Loading...

Tuesday, May 17, 2011

Waraka wa Wazi kuhusu Saratani ya Tezi Dume

SARATANI YA TEZI DUME
(PROSTATE CANCER)

WARAKA WA WAZI KWA
MKUTANO MKUU WA MWAKA WA 27
JUMUIYA YA TAWALA ZA MITAA (ALAT)
KUNDUCHI BEACH HOTEL - DAR ES SALAAM
14 – 16, MAY, 2011

Balozi Mstaafu George Maige Nhigula & Mch. Canon Dkt. Emmanuel J. Kandusi

1.0 Utangulizi:

Sisi katika picha ni waathirika, wahanga, manusura wa saratani ya tezi dume (prostate cancer). Kwa waraka huu tunapenda kuwahabarisha juu ya gonjwa saratani. Gonjwa hili kwa sasa ni gonjwa tishio kwa maisha ya watu wengi duniani. Katika nchi zinazoendelea na hususani Afrika chini ya jangwa la Sahara Tanzania ikiwa miongoni hali ni mbaya sana. Mwaka 2010 takwimu duniani zinaonyesha kuwa malaria iliua watu laki 5, kifua kikuu 2.1 milioni, ukimwi 1.8 milioni na saratani 9.9 milioni. Asilimia 75 ya hao 9.9 milioni ambao ni 7.4 milioni walifariki toka nchi zinazoendelea.Waraka huu unawahabarisha umuhimu wa kuliangalia gonjwa la saratani na hasa saratani ya tezi dume ambao sisi ni wahanga. Tunawaomba katika mipango yenu ya afya katika manisipaa na halmashauri zenu, muliangalie na kuliwekea uzito suala la kutoa elimu juu ya saratani na pia kuwa na mipango mahsusi ya kuboresha tiba kama mnavyofanya kwa magonjwa ya malaria, kifua kikuu na ukimwi. Katika hotuba ya kuahirisha bunge la Jamhuri ya Muungano, Mkutano wa Tatu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo K. P. Pinda (Mb) aliongelea kwa msisitizo juu ya saratani na hasa saratani ya tezi dume (prostate cancer) na magonjwa mengine sugu. Ninyi mnaweza kuendeleza mkazo huu huko mtokako mkiamua. Sisi tumelipata joto la jiwe la saratani ya tezi dume. Tunajua madhara ya saratani. Tusingependa wanaume wengine wapate mateso kama tunayoyapata kwa kuchelewa kugundulika gonjwa mapema. Hii ni sababu tosha iliyotusukuma kuanzisha Tanzania 50 Plus Campaign inayotoa elimu, utetezi na msaada wa saratani ya tezi dume kwa jamii nzima. Wachina wana methali isemayo, ‘Ukitaka kujua unakoelekea, muulize anayerudi’. Sisi tumerudi na tunakuhabarisha.
2.0 Je saratani ni gonjwa gani?
Neno saratani ni jina la gonjwa ambao hutokea wakati chembe chembe za uhai katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu na mfumo wa mwili - zinaasi na kutengeneza vivimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida chembe chembe za uhai mwilini huwa zinajigawa, zinapevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini chembe chembe za uhai za saratani hazifuati mfumo huo. Badala ya kufa, zenyewe zinaishi muda mrefu kuliko chembe chembe za uhai za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza chembe chembe za uhai asi zingine na kutengeneza vivimbe vidogo vidogo - saratani.

3.0 Saratani ya tezi dume ni gonjwa gani?
Tezi dume linapatikana katika mwili wa kiumbe mamalia dume tu (angalia mchoro – normal prostate). Chembe chembe za uhai katika tezi dume zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili - zinaasi na kutengeneza vivimbe vidogo vidogo, hapo mtu anakuwa ameathirika na saratani ya tezi dume. Zipo aina nyingi za saratani. Zipo zinazowapata watoto tu, vijana, wanawake na wanaume. Saratani ya tezi dume huwapata wanaume tu na hasa wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Tokana na tafiti mbali mbali, saratani hii imethibitika kushika nafasi ya pili, ukiacha saratani ya mapafu kwa vifo vya wanaume wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea. Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS:2010) na cha Afrika Kusini (CANSA) vimebaini kuwa,“mwanaume mmoja kati ya sita atapata saratani ya tezi dume katika uhai wake”. Na kama wanaume mia moja watakutwa na saratani ya tezi dume. “Saratani hii haina mipaka ya kitabaka” asema Askofu Mkuu Desmond Tutu. Askofu Mkuu Tutu, sisi binafsi na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela ni baadhi ya waathirika wa gonjwa hili ambao bila ya kujinyanyapaa na wala hofu ya kunyanyapaliwa, tumevunja ukimya na kuwa wawazi katika jamii. Pamoja na yote hayo, ifahamike bayana, saratani ya tezi dume ikigundulika mapema inatibika kwa urahisi zaidi.

4.0 Hali hatarishi:
Kuna hali hatarishi nyingi zinazochangia mwanamume kupata saratani ya tezi dume. Zifuatazo ni baadhi tu:-

Umri: Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume inaongezeka sana hasa ukifikia umri wa takribani miaka 50 na kuendelea; Nasaba: Kama katika ukoo kuna historia ya ugonjwa wa saratani ya tezi dume suala na nasaba linachangia kumweka mwanamume kuwa hatarini kuathirika na saratani ya tezi dume kwa misingi ya nasaba (genetic); Lishe: wanaume wanaopenda kula nyama (red meat) yenye mafuta mengi na aina ya maziwa yenye mafuta mengi (high-fat diet) wako katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume; Mazoezi: Wanaume wasiopenda kufanya mazoezi; Unene (obesity). Upungufu: Virutubisho E.

5.0 Dalili za saratani ya tezi dume:
Swali linakuja: Jee mwanamume ataziona dalili zipi zinazoashiria saratani ya tezi dume? Zipo dalili nyingi na hapa nazitaja baadhi tu:

Udhaifu katika kujisaidia haja ndogo na unapotoka unakatizakatiza; Kushindwa kukojoa na kushindwa kuanza pata haja ndogo; Unapohisi haja ndogo unapata shida kuzuia haja ndogo isijitokee yenyewe; Hisia ya kutaka kupata haja ndogo kila wakati hasa nyakati za usiku; hata kukojoa kitandani; Mkojo kujitokea wenyewe; Maumivu au kuhisi mwasho wakati wa haja ndogo; Mbabaa kusimama kwa shida; Maumivu wakati unapotoa manii wakati wa kujamiana; Damu damu katika mkojo na katika manii; Maumivu viungoni – kiunoni, miguu, mgongo nk. Kukosa hamu ya kula na kupungua uzito/kukonda.

Pamoja na kuorodhesha dalili hizo napenda msomaji ujue kwamba mwanaume anapoanza kuziona na kuzihisi kati ya dalili hizo, basi ajue chembe chembe za uhai asi katika tezi dume lake zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea.

6.0 Mwito kufanyiwa uchunguzi wa tezi dume:
Kwa kuzipitia dalili hizi, imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi huwa na soni kwenda kumwona daktari kwa uchunguzi. Wengi huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina – “kuna mkono wa mtu, nimelogwa”. Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuliita gonjwa la mabasha na wengine kuurahisisha kama ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni haki yake kuugua mtu mwenye umri wa utu uzima. Mambo kama hayo huleteleza wazee kujinyanyapaa na kujikuta wengine wakijitibia chochoroni au kwa waganga wababaishaji mpaka pale wanapokuwa hoi bin taabani, mambo yamekuwa mabaya ndipo wanapopelekwa hospitalini. Hapa tunatoa wito kwa wazee kuweka kipaumbele kuwa na tabia ya kufanyiwa uchunguzi wa afya kwa ujumla na ujumuishe uchunguzi wa tezi dume angalau mara moja kwa mwaka.

Kuna vipimo viwili ambavyo daktari anaweza kukupima mara moja ofisini kwake: Vipimo hivyo ni “Digital Rectal Exam (DRE)” na cha pili ni “Prostate Specific Antigen (PSA)”. Baada ya vipimo hivyo kama vitaashiria saratani ya tezi dume basi daktari anaweza kuamuru vipimo vingine vya uhakiki kama transrectal ultrasound au na prostatic needle biopsy. Kuwahi kugundua saratani mapema, kabla ya dalili, ni faida kubwa kwa mwaathirika. Maana saratani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.

7.0 Saratani na Matibabu:
Pamoja na yote hayo, katika zama hizi, matibabu ya saratani ya tezi dume yanapatikana. Ukigunduliwa una saratani hiyo unashauriwa ushauriane na daktari wako kuamua aina ya tiba itakayokufaa. Kuna tiba za uangalizi (active surveillance), upasuaji (surgery), mionzi (radiotherapy) vichocheo (hormone therapy) na kemikali (chemotherapy).

8.0 Hitimisho: Baada ya maelezo hayo tunapenda kutoa wito:
Mtakaporudi huko mtokako, lichukulieni suala la saratani kuwa ni suala mtambuka, endelezeni somo la saratani na hususani saratani ya tezi dume. Anzieni katika mabaraza yenu ya madiwani hadi kwa wananchi;

Washaurini wanaume wote wenye umri takribani miaka 50 na kuendelea, wajenge tabia ya kumwona daktari angalau mara moja kwa mwaka kwa uchunguzi wa afya ukijumuisha uchunguzi wa tezi dume;

Pia tunatoa wito kwa madaktari wenu wazingatie, wanapopata wagonjwa wanaume wenye umri wa takribani miaka 50 na kuendelea wawashauri pamoja na matibabu mengine, wafanyiwe uchunguzi wa tezi dume.

UKWELI KUHUSU SARATANI:
Saratani zote na hususani saratani ya tezi dume ikigundulika mapema ni rahisi kutibika.

Kwa mawasiliano zaidi: Mratibu, Tanzania 50 Plus Campaign, P. O. Box 1854 Dar es Salaam
au barua pepe info@tanzania50plus.org
Simu: 0754 402033.

Kuchangia kampeni :
Weka katika tawi lolote la CRDB. Jina la akaunti : Centre for Human Rights Promotion – CHRP;
Namba ya akaunti: 01 J 1027311100

M-Pesa: 0754 402033

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP