Loading...

Monday, October 24, 2011

MWAMKO WA VIJANA KISIASA NA HATIMA YA TANZANIA

MWAMKO WA VIJANA KISIASA NA HATIMA YA TANZANIANa. M. M. MwanakijijiMojawapo ya mambo ambayo yamejitokeza katika uchaguzi huu mkuu uliopita na ambayo naomba kupendekeza kuwa hayahitaji ubishi tena ni kuwa siasa za Tanzania haziwezi kuwa kama zilivyokuwa nusu karne ya uhuru wetu inayoyoma katika historia. Kwamba uchaguzi huu mkuu uliopita wa Rais na Wabunge umesimika mara moja na daima nafasi ya vijana katika kuamua mwelekeo wa taifa, nafasi ambayo haiwezi kufutwa tena na matakwa ya mtu, kikundi cha watu, vitisho au mabezo ya kisiasa. Kwamba vijana wa Tanzania wameamka na hatimaye kulazimisha kuchukua nafasi yao ya wanayostahili katika kushiriki kwenye uongozi wa taifa lao.Kwa maoni yangu kuna matukio machache ambayo yamelazimisha vijana wengi kuwa na mwitikio mpya wa kisiasa kuliko wakati mwingine wowote hasa tukikumbuka kuwa kwa miaka mingi sana wakati wa chama kimoja na wakati wa mfumo wa vyama vingi vijana walikuwa wanapaswa kupitia uongozi wa vijana na kulelewa kwenye vyama kabla ya kuanza kuingizwa kwenye uongozi wa taifa. Kwa upande wa CCM huu ndio ulikuwa utaratibu wa muda mrefu ambao ulikuwa unafuata modeli ya vyama vya kisoshalisti na kikomunisti.

Hata hivyo, miaka michache tu iliyopita ilibadilisha kabisa mfumo huo kwani vijana wawili ambao naweza kuwaita wanasimama kama miongoni mwa waanzilishi wa mwanzo wa kuwahamasisha vijana kuingia zaidi kwenye siasa za Tanzania walipojitokeza. Uchaguzi wa 2005 uliingiza Bungeni vijana wawili tofauti lakini marafiki na wakitoka katika vyama viwili tofauti. Vijana hao ambao ni Amina Chifupa (sasa marhemu, kutoka CCM) na Zitto Kabwe toka CHADEMA waliwakilisha sura mbili tofauti kabisa za vijana wa Tanzania ambazo katika uchaguzi huu wa 2010 tumeziona zikijitokeza tena. Zitto Kabwe, kijana msomi, mahiri wa kuzungumza na mwenye moto wa ujana aliwakilisha kundi la vijana wasomi. Amina Chifupa kijana mchangamfu, mwenye kuthubutu lakini siyo mwenye usomi wa hali ya juu aliwakilisha kundi la vijana wa elimu ya kawaida ambao mara kwa mara katika jamii wanapuuzwa na kutopewa umuhimu sana.Wakati Zitto aliwakilisha (kama alijijua au la ni somo jingine) vijana wenye elimu ya juu, wenye hamu ya kushika uongozi na madaraka na ambao wanajiandaa kuwa viongozi wa baadaye wa taifa, Amina Chifupa aliwakilisha (kama na yeye alijijua au la nalo ni somo jingine) kundi la hao vijana ambao wanahitaji kusikilizwa na kupewa nafasi ya kusikilizwa. Hawa wawili wakajikuta wanaleta kwenye siasa za Tanzania sura mbili za vijana wetu; wasomi na wanaotamani uongozi wa juu (kina Zitto) na wafanyakazi na vijana wahangahaikaji ambao wanataka kupata nafasi ya kusikilizwa. Kila mmoja kwa namna moja au nyingine alikuwa ni sauti ya vijana wa Kitanzania. Sauti ambayo ilitakiwa kupewa nafasi na kusikilizwa.Matukio yote yaliyofuatia tangu kuchaguliwa kwa vijana hao wawili hadi uchaguzi mkuu wa 2010 yaliweka wazi mbele za jamii kuwa vijana wa Tanzania hawawezi tena kukaa nje ya siasa za Tanzania. Matokeo yake ni kuingia kwa vijana wengi kwenye nafasi mbalimbali za uchaguzi kuanzia udiwani na ubunge. Matokeo yake ni kuwa uchaguzi uliopita umeonesha kuwa vijana wa Tanzania wakiamua kama mtu mmoja mmoja au kama kikundi wanaweza kabisa kulazimisha kuchukua nafasi yao kwenye uongozi wa taifa. Hata hivyo kuna kitu kingine ambacho naamini kimetokea kuwafanya vijana wajitokeze zaidi kuwania nafasi za uongozi wa taifa lao katika uchaguzi mkuu uliopita.Kushindwa kwa wanasiasa wakongwe kusoma alama za nyakati na kujibadilisha kuweza kuendana na ukweli mpya wa kihistoria ni kitu kingine kilichotokea hapa katikati. Miaka nenda rudi Watanzania walizoea kuyasikia majina fulani katika siasa; vijana waliokua kati ya miaka ya themanini na tisini wamejikuta wanaingia utu uzima huku majina yale yale yakizunguka katika kumbi za madaraka. Mabadiliko ya kisiasa na kimaisha katika Tanzania hayausababisha wanasiasa wetu wakongwe kusoma alama za nyakati na kubadilika. Matokeo yake vijana wakaanza kuwa na shauku ya kutaka kuleta mabadiliko ambayo wazee yamewashinda. Wakongwe katika uongozi wetu wakawa wamezama katika kutengeneza maisha ya watoto na wajukuu wao na kusahau maslahi ya taifa. Matokeo yake wakaanza kuingia mikataba mibovu, wakaachilia ufisafi ukue huku wakiamini majina yao ni kinga. Vijana wakasema inatosha. Vijana wakaamua kuingia ili waje kusahihisha makosa ya wazee hawa. Au angalau waliamini kuwa wao wakiingia wanaweza kuja na mawazo mapya.Hata hivyo jambo la mwisho ambalo naweza kusema limetokea na kubwa zaidi na likijumuisha mambo mengine yaliyotokea miaka hii mitano iliyopita ni mabadiliko makubwa ya kifikra ambayo yametokana na vijana wa sasa kupata nafasi ya kujua mengi kuliko vijana wa miaka michache tu iliyopita. Wakati vijana wa zamani walitegemea radio na maneno ya mdomo kupeana taifa vijana wa leo wana simu za mkononi, luninga, internet n.k na hivyo wanapata taarifa haraka, za kina na bila kuchujwa. Jambo hili limewafungua vijana kuelewa zaidi haki zao, kutambua matamanio yao na kuanza kuona kuwa na wao wanaweza kufanya vitu vinavyofanyika sehemu nyingine duniani. Ninaamini kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita naweza kusema kilikuwa ni kipindi cha mapinduzi ya kifikra. Yaani, vijana wetu wanafikiri tofauti sana na wazee wao; wanahoji zaidi, wanauliza zaidi, na wao wenyewe wanatafuta majibu! Leo hii kijana hawezi kuambiwa “kaa kimya kwa sababu mkubwa anasema” naye akakaa kimya bila kunung’unika.Yote haya na mengine mengi yametudokeza kitu kimoja ambacho nimekisema mwanzoni, Tanzania ya leo haiwezi tena kurudi ilikokuwa. Vijana wameamka na siyo kuamka tu wamejitokeza kutaka nafasi za uongozi wa taifa lao. Naamini changamoto kubwa sana ambayo upande mmoja inanitisha na upande mwingine inanitia matumaini ni kuwa vijana hawa wako tayari kutumika. Tatizo kubwa ninaloliona ni kuwa vijana wetu hajapata nafasi ya kuandaliwa kuwa viongozi. Nikiangalia vijana walioingia Bungeni na kwenye serikali za mitaa ninafurahi kwamba wako tayari lakini ninatishwa na uwezekano wa kile kile kilichotokea kwa vijana walioingia kwenye utumishi wa umma miaka ya mwisho ya sitini!

Kundi lile la vijana ndio leo tunawaita ‘wazee’ wetu. Hawa waliingia kwenye utumishi wakileta matumaini kwamba ni wasomi na wako tayari kujifunza. Lakini walipoonja madaraka hasa baada ya Nyerere kuachia ngazi walitambua kuwa ulikuwa ni wakati wao. Vijana waliosifiwa kwa uadilifu na walioaminiwa wakageuka ndio watawala wabovu na wengine kwa kweli kabisa majina yao yatatajwa katika historia kwa masikitiko. Hili ndilo linanitisha zaidi. Vijana hawa wa leo ambao watu wanawafurahia kuwa wameingia madarakani na kuleta matumaini wengine tumeshaanza kuwaona wameonja kile kileo cha madaraka na wameanza kulewa; wameanza kuamini wao ni wao na hata wengine wameharibiwa kabisa na madaraka hayo. Na tumewaona wengine wakikataliwa na kizazio cha wenzao.Sasa utitiri huu wa vijana Bungeni na kwenye serikali za mitaa na nafasi mbalimbali za uongozi ni dalili njema? Je ni tiba ya tatizo la uongozi tuliloliona miaka mitano iliyopita au ni dalili tu kuwa tusipoangalia kumbe tumeongeza matatizo zaidi huko mbeleni kwa kuwa na vijana ambao hawakuandaliwa vyema kushika uongozi?Swali kubwa ambalo hatuna budi kubakia nalo basi na kulitafutia jibu ni jinsi gani viongozi hawa vijana wanaandaliwa, kusimamia na kupewa nafasi ya kulitumikia taifa bila ya kuwaweka katika mazingira ambayo wataharibiwa na madaraka na unono wa vyeo?Vinginevyo, miaka ishirini au thelathini kuanzia sasa wakati vijana hawa watakapokuwa ndio “wazee” tutajikuta tumerudi pale pale kwa wazee wa sasa hivi ambao ndio walikuwa vijana wa kwanza baada ya uhuru kushika madaraka. Tutajikuta tunahangaika bado na mikataba mibovu, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka; matatizo ya wazee wetu leo hii ambao miaka thelathini tu nyuma ndio walikuwa vijana waliolipa taifa letu matumaini.

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP