Tuesday, August 16, 2011

KUTOKA KWA WAZIRI KIVULI WA ARDHI

MIGOGORO YA ARDHI

Mheshimiwa Spika,migogoro ya ardhi hapa nchini hivi sasa imekithiri kufikia hatua ya uvunjifu wa amani na kufikia hadi umwagaji damu na pengine vifo kutokea katika maeneo kadhaa. Hali hii imeondoa utamaduni wetu wa asili wa kuvumiliana na kumaliza matatizo yetu kwa njia mwafaka za mazungumzo. Ni muhimu serikali ikaelewa kwamba kupuuza migogoro hii ya ardhi nchini ni sawa na kuatamia bomu, hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe!

UWEKEZAJI, UBINAFISHAJI NA HATMA YA ARDHI YA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, Migogoro, hasa ya wananchi na wawekezaji inakua kwa kasi na kuchukua sura mpya. Anapokuja ‘mgeni’, kwa jina la ‘Mwekezaji’ matendo ya Serikali yetu, yanapingana na usemi usemao ‘mgeni njoo mwenyeji apone’ bali imekuwa ‘mgeni njoo mwenyeji asulubike’ .

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali inawapa matumaini makubwa wakulima wa Tanzania , kwa mipango kabambe ya kilimo cha kisasa, pamoja na uwekezaji mkubwa wa kilimo utakaogharimu mabilioni za dola la kimarekani kutoka kwa wanaoitwa wafadhili, hoja za msingi ni kama kilimo hicho kina malengo ya kumnuufaisha mkulima wa Tanzania , au malengo yake ni kupokonya ardhi ya wazawa na kisha kuwageuza vibarua /manamba ndani ya ardhi yao!

Mheshimiwa Spika,Utafiti uliofanya na HakiArdhi juu ya hali ya maeneo yaliyokuwa ya Nafco, NARCO na Mashamba yaliyotelekezwa wamebainisha yafuatayo:1) Ubinafsishwaji wa mashamba ulitawaliwa na utata na udanganyifu mkubwa hali iliyopelekea uadui baina ya wawekezaji na wakulima wadogo wadogo kwa upande mmoja na mgogoro kati ya wakulima wadogo na wafugaji kwa upande mwingine 2) Katika maeneo ya yaliyokuwa mashamba ya Ngano, Hanang (Hanang Wheat Complex (HWC)) na Dakawa Ranch iligundulika kwamba wakati wananchi wanaozunguka mashamba hayo wana mahitaji makubwa sana ya ardhi wawekezaji na vigogo wenye fedha wamejilimbikizia maeneo makubwa ambayo hawayaendelezi kwa kwa ukamilifu[1].

Kambi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu na watanzania kwa ujumla nini kilichojiri katika ugawaji wa ardhi ya iliyokuwa Dakawa Ranch na ni wanakijiji wangapi walinufaika na mgao huo!

3) Wawekezaji kuwakodisha wananchi wenyeji mashamba kwa ajili ya kilimo na kuwatoza fedha. Haya yalitokea katika Mashamba yanayomilikiwa na Rai Group ambapo wananchi walikuwa wanakodisha $ 10 kwa ekari. Hali kama hii pia inafanyika katika Shamba la mpunga Mbarali na Kapunga, yote yakiwa wilaya ya Mbarali.[2]4) Mashamba yaliyotakiwa kurejeshwa kwa wananchi lakini hayajarejeshwa , kati ya mashamba hayo ni shamba la Gawal na Warret ,lililopo Hanang lenye ukubwa wa hekta 4,000. Maamuzi ya kuyarejesha mashamba kwa wananchi yalifanyika toka mwaka 2004/05.[3] Kambi ya upinzani inataka kauli ya serikali kuhusiana na mustakabali wa mashamba haya! Kambi ya upinzani inaitaka pia serikali itoe tamko juu ya mustakabali wa shamba la Bassotu.

(SEHEMU YA HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MWAKA WA FEDHA 2011/2012)

Soma Hotuba nzima hapa:

Soma Ripoti ya Hakiardhi hapa:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP