Loading...

Monday, May 23, 2011

NIPITIE NIKUPITIE BARABARANI DARISALAMA!

NIPITIE
Na Jacqueline Mgumia

Ndugu zangu,

Leo asubuhi, katika barabara ya Ali Hassani Mwinyi nikitokea Mwenge kwenda Mjini, kama kawaida watu walikuwa wengi barabarani wakisubiri mabasi kuelekea katika mihangaiko yao ya siku. Wengi wao wakiangalia muda na kusogelea mabasi kila walipoyaona. Mengi yalipita bila kusimama maana yalikuwa yamejaa, na yale yaliyosimama abiria walijaribu kujichomeka hivyo hivyo ili mradi wapate mahali pa kupenyeza mguu.

Lakini katika magari madogo zaidi ya ishirini niliyoweza kutayatazama, likiwemo la kwangu, ndani ya gari hakukuwa na watu zaidi ya watatu, na hivyo kuacha viti viwili hadi vinne wazi ambavyo vingeweza kubeba baadhi ya watu vituoni.

Nikabaki najiuliza, kwa nini hatutatui tatizo la usafiri Dar es Salaam wakati magari yapo lukuki? Sio swali geni lakini hatujalipatia ufumbuzi. Labda niulize tena, kwani kuna ugumu gani magari madogo kubeba watu walioko vituoni iwapo wote wanaelekea sehemu moja?

Hofu zilizopo juu ya suala hili ni bayana na zinaeleweka, “aha dunia hii haiaminiki bwana!” Kwa wale wanaokwenda na muda, wanaweza kusema ni “kazi ya ziada!” Kwa misingi ya kibepari, ‘kubebanabebana ndio maana hatuendelei Tanzania!’ Wale wanaokumbuka historia ama kuona wazo hili ni ndoto za Abunuwasi, wanasema “hadithi za ujamaa hizo!” Huku wengine wakikumbusha mabasi ya UDA na ndoto ya “mabasi ya ghorofa mbili” na "barabara za angani" – kwa namna moja au nyingine wanasema “kazi ya serikali hiyo!” SAWA.

Nafsi yangu katu haishangazwi na majibu haya, wala sina nia ya kutoa ushawishi ama kuchanganua kiini cha mitazamo hii. Yawezekana kabisa ndio sehemu ya tatizo – lakini sitozungumzia hilo leo.

Nia yangu haswa ni kutoa mhangaiko wa moyo wangu na kukiri kuchoshwa kuwaona watu wakigombania mabasi asubuhi, huku Serikali na sisi wananchi tukiendelea kuzoea tatizo hili.

Labda, pia nimechoshwa kuulizwa maswali na mwanangu nimpelekapo shule asubuhi kushindwa kuelewa kwa nini watu wazima wanaoenda kazini kama wazazi wake hawana magari na kwa nini hatuwapandishi kwenye gari letu – wakati kila siku anakumbushwa “kushare” na wenzake vitu vyake. Na leo wakati tunapita Makumbusho kaniambia, “mama mbona yule mzee mwenye shati la bluu simuoni!” Kabla sijajibu, akajijibu mwenyewe kwa swali “atakuwa amepata basi leo?”

Wazo langu:

Hakika Serikali ina wajibu wake na tutaendelea kuisemesha, tena kusema nayo sana tu. Ila na sisi pia, kama wananchi waungwana, tunaweza kutafuta ufumbuzi kwa nafasi zetu. Pendekezo langu tuanzishe utaratibu wa kusafirishana, tuuite “NIPITIE”. Tukimaanisha wale watu wenye magari wawe wanachukua watu wasio na magari kwenye vituo vinavyotambulika kulingana na mizunguko yao. Ili kufanikisha hilo, napendeka utaratibu ufuato:

1. Kwanza, wenyeviti wa mitaa waandikishe watu wote wanaohitaji usafiri, kuanzia kituo wanachoanzia kwenda kituo wanachoishia. Ili kujiandikisha mwananchi huyo lazima awe mkazi wa eneo hilo, atoe kithibitisho chake cha kazi/shughuli na barua ya kumhakikisha.

2. Pili, wenye magari na nia ya kutoa msaada wa usafiri, watoe ratiba ya mzunguko wao wa asubuhi, nikimaanisha – kituo wanachoanzia na kuishia – ama ambapo wangependa kuchukua watu na kuwashusha watu, na idadi yao. Pia atoe muda wa kupita njia hiyo.

3. Tatu, wanaopewa msaada wa gari watoe elfu 20,000 kwa mwezi – ambayo inaweza kulipwa 5,000 kwa wiki ili kukidhi mahitaji ya usimamizi wa shughuli hiyo, vilevile kutoa ajira kwa wasimamizi wa shughuli hiyo.

4. Nne, kila eneo liajiri mtu/watu watakoahamasisha/kusimamia na kufikiria ni jinsi gani utaratibu huo ufanyike kwa kuzingatia usalama wa wenye magari, abiria, - na kuona jinsi gani Serikali na jamii itakuwa sehemu ya mpango huu ili uendeshwe kwa amani.

Ama shughuli hii inaweza kuanzishwa na wenye magari ama wanaohitaji usafiri na wajiwekee utaratibu wao wenyewe!

Nyie wenzangu mwasemaje?

1 comments:

Anonymous June 1, 2011 at 11:30 AM  

wazo zuri ila linachangamoto zake tena nyingi
1. litaongeza tax bub mtaani kwani watu watatumia hiinjia kujinufaisha wenyewe
2.uporaji wamagari utaongezeka sijui kama ulizi utaweza kuapo wakutosha kwani hata sasa hivi ma Tax zinapata tabu sana
3.itabidi kufanyiwa marekebisho sheria ya usafirishaji abiria kwani kitendo cha wao kulipi gariyako itakua imeshakua kama tax na unatakiwa ulipe codi na sheria hiukuruhusukulipa kodi yatax kama huna plet no nyeupe
4.watu wengi tunakua hatuna parmanent address so nivigumu kwa wenyekiti wa vitongoji kuratibu kwasasa labda baada yakupata vitambulisho
5.nafikiri unajua kazini wengine wana ingia mapema na kuchelewa kutoka je kama mimi mwenye gari nimechelewa inakuaje wakati watuwalishalipa helayao? naje kama mtu akiugua gafla na akashindwa kutoka asubuhi siitakua tabu?
6.kwakweli nizuri lakini kwautamaduni wetuwatazania itachukua mudasana kueleweka

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP