Loading...

Tuesday, April 5, 2011

Tuchimbe au Tuokote tu Magadi Ziwani Natron?

Katika safari yangu ya Loliondo kwa Babu nilibahatika kupata kipande kikubwa cha magadi. Kipande hicho kilikuwa kinauzwa kwa Shilingi 500 kando kando ya Ziwa Natron na wenyeji wa maeneo hayo. Katika basi letu watu wengi tu walinunua vipande hivyo kwa ajili ya dawa na matumizi mengine.

Lakini miaka michache iliyopita nilihudhuria mjadala mkali katika Ukumbi wa Karimjee kuhusu mpango wa kujenga kiwanda cha kuchimba magadi hayo. Wenyeji wa maeneo hayo ambao inasemekana walifadhiliwa na wapigania haki za wanyama na wanamazingira waliongea kwa uchungu mkubwa kuwa kiwanda hicho kitaharibu mazalia ya ndege wazuri wa flamingo pamoja na kuathiri upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

Hapo Karimjee alikuwepo pia mwanaharakati maarufu Rugemeleza Nshala aliyeichambua ripoti ya athari za mazingira na kijamii - Environmental and Social Impact Assessment (ESIA) - iliyowasilishwa hapo kwa hisia kali ya kizalendo. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ilibidi likubali hoja hizo za wapinzani wa mradi huo japo wawakilishi wa wawekezaji nao waliongea kwa uchungu kuhusu jinsi ambavyo Tanzania inapata shida kuagiza magadi nje ya nchi ilhali ina magadi mengi sana hapo ziwani Natron. Ni dhahiri tuna magadi tele na watu wanajiokotea tu hapo ziwani kama nilivyoshuhudia nikitokea Kijijini Samunge kwa Babu wa Loliondo. Na ni kweli magadi yanatumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwenye viwanda vya kemikali na kadhalika. Ndio maana watabiri wa mambo tulijua tu kuwa baada ya muda Serikali itarudi tena na ajenda ya kujaribu tena kujenga kiwanda hicho hapo katika mazalia makuu ya flamingo wa kaskazini mwa Afrika. Sasa zaidi ya miaka 3 baada ya mjadala mkali uliofanyika Karimjee, Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa akitoa agizo tata kuwa ujenzi wa kiwanda hicho uanze haraka wakati wa ziara yake katika Wizara husika. Tena tamko hilo limetolewa wakati kuna mjadala mkali kuhusu mpango tete wa Serikali yake wa kujenga barabara kuu ya Serengeti ambayo itapita hilo eneo.

Je, ni lazima tuyachimbe magadi hayo kiwekezaji? Au tuwaachie tu wenyeji waendelee kufaidika nayo angalau kidogo kwa kuyauza kwa shilingi 500 kwa wasafiri wanaopita njia hiyo bila kuathiri vyanzo vya maji na mazalia ya flamingo? Na, je, wanyama wa Serengeti na ndege wa Natron ni kisingizio tosha cha kuwanyima wakazi wa Mto wa Mbu, Engaruka, Ngarasero, Ol Doinyo Lengai na maeneo mengine barabara ya lami walau inayofika Loliondo?

1 comments:

Anonymous April 5, 2011 at 12:56 PM  

wanyama wa Serengeti na ndege wa Natron ni kisingizio tosha cha kuwanyima wakazi wa Mto wa Mbu, Engaruka, Ngarasero, Ol Doinyo Lengai na maeneo mengine barabara ya lami walau inayofika Loliondo?

Kinachotakiwa ni kuunganisha Mugumu na Musoma kwa lami na Loliondo iunganishwe na Arusha.

Ni muhimu vilevile kuangalia which area we are earning more kwa sasa na kulipa uzito unaostahili.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP