Loading...

Saturday, October 15, 2011

VIJANA WA TANZANIA

VIJANA WA TANZANIATangu alipotutoka, baba yetu wa taifa,

... Mwalimu alosifika, tulompa nyingi sifa,

Kizazi tulikiweka, cha kukomboa taifa,

Tukakiita vijana, vijana wa Tanzania.Tukakivika viatu, vyenye kuzuia miiba,

Tukakivika kofia, yenye kuzuia jua,

Tukakivika myavuli, ili kuzuia mvua,

Tukakikingia ngome, kizazi cha Tanzania.Bashiru amesimama, kama Mkuki wa chuma,

Awaita kusimama, vijana wenye hekima,

Unganeni akasema, wachagga na wasukuma,

Ili tuinusuru nchi, vijana wa Tanzania.Wala hakuwa Nkuruma, Ni ukumbi wa Mwalimu,

Nimemwona alalama, pia atoa elimu,

Kigoda kikiwa wima, kwa shairi lilo tamu,

Akawaita vijana, vijana wa Tanzania.Ili waje wimawima, ‘kuonewa tumekoma’

Tuirudishe heshima, ya nchi iliyokama,

Awataka kusimama, ili wathubutu vema,

Vijana wa Tanzania, vijana wa Tanzania.Tukomboe twiga wetu, almasi na dhahabu,

Pia navyo vyura vyetu, kuuzwa bila sababu,

Ardhi yetu bikira, kubakwa tukiwa bubu,

Akataka waungane, vijana wa Tanzania.Ataka wajitahidi, wasiogope lawama,

Bila kuhofu baridi, wala giza la mtama,

Na mabomu ya baridi, wadai yetu heshima,

Waje bila kukaidi, vijana wa Tanzania.Namuonea huruma, mwalimu nahurumia,

Siwezi mpa lawama, kazi ye kajifanyia,

lakini wamesima, tuli wamuangalia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wanasita kusogea, ili kuokoa umma,

Wao wamenyongonyea, sura zao kama kima,

Meno yamewasogea, wengine kama wanyama,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Woga umewavamia, watetema kama ndama,

Nywele zimewasimama, kama miti ya kahama,

Miguu yawatetema, yashindwa hata kuhama,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wengine wao kijani, kama mashamba ya bangi,

Wengine na maruhani, nyekundu ni yao rangi,

Wa rangi ya baharini, vichwa ni kama mitungi,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wamerithishwa na njaa, njaa kama ya ngamia,

Ma mioyo ya tamaa, macho yao na mikia,

Wajiita wajamaa, zalendo wajisifia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wamekuwa mabwanyenye, Kamata alivyosema,

Walipoenda kanyenye, na kijiji kimehama,

Ardhi ya Wakanyenye, wakalia wakulima,

Vijana wa Tanzania, wamegeuka ngamia.Wamegeuzwa ngamia, wabebeshwa magunia,

Wengine wawatumia, wamewageuza njia,

Daraja la kuvukia, ili ng’ambo kuvukia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wengine wawatumia, wawageuzageuza,

Mbele wakijishibia, nyuma wanawageuza,

Utamu ukiishia, kama samaki wauza,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Myavuli wamegeuzwa, mvua kujifunikia,

Viatu wamegeuzwa, wao wawakanyagia,

Majamvi wamegeuzwa, wengine wawalalia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Wengi wao ni ngamia, si watu kukimbilia,

Macho yamewang’aria, sumu wameshawatia,

Tuliowategemea, wamegeuzwa ngamia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Nani ataiokoa, nchi inaangamia,

Tuliowategemea, wamegeuzwa ngamia,

Matumbo yamelegea, njaa imewazidia,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Hata tukiwachangia, mbegu tukawapatia,

Shamba hawatozitia, njiani watajilia,

Wana njaa yatishia, vijana wa Tanzania,

Vijana wa Tanzania, wamegeuzwa ngamia.Shime wote Tanzania, tuunde kipya kizazi,

Kitakachotusaidia, tulinde hiki kizazi,

Tukifunike pazia, kisichafuke kwa nzi,

Kizazi kitachoitwa, vijana wa Tanzania.Tukilinde tukilee, kiwe juu ya mlima,

Kilime mwingi mchele, kiwalishe wakulima,

Wa kalamu chekelee, mwisho giza kulizima,

Tukomboe nchi yetu, Tulinde Uhuru wetu.Shairi: ©Respicius Shumbusho Damian


Picha: ©Jakaya Kikwete

1 comments:

Anonymous October 29, 2011 at 4:58 PM  

Jamani huyu mshairi ana maneno yanagusa kweli. Kwa nini asikae akatuandikia kitabu. His poems are as sharp as those of Bitek. Nitapata wapi mawasiliano yake tushirikiane kuandika?

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP