Loading...

Thursday, November 17, 2011

TUNAANDAA KATIBA AU TUNAANDIKA KATIBA?


Mchakato huu ni wa Kuandaa Katiba au Kuandika Katiba?Salma MaoulidiJana nimeugua ghafla, nimelala taabani kitandani sijiwezi, sijitambui. Nimeugua baada ya kufuatilia sehemu ya mjadala unaoendelea Bungeni unaohusiana na Muswada unaokusudiwa kuweka utaratibu wa kupitia ama kutahmini ama kudurusu (review) Katiba. Kwa bahati mbaya nilichokisikia na kukishuhudia ni utamaduni unaojirudia miongoni mwa wabunge na viongozi kwa ujumla wa kumuanika na kumtuhumu mchawi kwa yale mambo wasiokubaliana na msemaji.Mara hii mchawi ni Mhe. Tundu Lissu kwani ndiye aliyesoma hoja ya wapinzani Bungeni kuhusiana na Muswada husika. Ila anavyozungumzwa na kuandamwa Tundu Lissu kwa sasa ni hali kama ilivyokuwa wakati Mhe. Zitto Kabwe alipohoji suala zima la mikataba inayoingiwa kiholela ambayo inaiweka nchi yetu pabaya kiuchumi. Hususan alihoji mikataba katika sekta ya madini na nafasi ya watanzania kukubali kulipa au la madeni inayotokana na uzembe ama uroho wa viongozi.

Wakati huo Zitto alionekana mtovu wa adabu na hata kuandamwa na washabiki wa vyama waliotaka ‘damu au nyama’ yake. Wabunge walio wengi hawajataka kuikabili na kuijadili hoja ila walitaka kumvaa Zitto kama kijana, anayejidai msomi, mwanaharakati na kosa kubwa lilikuwa kuwa yeye ni mpinzani. Matokeo yake Zitto alifungiwa kuwakilisha wapiga kura wake katika vikao kadhaa.Siku nenda siku rudi hata baadhi ya wabunge katika Chama Tawala wameibebea bendera hoja ya ufisadi na upotoshaji wa mikataba ya uwezekaji inayoitia nchi hasara. Leo, suala la kushughulikia walioingiza nchi katika hasara iwe katika mikataba yanayohusu upatikanaji wa nishati, ununuzi na uendeshaji wa migodi, ununuzi wa rada na nyanja nyingine nyingi imekuwa ni ajenda namba moja ya raia.

Wakati huo nilijiuliza mbona mtu kama Mhe. Slaa akitoboa mambo Bungeni alikuwa hashambuliwi kwa kiasi cha Zitto? Au hata wabunge wengine katika chama tawala waliothubutu kuhoji baadhi ya sera na mwenendo wa chama chao walikuwa hawaandamwi kwa lugha na kishindo kama ilivyokuwa kwa Zitto? Bila ya shaka namna ya kuuliza na kuongea kwa Zitto hakukuwapendeza wengi kwa vile alionekana kuwa Mbunge chipukizi tena msomi hivyo kuonekana si tu tishio lakini huenda akawa ana jeuri ya kisomi na alihitaji kuwekwa katika nafasi yake. Huu ni ugonjwa hapa kwetu Tanzania yaani kuwekana katika nafasi yetu, kuonyeshana.Hakika bado wengi wanapata shida na utamaduni wa kuhoji ama kuhojiwa labda waulizwe na wafadhili wa nje lakini si na mbunge anayeonekana kijana, tena msomi mwenye uthubutu na si mbembwe tu. Pia hatujazoea kuweka ajenda ya kitaifa kuliko ya chama au binafsi. Kwa vile mwisho wa siku ujasiri huu huleta umaarufu basi dawa ya kukata mzizi wa fitina ni kumpaka mtu matope.Zitto na Lissu si malaika. Wana mapungufu yao kama kila mmoja wetu. Hivyo, tataizo liko wapi? Bila ya shaka kwa Bunge lililozoea kufanya kazi kwa misingi ya “ukuu” yaani nani ndio mzee wetu na aliyetutangulia, ama linalofanya kazi kwa misingi ya uwanachama yaani huyu mwenzetu au si mwenzetu na pia linalofanya kazi kwa misingi ya mahusiano ya matabaka yaani ‘hierarchy’ inayoshughulishwa na ada iliyojiwekea na si ufanisi unaotafutwa na kutarajiwa, hulka za watu kama kina Zitto na hata Lissu zitawapa watu ambao wana mazoea fulani shida.Kwa watanzania wengi wanaotafakari mambo wanajiuliza iweje wabunge wanakosa kuongelea hoja ya muswada ulioletwa Bungeni na badala yake anatusiwa mtu, anachambwa mtu na si hoja? Iweje wabunge kwa wengi wao wote watetee suala moja kama vile hakuna masuala mapana ya kuzungumzwa juu ya muswada husika?Mtizamo wa Chadema ni wa Chadema wana uhuru wa kuwa na msimamo wao kama vile CCM au TLP walivyo na msimamo wao. Na wala haitakuwa ajabu kama wanachama wa chama kimoja watakuwa na mitizamo tofauti juu ya suala hili hata kama si wote watakuwa werevu wa kutangaza hivyo hadharani.Nadhani ugonjwa ulionisibu umesababishwa na sababu mbili kuu. Ya kwanza ni mshituko nilioupata na sijaweza kuamini kuwa wabunge wetu hawana ukomavu (maturity) ya kupambanua kilicho dhahiri na nyeti. Kuu katika hili ni kutoweza kubaini tofauti kati ya kuandika Katiba jambo ambalo wabunge wengi ndilo walilokuwa wakilizungumzia na suala la kuandaa Katiba mpya. Pili ambalo linahusiana na hili la mwanzo ni upeo wa kimtizamo kuhusiana na maana nzima ya kuandaa na si kuandika Katiba mpya.

Hakika kama muswada huu una nia tu ya kuwezesha katiba mpya kuandikwa basi wabunge wa chama tawala wana kila sababu ya kuhoji akina Lissu na dhamira yao. Lakini kama suala ni, kwa kupitia mchakato huu wa Katiba, kutafakari upya aina ya taifa tunalolitaka ikiwemo utamaduni wa utawala tunaoutaka basi hatuna budi kuelewa suala zima la uundaji wa Katiba kuwa pana kuliko kuandika tu Katiba.Kama hivi ndivyo kamwe haliwezi kuwa ni suala tu la kuunda Tume na kukusanya maoni lakini lazima lianze mwanzo katika kuandaa hadidu za rejea za mchakato wenyewe. Huwezi kufanya maandalizi ya kupika mseto halafu ukasema ukitaka kupika pilau chakula kikiletwa mezani watu wakakishangaa kuwa sicho walichoahidiwa! Lakini ndo tuseme hakuna namna nyingine zaidi ya kuwaza au kuunda isipokuwa kuwa na vyombo kama Tume kuongoza huu mchakato? Kwa nini kuweka urasimu kati ya raia, wadau wa kuu wa Katiba na matakwa na matumaini yao?Hakika kumekuwa na utata mkubwa katika utaratibu mzima wa kuandaa msingi wa kuandaa Katiba mpya. Kwa sasa sitaligusia suala la utata uliopo katika tarehe iliyotumika kuuwasilisha muswada huu inagwa tunaambiwa kuwa kuna marekebisho yamefanyika ilihali tarehe iliyouwekea sahihi muswada ni hata kabla muswada haujaletwa Bungeni kwa mara ya kwanza. Ama sahihi ya Katibu wa Baraza la Mawaziri imewekwa kabla ya Bunge la Bajeti. Hivyo, kilichobadilishwa hasa ni nini na lini ? Kisheria, unapokuwa na mkataba ukaufanyia marekebisho tarehe inayowekewa maanani ni ya mwisho yalipofanywa marekebisho na si ulipoandaliwa mara ya kwanza. Iweje Waziri wa Sheria afanye mambo ambayo hayaendani na msingi wa sheria?Kadhalika tunaambiwa muswada wa kwanza uliondolewa. Kisheria kama unaondoa kesi yako haina maana kuwa imesikilizwa. Hivyo kama mara ya kwanza Serikali au kama ilikuwa Bunge umeuondoa muswada na si kuukataa au kuagiza ukafanyiwe marekebisho iweje sasa usemwe kuwa unasikilizwa kwa mara ya pili na tatu ilihali uliondolewa?Hakika tumekuwa na Tume nyingi kabla yetu lakini tumepata tija gani kwa kuendelea na mifumo ya miundo ya Tume? Kuwa na Tume ndio kuwa na mchakato shirikishi? Au kuwa na Tume ndio kuhakikisha kuwa kila linalosisitizwa na raia litazingatiwa? Tuna haja tu ya kutizama yanayoendelea polisi na mahakamani tunapotoa maelezo yetu kujithibitishia kama mawazo ya raia zaidi ya milioni 30 yatawekwa maanani kwa namna yalivyowasilishwa kwao.

Hivi punde tu nasikiliza taarifa ya habari ambapo Waziri wa Sheria na Katiba tena anakoroga mambo kwa kusema wamejidhatiti kuchapisha katiba laki 2 ili kuzisambaza watu waijue Katiba yao. Kwa nini kazi hii ifanywe zaidi ya robo karne toka kupitishwa kwa Katiba? Aidha Dar es Salaam peke yake inasadikiwa kuwa na watu zaidi ya milioni nne hivyo katiba laki 2 ni za Ilala tu au na Temeke pia? Bila ya shaka kwa vyuo vilivyoko kwa sasa mjini Dodoma tu basi vinazidi idadi ya laki mbili. Sasa hizo Katiba zitakazopewa mashule na mawizara na asasi za kiraia zitajidurufisha zitoshe au tunazugana tu. Hakika ni kauli kama hizi watu wa Ze Komedi Orijino wanazoziita “danganya toto” ndio zinazowapa wananchi wasiwasi mkubwa.


Ingefaa wabunge wasome alama za nyakati badala ya kuendeleza siasa zilizopitwa na wakati. Kuna hoja za msingi mbele yetu ambazo wananchi wana shauku kubwa nazo. Haja ya kuandaa Katiba yaani 'Constitution making' ni mojawapo na hii ina tofauti kubwa ya 'Constitution writing' ambacho ndicho kikifanyika hapo awali na kinataka kuendelezwa na Bunge kama wakiridhia na kuupitisha Muswada huu. Suala ni kukubaliana upeo wa kuandaa Katiba si kufunga watu kifikra ili wasiwe na haki ya kufanya uchaguzi (exercising options) ya kile ambacho kitawafaa.


Raia Taabani0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP