Loading...

Sunday, December 25, 2011

Mabadiliko ya tabia ya nchi sio sababu pekee za Mafuriko

Ndugu Wadau,


Nimekuwa nafuatilia kwa ukaribu sana juu ya hali ya mvua na jinsi uokoaji unavyoendelea katika Jiji la Dar. Sambamba na hapo nimepata wasaa wa kusoma maoni ya wadau mbali mbali na mitazamo tofauti kuhusu suala la majanga. Na ni kweli inasikitisha na kutia simanzi sana kuona tunapoteza ndugu zetu na Watanzania wenzetu kwenye mafuriko kama haya sanjari na kuona watu wanapoteza mali zao na hivyo kulazimika kutafuta njia ya kurudi katika hali zao za mwanzo.


Ni kweli tatizo hili linatokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na hivyo Tanzania sio nchi pekee iliyokumbwa na mafuriko na kumbukumbu zetu zinaonyesha pia nchi za Marekani na Japani zilikumbwa na aina hii ya janga. Ila pia hatuwezi kuficha ukweli na kuishia kusosoneka bila kuangalia vyanzo vingine vilivyotufikisha hapa.


Kuna baadhi ya watu wanajitahidi kuzuia watu wasihoji suala hili kwa kisingizio kuwa sio wakata wa “siasa” ingawa mimi naona kwa nini watu wazuiwe kufanya hivyo maana bila kufanya hivyo tukiishia kusononeka tu hatutajua wapi tulipoanguka, kupasahihisha na kusonga mbele. Na hii sio mara ya kwanza watu kujificha kwenye mwamvuli huu wa “siasa” ili kuzuia watu wasihoji. Tunakumbuka kuhusu EPA, RICHMOND, mvua za Morogoro, MABOMU YA MBAGALA na kisha yale ya Gongo la Mboto n.k. Hatuwezi kwenda na mtindo huu lazima tubadilike.


Mbali na mabadiliko ya tabia ya nchi, tumefika hapa tulipofika kutokana na MIUNDO MBINU MIBOVU ya kupitisha maji na wengine kujenga kwenye mkondo wa maji mabondeni. Na hili mbali na jamii kupuuza watendaji wa serikali nao wanahusika katika hili maana wamefanya UZEMBE katika kutekeleza majukumu yao. Nakumbuka kipindi cha aliyekuwa mkuu wa mkoa Mhe. Yusuf Makamba alianzisha kampeni ya kubomoa nyumba zilizopo mabondeni (ingawa kulikuwa na hitilafu katika kutekeleza hilo zoezi) ila alionyesha nia ya dhati ya kuleta mabadiliko lakini siasa ziliingia na kulizuia hilo suala maana tulikuwa kwenye kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005. Tunapaswa kuwawajibisha viongozi wote wanaohusika na uzembe huu. Dar hata mvua ya saa 1 tuu inaleta maafa kwa wakazi wa maeneo ya Jangwani, Mikocheni, Kigogo, Mto Msimbazi, Tandale n.k ila tumekuwa hatujifunzi hata kidogo - hata mvua za El Nino za mwaka 1998 bado hazikutufunza!


Tunapaswa kuanzisha mtindo wa kuwawajibisha watendaji wetu na kinachoshangaza zaidi ni pale ambapo mbali na watabiri wetu kubashiri mvua hizi ila serikali haikujiandaa na hivyo kusababisha uzembe mwingine wa kuchelewesha uokoaji kwa wahanga. Na hili si sawa na haliwezi kuwa sawa.


Kutokana na hili tutegemee kuona uchumi ukizidi kuzorota maana uzalishaji utapungua, mfumuko wa bei utapanda tena maradufu kutoka hapa tulipo kwenye 19.2% na wengine kukosa kazi na makazi pia.


Moses Robson Kavishe

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP