. Ndio maana wanasisitiza tuandike kuhusu umuhimu wa kutengeneza barabara inayokwenda kijijini kwao ili watu wafike kwa urahisi. Pia wanataka makampuni ya simu yalete huduma zao.

Nilichojifunza mpaka dakika hii ni kuwa ni kweli kwa kiasi kikubwa jamii za Kiafrika zinaangalia nini kinafanya kazi au kinaonekana kufanya kazi. Kama dawa ya ‘kiasili’ iko hivyo basi wataitumia. Na kama dawa ya ‘kisasa’ iko hivyo wataitumia. Pia kama dawa ya ‘kiroho’ iko hivyo nayo wataitumua. Ndio maana tulipokuwa tunarudi wasafiri wenzangu walinunua vipande vya magadi pembeni ya Ziwa Natron, wakaniambia navyo ni dawa na kuniuliza: “Kwani hujui?”

1 comments:

Sulle March 17, 2011 at 8:42 PM  

Salam Chambi,
Hawa wazee kwa lugha ya pale wanaitwa wanamijye... Ha ha nilikuwa Samunge na vijiji vya jirani yaani Digo digo kwa wiki mbili mwwaka jana. Hawa wazee bila shaka wamekusimulia mengi.

Ninaversion kidogo ya uhifadhi wao. Nitatafuta mda niifanyie kazi.

Hongera sana pia kupitia Lake Natron maana ndiko huko kwenye dawa serikali inataka kujenga kiwanda cha magadi na ndio sababu pia ya kutaka barabara ya Serengeti kuunganisha na Bandari ya Tanga

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP