Loading...

Monday, March 28, 2011

Vuta Nikuvute: Tutajenga Barabara ya Serengeti?

Sakata la Mpango wa Ujenzi wa Barabara ya Serengeti

Navaya ole Ndaskoi

Karibu mwaka mzima sasa mashirika makubwa ya uhifadhi wa wanyamapori ya ndani na nje ya Tanzania yamekuwa yakipinga kwa kila mbinu mpango wa Serikali ya Tanzania kujenga barabara kuu kuunganisha mikoa ya Arusha na Mara kupitia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Vyombo vya habari vya nje pamoja na tovuti zimekuwa zikitumika kupinga ujenzi huu ambao bila shaka ungeleta huduma kwa wananchi.

Pengine kuna umuhimu wa kueleza japo kwa muhutasari historia ya mgogoro huu.

Takriban miaka ishirini hivi iliyopita Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipendekeza kujenga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Serikali ilipeleka pendekezo lenyewe Benki ya Dunia kutafuta fedha ili ujenzi uanze. Benki ya Dunia ikafanya uchunguzi na kutupilia mbali pendekezo la ujenzi wa barabara yenyewe kwa madai kwamba ungeathiri kwa kiasi kikubwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Hata hivyo, mwaka 2005, Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliingia madarakani. Kikwete alimteua rafiki yake, Edward Lowassa, kuwa Waziri Mkuu. Serikali ikaanza upya mkakati wa ujenzi wa barabara hiyo iliyokosa ufadhili wa Benki ya Dunia hapo mwanzo.

Tarehe 2 Julai 2007 Lucy Owenya, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, alisimama Bungeni na kumuuliza Waziri Mkuu maswali kadhaa kuhusu mpango huu. Owenya aliitaka Serikali ifafanue kuhusu mipango yake ya kujenga (1) mahoteli katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (2) uwanja wa ndege wa kimataifa kilomita 16 tu Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (3) barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na (4) mpango wa kuchimba magadi katika Ziwa Natron.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, kama mwenye ghadhabu vile na akishangiliwa sana na wabunge, alisimama na kusisitiza kwamba Serikali lazima itajenga vyote alivyoulizia Owenya. Lowassa alisema ni lazima barabara ya lami itajengwa kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Engaruka, Loliondo, Hifadhi ya Taifa Serengeti hadi Musoma.

Wakati huo, kama ilivyo sasa, mashirika mengi ya uhifadhi ya wanyamapori yalikuwa Tanzania. Hata hivyo yalitulia kama vile maji kwenye mtungi au kama yananyolewa vile. Punde si punde Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikampata mtetezi. Lakini Lowassa alilazimika kujiuzulu mwezi Februari 2008 wadhifa wa Waziri Mkuu baada ya Kamati Teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ufisadi katika sekta ya umeme.

Mwanzoni mwa mwaka jana mradi huu wenye thamani ya $480 milioni uliibuka tena. Rais Kikwete aliapa mara kadhaa kuwa lazima Serikali itajenga barabara hii kuanzia 2012.

Tarehe na Matukio Muhimu Katika Mjadala Huu

Aprili 2010

Shirika la Kijerumani la Uhifadhi wa Wanyamapori, Frankfurt Zoological Society(FZS), lilichapisha ripoti dhidi ya Barabara kwenye ukurasa wake wa tovuti. Ripoti hii iliandikwa na Prof. Prof. Anthony Sinclair wa Chuo Kikuu cha British Columbia, Kanada, Dk. Markus Borner, Mkugenzi wa FZS-Afrika, Gerald Begurube, aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa ambaye baada ya kuondoka TANAPA aliajiriwa na FZS. Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari "The Serengeti North Road Project" imekuwa ndio msingi wa upinzani dhidi ya barabara hii.

1 Juni 2010

Ukurasa wa Facebook (FB) waanzishwa, baada ya Boyd Norton kurudi kutoka Tanzania aliposikia habari za barabara hii, na sasa karibu ina mashabiki zaidi ya 37,000. Miongoni mwao ni karibu wahafidhina wote wakubwa wa uhifadhi wa wanyamapori kutoka kona zote za dunia. Wanatumia jukwaa hili kikamilifu kuendesha kampeni dhidi ya mpango huu wa Tanzania. Mbali na Boyd Norton na Dave Blanton viongozi wengi wa huu upinzani wameamua kujificha kwa kutotaja majina yao. Ni muhimu kusema kwamba FZS na African Wildlife Foundation (AWF) ndiyo vyanzo vya taarifa yao.

16 Juni 2010

AWF, shirika la uhifadhi wa wanyamapori la Marekani linalojiita kuwa ni la Afrika, lilitoa tamko kuhusu barabara na kusema, kama lile la Ujerumani lilivyosema, Serikali ijenge barabara kupitia kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

31 Julai 2010

Rais Jakaya Kikwete, akihutubia Taifa mwisho wa mwezi, alisema Serikali yake itajenga barabara hii pamoja na kelele za wanamazingira.

16 Septemba 2010

Jarida maarufu, Nature Journal, linalochapiswa nchini Uingereza, lilichapisha habari iliyoandikwa na “wanasayansi” 27 dhidi ya barabara hii. Kwa mujibu wa Nature “wanasayansi” hao ni Andrew P. Dobson, Markus Borner, Anthony R. E. Sinclair, Peter J. Hudson, T. Michael Anderson, Gerald Bigurube, Tim B. B. Davenport, James Deutsch, Sarah M. Durant, Richard D. Estes, Anna B. Estes, John Fryxell, Charles Foley, Michelle E. Gadd, Dan Haydon, Ricardo Holdo, Robert D. Holt, Katherine Homewood, J. Grant C. Hopcraft na Ray Hilborn. Wengine ni George L. K. Jambiya, M. Karen Laurenson, Lota Melamari, Alais ole Morindat, Joseph O. Ogutu, George Schaller na Eric Wolanski; kwa mpangilio huo. Wako wapi waTanzania na waAfrika kwa ujumla? Kama majina ni kielelezo, ukiwaondoa Bigurube, Jambiya, Melamari, Morindat na Ogutu genge zima hili ni Wamarekani na binamu zao toka Ulaya. Ajabu ni kwamba siku chache baadaye wanasayansi 290 walijiunga nao.

30 Septemba 2010

Dk. Jane Goodall aandika kujitetea kutokana na mashambulizi dhidi yake kutoka kwa wahafidhina wa uhifadhi wa wanyamapori, karibu 22,000 wakati huo, kwenye tovuti FB ya Stop the Serengeti Highway (STSH). Itakumbukwa kuwa Taasisi ya Jane Goodall ilimtunukia Rais Kikwete nishani kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori. Wahafidhina walimtaka Goodall ajiweke pembeni ama wamchanganye na Kikwete (Barua kutoka kwa Dk.Jane Goodall kwenda STSH iliyochapishwa kenye FB).

1 Novemba 2010

Baada ya mapambano makali kwenye FB wahafidhina wanasalimu amri na sasa kupendekeza barabara ya Arusha-Babati-Singida-Shinyanga-Mwanza-Musoma. Awali walipendekeza barabara ijengwe kuanzia Karatu-Eyasi-Lamadi-Musoma kupitia ardhi ya Hadza.

Novemba 2010

Serengeti Watch (SW), Shirika Lisilo la Kiserikali, latangaswa kuanzishwa mapema mwezi huu. Inaelekea Dave Blanton na Boyd Norton wanaliendesha watakavyo na wahafidhina wengine wamebaki mashabiki. SW lilisajiliwa chini ya Sheria 501(c)3, maana yake inaweza kuchangisha fedha bila kodi, ya Marekani. Hii nayo ni taasisi nyingine ya Marekani.

10 Disemba 2010

ANAW, taasisi ya kutetea haki za wanyama Kenya, yafungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki. Kwa mujibu wa Saitabao ole Kanchory, Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, anayeiwakilisha ANAW, mteja wake anaiomba mahakama kuipiga marufuku Serikali ya Tanzania kujenga barabara hii sasa na hata milele.

27 Januari 2011

Rais Jakaya Kikwete akutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Ms. Ngozi Ikonjo-Iweala, Davos, Uswiss, na kumhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania haitajenga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kiwango cha lami (Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Januari 28, 2011).

8 Februari 2011

Mabaraza ya Madiwani kutoka wilaya nane za Mikoa ya Arusha na Mara yatoa tamko la pamoja kuunga mkono mpango wa Serikali kujenga barabara kuanzia Mto-wa-Mbu kupitia Loliondo na Mugumu hadi Musoma. Wilaya hizo ni Monduli, Ngorongoro, Serengeti, Tarime, Bunda, Musoma, Rorya na Musoma (Daily News, February 9, 2011).

9 Februari 2011

Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania, John McIntire, pamoja na wasaidizi wake wakutana na Rais Kikwete Ikulu Dar es Salaam na kuahidi kuipa Serikali fedha kwa ajili ya kujenga barabara kupitia Kusini mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti. Rais aliwashukuru na kurudia kusema kuwa wananchi waishio Mashariki na Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti wanahitaji maendeleo (Daily News, February 10, 2011).

14 Februari 2011

Ripoti ya Uhakiki wa Athari za Kimazingira za Ujenzi wa Barabara ya Serengeti (Environmental Impact Assessment - EIA) inachambuliwa mtandaoni na mpinzani wa ujenzi wa barabara hiyo baada ya kuvujishwa kwenye tovuti kadhaa na watu wasiojulikana.

18 Februari 2011

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, ajiunga na wanaopinga barabara kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti. Niebel alisema Ujerumani, kama Benki ya Dunia, itatoa fedha kufadhili ujenzi wa barabara kusini mwa Serengeti. Niebel aimiminia sifa Frankfurt Zoological Society kwa kazi nzuri inayofanya (Frankfurter Rundschau Februari 17, 2011).

11 Machi 2011

Tanzanian Association of Tour Operators (TATO) wanatoa tamko kwenye Daily News linaloitaka Serikali iache mpango huu na inapendekeza ijenge barabara mbadala - tangazo hilo linakuja kutolewa tena kwenye Arusha Times.

19 Machi 2011

Ni siku maalum iliyopangwa na wanauhifadhi wa wanyamapori kote duniani (samahani Ulaya na Amerika ya Kaskazini) kwa ajili ya maandamano ya amani kupinga barabara ndani ya Hifadhi ya Serengeti.

21 Machi 2011

Shirika la Habari la Kijerumani la Deutche Welle (DW) linaripoti kuhusu kuongezeka kwa shinikizo la kuizua Tanzania isijenge Barabara Kuu ya Serengeti. Inaripotiwa kuwa shinikikizo hilo limeongezeka baada ya Serikali ya Ujerumani na Benki ya Dunia kuahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga barabaraba mbadala. Magazeti na blogu mbalimbali zinaitangaza taarifa hiyo pia.

26 Machi 2011

The Citizen inachapisha makala kuhusu uhusiano kati ya barabara ya Serengeti na Loliondo baada ya ziara ya muandishi wa makala hiyo kwenye kijiji cha Samunge ambapo Babu Mchungaji Ambilikile Mwasapile anatoa kile anachodai ni tiba ya kikombe cha dawa kwa maelfu ya watu.

27 Machi 2011

Ripota wa The Observer, Tracy McVeigh, anachapisha makala inayopinga ujenzi huo ambayo inachapishwa pia katika tovuti ya The Guardian la Uingereza na kusambazwa kupitia mitandao mbalimbali duniani. Makala hii inatumia zaidi vyanzo vya wanasayansi waliotajwa hapo juu japo ina makosa kadhaa ya kitaarifa. Mjadala unaendelea mitandaoni.

28 Machi 2011

Mazingira Network - Tanzania (MANET) nao wanatoa tamko kwenye The Citizen dhidi ya pendekezo la kujenga barabaraba kuu ya Serengeti na kupendekeza ijengwe barabara kupitia kusini mwa Serengeti.

Hawawajali Wananchi wa Tanzania

Itakumbukwa kwamba wananchi wengi wanaoishi Mkoa wa Arusha (Mashariki mwa Serengeti) na Mkoa wa Mara (Magharibi mwa Serengeti) waliondolewa kimabavu miaka ya 1950 ili kupisha uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti bila ridhaa yao.


Loliondo ni makao makuu ya Wilaya ya Ngorongoro. Ni karibu kilomita 400 hivi kutoka mjini Arusha. Kwa kuwa hakuna barabara msafiri hupoteza zaidi ya muda unaopotezwa na msafari anayetoka Arusha kwenda Dar es Salaam karibu kilomita 800. Endapo barabara hii ingejengwa bila shaka huduma ingewasogelea wananchi hawa.


Sasa hivi magari zaidi ya 400 yanayobeba watalii kutoka nchi wanakotoka wahafidhina hawa wanaopinga ujenzi wa barabara hupita kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa siku (Daily News [Dar es Salaam] February 24, 2010). Kulinganisha, kuna basi moja to kwa siku linatoka Musoma kwenda Arusha na moja kutoka Arusha kwenda Musoma. Kuna wakati wanamazingira alilazimisha kusimamishwa uzalishaji wa umeme kwa ajili ya vyura wa Kihansi na sasa wanapinga mkakati wa kujenga bwawa la kuzalisha umeme kwenye Bonde la Stiegler katiaka Pori Tengefu la Selous. Madai ya wahafidhina wa uhifadhi wa wanyamapori ni kuwa ujenzi wa barabara kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanyama kama nyumbu na wengine wataangamia. Hoja nyingine inayotumika kuwanyima wananchi waishio pembezoni mwa Serengeti kwamba Serengeti ni Eneo la Urithi la Dunia. Kwamba Tanzania haina kauli ya mwisho kuhusu Serengeti na maeneo mengine ya urithi wa dunia. Wahafidhina wa mazingira wanapendekeza barabara kupita Kusini mwa Hifadhi ya Tafa ya Serengeti (Arusha-Babati-Singida-Shinyanga-Mwanza-Musoma).


Barabara hii kwanza tayari inajengwa na hivyo hawawezi kuiambia Serikali kujenga barabara ambayo inaendelea kujengwa. Pili, barabara hii inapita katika kundi kubwa la pili la wanyamapori wanao hama hama waliobaki katika uso wa dunia hii kule Tarangire-Manyara. Tatu, barabara kupitia Mto-wa-Mbu na Engaruka ni maamuzi ya kisiasa ya Edward Lowassa.


Barabara Mbadala ya Afrika Mashariki


Mbunge Mwanzilishi wa Ngorongoro, Moringe Parkipuny, anapendekeza barabara ya Afrika ya Mashariki. Barabara hii itaanzia Lengijape kwenda Ngaresero na hatimaye Naan Mashariki mwa Loliondo. Kutoka pale itavuka mpaka na kuigia nchini Kenya kuelekea Narok na mbuga za Ngano kule Lemek. Itaendelea hadi Lolgorien na kuvuka tena mpaka pale Sirari na kuendelea kwenda hadi mjini Musoma. Barabara hii inaepuka kukatisha katikati ya wanyama wanao hama hama Tarangire-Manyara na Serengeti-Maasai Mara bila kuathiri haki ya wananchi waishio pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kupata barabara kama wananchi wengine. Vile vile inaifanya Kenya iwajibike kwa kubeba mzigo wake wa wanyamapori badala ya kuiachia Tanzania pekee. Hii pia inaiweka majaribuni roho ya muungano wa Afrika na juhudi zinazoendelea kuunganisha Afrika Mashariki.


Je, Tanzania ni nchi huru yenye haki ya kutumia maliasili zake kwa ajili ya maendeleo ya watu wake? Kati ya wananchi na wanyamapori nani ana haki zaidi? Wote wako sawa? Tanzania ina uhuru bado wa kujiamulia mambo yake yenyewe kama nchi huru? Rais Kikwete ataweza kuhimili mapambano dhidi ya vyombo vya habari vya Magharibi? Kwa nini UNESCO wanaweza kuipelekesha Serikali ya Tanzania kuhusu maendeleo ya wananchi wake lakini UNESCO hiyo hiyo inaziogopa Serikali kama za Ujerumani? Tanzania bado ni nchi huru?

1 comments:

ngorisajr March 28, 2011 at 11:35 PM  

Asante sana ndugu Navaaya Ole Ndaskoi kwa uchambuzi wako wa kina juu ya barabara ya Mto wa mbu - loliondo - musoma na haki za rasilimali za nchi yetu, kwa kweli inashangaza kuona hata watanzania wenzetu labda kwa kudanganywa au kwa kwasababu wamekuwa wakifanya tafiti zinazo wafaididsha wao ili nao waitwe "world scientist"kama SW wanavyo waita au kwa malengo gani! Katika hao watano ambao ni waafrika atleast nawafahamu wanne, Dr Jambia wa chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Jiografia ni mwalinu wangu na ambaye kwa miaka yote mitatu niliyokaa chuo nilimuona kama busy person and sometimes haingii darasani labda kwasababu ya issue nyingi alizo nazo but akingia darasani he used to be a nice teacher.
sinatatizo na kazi yake ila napata pia mshutoko mwalimu wangu wa environmental education anapoargue na kushirikiana na wenzake kama "world scientist" katika journal iliyochapishwa wanapobase kwa upande wa wanyama tu na kusahau kuwa kabala ya serengeti kuitwa hivyo ilikuwa inaitwa sirinket na walio sema hivyo ni binadamu hivyo serengeti na uzuri wake usingekuwepo kama waliotutangulia yaani jamii zilizoishi pale kabla ya Prof wa Ujerumani Gtzimek or kabla ya 1958 waliishi na kutegemeana na viumbe vilivyopo.

Kuhusu barabara ya mto wa mbu - ngaresero - loliondo - musoma ni haki ya watanzania kupata huduma za barabara kwani tangu 1958 jamii zilizo toa serengeti (Waikoma, Kurya, wamasai etc)wanastaili nao kuingia katika muungano wa jamhuri ya tanzania, kama kweli Tanzania ni nchi huru basi either itumie ubabe kama nchi (nyerere alipotangaza vita vya Uganada alisema ........uwezo tunao, sababu tunazo za kuweza kupiga Idi Amini) basi kama Kikwete na serikali yake inaweza na sababu inayo ya kujenga barabara basi wasitishike na wimbi la walanguzi wanaotoka/ wanoandika kwa niaba ya amerika, uingerza na popote pale duniani juu ya barabara hiyo.

Sababu zinazo tolewa juu ya kwanini barabara isijengwe zote zinahusu wanayama. Je kwanini hawa walanguzi wasitoe pia sababu za kibinadamu? Wanafikiri wanawapenda wanyama zaidi yetu amabo tumekuwa tukiishie nao miaka na miaka?

Wanasayansi wametoa sababu kwani wasingewauliza wananchi wa loliondo, Ikoma, Mara/Musoma kama wanataka Barabara?

Nafikiri Tanzania ni nchi huru, basi kama ni huru na imeona tusitimize miaka 50 ya uhuru bila wananchi tuliowanyanyasa (serikali ikishirikiana na deep ecologist i.e frunkfurt zoological society etc) bila kuwa na mawasiliano na wengine then itumie katiba na mamlaka kama nchi kujenga barabara hiyo.

Wasiwasi wangu ni kuwa serikali yetu inaweza kurudisha kucha zake kwasababu ni ombaomba hivyo kuogopa vitisho vya walanguzi kuwa watakata hundi ya misaada.

Sioni haja ya kuwa na nguo nzuri kwenye begi bila kuvyaa, sasa ulinunua au umetengeneza ya nini?

We need the road
Valentin Olyang'iri

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP