Loading...

Thursday, June 2, 2011

Kujivua Gamba Katika Falsafa Ya Kiafrika

KUJIVUA GAMBA: MTAZAMO KIFALSAFA YA KIAFRIKA?

Na Jason Ishengoma

Malumbano yanayoendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kati ya vikundi vya chama hicho yanatia kinyaa. Yote hayo yanatokana na dhana ambayo haikufanyiwa uchambuzi kifalsafa kabla ya kuitangaza na kuisambaza nchi nzima. Dhana ya kujivua gamba ilitolewa bila kuangalia alama (symbol) iliyotumika kama inaashiria kiashiriwa kinacholingana na lile lililotakiwa kufanywa. Gamba lililoashiriwa ni lile la nyoka. Je, ishara ya nyoka inaweza kueleza kwa makini na ufasaha kile ambacho CCM kama chama wanatakiwa, na siyo wanataka, wafanye?

Kwa muda nimekuwa nikifuatilia mazungumzo ya wana wa nchi hii kuhusu dhana iliyotangazwa na Mwenyekiti wa CCM ya kujivua gamba. Kinachonifurahisha ni kuona na kusikia kwamba Watanzania wa tabaka mbalimbali wanaweza kudaka, kuchambua, kuchangia na kulieleza jambo ambalo linasemwa na wakubwa ambao wanatakiwa kuwa viongozi wao. Kwa mwezi wa Mei nimepata kusafiri sehemu tatu tofauti kabisa za nchi yetu.

Nimejikuta niko Rukunyu kandokando ya ziwa Victoria kwenye pembe ya mpaka kati ya Tanzania na Uganda. Nikiwa kwenye kilabu nikishirikishana mawazo na walala hoi ambao kinywaji na kiburudisho chao baada ya suluba ya siku nzima ni gongo ambayo wenyeji wanaiita konyagi, watu wakaanza mjadala kuhusu dhana ya chama tawala ya kujivua gamba. Wengine wakaiunga mkono na wengine wakaibeza. Siwezi kusema ni kundi lipi lilishinda bali nikapata somo kwamba wana wa nchi hii hawako mbali na wanayosema viongozi ambao wamekuwa watawala wao.

Wiki mbili baadae nikapata nafasi ya kutembelea kijiji cha Chilungutwa wilaya ya Masasi kusini kabisa mwa Tanzania. Kule nako nikakutana na wenyeji wakulima wa kawaida nao wanajadili mambo ya siasa ya nchi yetu. Nao pia waligusia dhana ya kujivua gamba wakiifafanua na kuichangia moto. Wote katika utofauti na umbali kijiografia wao; walieleza dhana ya kujivua gamba kwa kutumia kiashiria cha nyoka kama inavyoakisia dhana yenyewe. Walifananisha kujivua gamba na nyoka mwenyewe ambaye ni kiumbe hai na ambaye kama kiumbe ana maumbile yaliyoko ndani mwake na ambayo hayahitaji utashi wa kitu kingine ili yatokee.

Mwezi huo huo wa Mei nikapata nafasi ya kutembelea Unguja. Kule nikazungumza na wananchi juu ya mambo mbalimbali likiwemo ya kisiasa. Waunguja wa Zanzibar hawakugusa sana dhana ya kujivua gamba; wao waliguswa sana na serikali ya umoja wa kitaifa iliyozaa serikali ya maridhiano.

Katika mazungumzo na ndugu zangu wa Zanzibar nilipata swali moja kuhusu siasa za kiafrika: hivi kweli Waafrika tuna mtazamo kisiasa wa ushindani ambao unajenga msingi wa vyama vingi vya siasa au tuna mtazamo kisiasa wenye msingi wa maelewano? Tofauti kati ya dhana hizi mbili ni kwamba, dhana ya ushindani inahitaji mwingine abaki na utofauti wake, ili kila mmoja katika utofauti wake aweze kuonyesha kwamba yeye ni zaidi ya mwingine katika kile wanachokishindania. Hii ni dhana ambayo inataka kila mtu abaki katika kutokubaliana ila wote wakubali kutokubaliana. Wanafanya ushawishi ili wananchi walio raia wachague kati ya mmoja wao.

Baadhi ya Wazanzibar wa vyama vidogo vya siasa, kwa kutilia msingi wa maridhiano na siyo kushindana, wanaona kama wao wameonewa kwa vile, pamoja na udogo wao bado walitakiwa wawemo katika serikali ya maridhiano. Maana yake ni kwamba, serikali inapaswa kuwawakilisha wote wadogo kwa wakubwa. Iwawakilishe vipi hilo siyo swali kwa wenye dhana hiyo, bali wanaona na kutaka wote katika uwote wao wawakilishwe.

Kilichonisukuma kuandika makala hii siyo kujadili yale waliyozungumza wale niliokutana nao kwa kipindi kidogo cha mwezi Mei; ila somo nililolipata kwenye mazungumzo na majadiliano yao.
La kwanza na kubwa zaidi nimejifunza kwamba Kiswahili kimeifanya nchi yetu iwe moja zaidi ya tunavyofikiria. Kwa kuona watu wa sehemu tofauti kabisa na sehemu zenye umbali mkubwa kiasi hicho wanaguswa na kuzungumzia jambo moja, ilinifundisha jambo kubwa nalo ni umoja wa kitaifa; ingawa kuna “walevi” wachache; kwa kutumia msemo wa mwanazuoni wa kitanzania Euphrase Kezilahabi na mtunzi wa riwaya ya Gamba la Nyoka; wanaotaka kuuharibu na kuuvunja pamoja na kwamba tunu hii inatunzwa na Kiswahili.

Katika mojawapo ya uchangiaji, wachangiaji walitumia, kufafanua na kudurusu dhana ile ambayo inatokana na maumbile ya kiumbe hai anayeitwa nyoka. Kwa maumbile yake, nyoka anabadili au kujivua gamba lake kadri anavyoongezeka umbile lake. Gamba ambalo ni sehemu ya nje ya nyoka, pamoja na kufanya kazi ya kumlinda nyoka dhidi ya baridi au joto, humpa uonekano wake.

Alama ya nyoka iliyotumiwa kutoa na kuwakilisha kile viongozi wa CCM walichotaka kifanyike imenikumbusha dhana-kifalsafa-kiafrika, hasa ya wale wanaofuata mafundisho ya Placide Temple, kwamba Mwafrika anaamini katika uwepo wa nguvu hai (Force Vitale) katika kila kitu kiwacho. Nguvu hai hiyo ndiyo inakipa kitu ukiwe wake; yaani ndiyo inafanya kitu kiwe kama kilivyo. Nguvu hai hiyo inaweza kuongezeka au kupungua kwa jinsi inavyojioanisha na nguvu hai iliyo juu zaidi. Kwa maneno mengine, kitu kinakuwepo kwa kuwa na nguvu iliyomo ndani mwake na inayokifanya kitu kibadilike au kwa uzuri, yaani kuongezeka; au kwa ubaya, yaani kupungua nguvu hizo. Nguvu hiyo inafuata nafasi ya ngazi ambayo kitu husika kinashikilia. Mtu anashikilia nafasi ya juu zaidi kati ya viumbe hai kuliko mnyama, mnyama anashikilia nafasi ya juu zaid kuliko mmea na mmea unashikilia nafasi ya juu kuliko kitu kisicho na uhai. Katika mlolongo huu wa kuwa na nguvu-hai kwa kila kitu, nafasi ya kitu ni muhimu sana.

Kwa kufuata mafundisho au imani hiyo naona muasisi wa dhana ya kujivua gamba alitoa dhana hiyo kama mwafrika anayeamini, kwa kujua au kwa kutojua, kwamba CCM ni kitu hai chenye nguvu hai ambacho kinaweza kuongeza au kupunguza nguvu-hai yake. Kwa vile CCM, kama kitu hai, inaonekana kupunguza nguvu-hai yake, kinachotakiwa ni kujiongezea nguvu-hai yake kwa kuondoa u-nje, yaani gamba, ambao ndio unakifanya chama hicho kikose mvuto mbele ya umma.

Je, dhana hiyo ina nguvu au udhaifu gani kifalsafa? Kwa kutumia dhana ya kiumbe hai (nyoka) tukitambua kwamba nguvu hiyo imo ndani ya kitu hicho, yaani ni sehemu mahsusi ya kiumbe hicho tunaifanya CCM ionekane au kueleweka kama kiumbe hai kinachojiendesha chenyewe na ndiyo maana kinajipa jukumu la kujivua gamba. Je, hii ni sawa na sahihi?

Tukifuata mapokeo ya CCM hiyo hiyo na kwa kudurusu fikra na maono ya Waasisi wake tutagundua kwamba Mwl. Nyerere alipoona nchi ina matatizo na inahitaji marekebisho makubwa kama kilivyo Chama Cha Mapinduzi, alitumia alama ya nyumba na siyo ya kiumbe hai. Alisema, ukijenga nyumba ukaipamba na kuona kuwa ni nzuri na imara, hauwezi kuwa na uhakika wa uimara wake hadi pale itakapopata msukosuko mkubwa wa mvua au kimbunga. Mvua na kimbunga zikitokea nyumba hiyo ikapata nyufa, utapata nafasi ya kurekebisha nyufa hizo na kama zinagusa msingi utalazimika kuvunja nyumba hiyo na kuijenga upya kwenye msingi mpya. Kwa kutumia dhana ya nyumba na siyo ya nyoka, Mwalimu alitumia dhana inayoonyesha kwamba CCM au Taifa ni matunda au tokeo la watu ambao wanafikiri na kuweka fikra zao katika uhalisia. Taifa kama kilivyo chama cha siasa ni tokeo la fikra na siyo tunda la maumbile.

Ukitumia dhana ya nyoka kwa kutoa fikra za namna ya kukifanya chama kiwe hai, unaleta wazo la kifo ambalo linatisha. Wazo la kifo ndilo linalazimisha tendo la kujivua gamba maana kisipojivua gamba hilo hakina namna nyingine ila kufa. Wazo la kujivua gamba siyo wazo linalotokana na fikra tunduizi. Ni wazo linalotokana na ulazima wa kimaumbile, sharti la kuendelea kuishi. Wazo la nyoka (yaani CCM) linamfanya “mwenye nyoka” (wana CCM) awe kibaraka wa kitu chake; badala ya kuwa mtengenezaji au muumba wake. CCM haijimiliki wala kujiendesha (kama nyoka) bali ilianzishwa,tena inamilikiwa na kuendeshwa na wana CCM.

Wazo la jengo tofauti na wazo la nyoka, linalompa mjenzi au mwenye jengo, kuwa na uwezo juu ya jengo lake. Anaweza kuangalia kama jengo hilo ni imara au linalingana na matakwa yake ya wakati huu. Na kutokana na kuangalia kwake anaweza au akalikarabati au hata kulivunja, akachukua baadhi ya vipande vya jengo lake la zamani na kujenga jipya linaloendana na mahitaji ya wakati huo. Hataogopa matokeo yake, maana jengo tofauti na nyoka, haliwezi kufa, litabomolewa. Na likibomolewa, yeye kama mjenzi atafanya kama kile anachotuasa Kezilahabi katika riwaya yake ya Mzingile: “maisha ni kama mkufu, unachukua kipande hiki unakiunganisha na kingine. Kile kisichokufaa kiache kitamfaa mwingine”.

CCM ya sasa haiwezi kupata nguvu na mvuto mpya kwa kujivua gamba. Tena gamba lenyewe ni la nyoka analojivua mwenyewe na wala si la mti ambalo linatoka lenyewe. Sana sana inachoweza kufanya CCM ni kuishia kujikata vipande vipande ambavyo labda havionekani kuhatarisha uhai wake wakati ikibaki ni ile ile yenye chembechembe zile zile ambazo hazikidhi mahitaji mapya ya wakati uliopo.

CCM lazima ibomolewe. Ichukue vipande vile vinavyofaa iviunganishe na vingine; vile visivyoifaa iviache vitawafaa wengine. Baada ya kuchambua vifaa vya zamani na kuangalia vipya vinavyofaa kwa jengo inalolitaka; ijenge jengo jipya linaloweza kustahimili mikikimikiki ya wakati huu. Kuondoa mabaka na bati linalovuja kwenye nyumba ambayo msingi wake unalegalega, ni kujidanganya. Katika lugha inayoeleweka; kuwanyooshea vidole baadhi ya wanachama wa CCM na kutishia kuwaondoa eti chama kitakuwa safi ni uongo wa mchana. Haviwezi kuleta mabadiliko katika CCM. Yataishia kwa kikundi kimoja kunyoshea mkono kikundi kingine na vurugu za namna hii zitashinda kwa kutegemea utashi wa fedha na siyo utashi wa kisiasa.

Nini kifanyike katika kubomoa jengo la sasa la CCM na kulijenga jipya?

Uongozi wa CCM hauna budi kuangalia upya katiba yake: imani yake, madhumuni na lengo lake; pamoja na kupanga njia za kufikia lengo na madhumuni hayo. Kuangalia mfumo wa chama kama vile uwakilishi kutoka wilayani badala ya mkoani, bado haitoshi. Mfumo hauji kabla ya Sera. Sera kwanza mfumo baadae. Baada ya kuweka wazi sera inayokiongoza chama ndipo iweke vigezo vya wale wanaoweza kuwa viongozi kwa kuangalia kama matendo na maisha yao yanalingana na imani na sera ya chama.

Kwa mfano, hauwezi ukawa na chama kinachoamini katika kutetea wakulima na wafanyakazi ambacho kitakubali wanaotunga mikakati ya chama chake imkubali kabaila au bepari anayeajiri wafanyakazi wengi awe mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu. Kabaila au bepari hawezi kutunga sheria au ilani za kumlinda mkulima wa kawaida au mfanyakazi. Yeye kama mfanyabiashara atataka wakati wote awe na sheria inayolinda na kumpa faida zaidi. Hilo halihitaji msomi wa Ph.D. kulitambua. Akili ya kawaida kabisa tunayozaliwa nayo inang’amua hayo.

Baada ya kuwa viongozi wa CCM wameandaa muswada mpya wa chama chao, waitishe mkutano mkuu wa chama, wawaite wenye nyumba na kuwapa ramani ya nyumba mpya wanayopendekeza ijengwe; kama wakikubali mapendekezo yao basi yapitishwe na yawe ndiyo mwongozo wa chama, iwe ndiyo sera. Hapo watu watajiondoa wenyewe kwa vigezo vinavyofahamika na vilivyo wazi. Kama hilo halifanyiki, tutaendelea kuona mapambano ya mtu kwa mtu, jino kwa jino, yakiongozwa na vikundi ambavyo vinafadhiliwa na wenye pesa.

Turudi kwenye historia ambayo tunaambiwa ni mwalimu mkuu. Hilo ndilo lililotendeka wakati wa TANU. Baada ya kuona wana TANU wenye nguvu na madaraka ndani ya chama hawaendani na matakwa ya wananchi ya kugawana rasilimali za nchi tuliyopigania wote iwe huru; viongozi wa TANU walitoka na wazo la Azimio la Arusha. Wakaweka pamoja fikra zao, wakatengeneza mwongozo na maono yao; wakaitisha mkutano mkuu ukapitisha azimio likawa ndiyo kigezo cha uongozi. Wale ambao hawakuwa tayari kuongoza katika TANU ya wakati huo wakajiondoa wenyewe na nchi ikawa salama.

Kwa nini historia yetu wenyewe haitufundishi? Kweli viongozi waliokaa kwenye madaraka kwa muda mrefu na waliokuwa na maslahi yao wataondoka hivi hivi bila kuleta madhara kwa chama na kwa nchi? Sidhani.

Napendekeza wana CCM wasome tena Azimio la Arusha. Watenganishe taswira iliyotolewa na viongozi wa TANU, ambayo ni sehemu kubwa ya kajitabu ka Azimio, na waone jinsi wazee wetu wa TANU walivyotoa Azimio lao baada ya kuelezwa, kuelewa na kutafakari yale waliyoelezwa ndipo wakaazimia. Azimio lenyewe, kwa wale wanaotaka kulisoma, si refu. Ni fupi sana. Kirefu na ambacho kilichukua muda mrefu wakati wa mkutano mkuu wa kule Arusha, ni maono, maelezo na mafafanuzi yaliyofanya Azimio likaazimiwa.

Tunahitaji watu wa kutumia vichwa vyao kufikiri badala ya kuangalia matumbo yao. CCM ijenge upya sera yake. Kwa sasa haipo na kama ipo haijulikani hata kwa viongozi wenyewe. Mwalimu aliwahi kusema kwamba CCM inahitaji viongozi ambao ukimwangalia usoni tu unaona anaendana na kile anachoamini.

Hakuna anayeweza kuwaondoa watuhumiwa wa ufisadi na chama kikabaki salama bila kuweka sera mpya. Wanao wafuasi wengi kila mahali: kwenye matawi, wilayani, mikoani mpaka taifa. Kuwaondoa hao wanaoitwa mafisadi bila kuweka bayana imani na sera za chama ni kutotumia akili katika upeo mkubwa wa kutunduiza; ni kujibu maswali magumu kwa majibu mepesi.

Kwa mawazo yangu, wazo la nyoka kujivua gamba, linamfanya “mwenye nyoka” awe kibaraka wa kitu chake. Kitu kinakuwa na nguvu kwa vile anafikiri kina nguvu-hai. Wana CCM ndiyo wajenzi wa jengo lao. Wanaweza kulibomoa kama wanaona halikidhi vigezo vya sasa au wanaona limevamiwa na vichuguu na mchwa humo ndani ya misingi yake. Wanaweza kuchukua baadhi ya vifaa vya jengo la zamani na kujenga jipya lililo imara zaidi linaloweza kuhimili vishindo vya uchumi wa ukoloni mamboleo unaohubiriwa na utandawazi.

TUTAFAKARI.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP