Loading...

Thursday, February 2, 2012

BURIANI KAMARADI HENRY MAPOLU

SitaombolezaRafiki yangu, kamaradi Henry Mapolu


Sijaja kukuzika


Sijaja kukuaga


Sitaomboleza


SitabubujikaNimekuja na marafiki zetu


Na makamaradi wetu


Kupokea mchango wako


Kujikumbusha mfano wako


Ewe kamaradi!


Unatukumbusha mengi ya usafi, sio ya ufisadiUhongo wa kisiasa uliukata,


Ukaenda wilayani


Udisi wa Mzee Ruksa haukufarijisha,


Ukauficha ukayani


Aha! hili halikuwa geni kwako


Kwani ulijiuzulu Uzuoni,


Ukaenda UrafikiniMwito wako kuinua uelewa wa proletari


Hukujali kutunikiwa uzamili wa profesari


Ulituachia mabepari-chipukizi


Wakicheza ngoma ya ulimbikiziTumefika kukuenzi


Kwa fikra na mawazo yako


Kwa mtazamo na msimamo wako


Na waledi usiotetereka


Uaminifu usiopingikaWapo kina Adamu na Zakia


'Bakileki na Bgoya


Karimu na ukarimu wake


Na Kashiwaki namuona pakeWapo pia Joe na Jenerali


Sio wa wanajeshi


Wa waandishi-wacheshi


Sitaki niwasahau Mwami na mwenzie Masanja


Eti wakijidai wanasosolojia viranjaQorro wa Karatu


Amefuatana na Msoma Salumu


Aliyekuwa anatusalimu


'Venceramos! A luta continua'


Ndio kamaradi: A luta continuaAmekuja pia Rameshi


Vijana wakimtania 'wa Bangladeshi'


Na mwandishi mwenzio Nizari


Aishio nchi-kavu Kariakoni


Akijitambulisha orijino wa nchi-VisiwaniNamuona mheshimiwa Liundi, balozi


Akipambana na mawimbi ya machozi


Na Mzee Butiku amekaa majanini


Unakumbuka tulivyomsumbua ujanani?Nimemuona rafiki yako wa siku zile za Kivukoni


Mzee wetu, mzee Ngombale wa Kiliwani


Alikuwa anakuulizia juzijuzi


Nipashe za Kamaradi Henry asiye na upuuziSikuwa na ujasiri wa kumkumbushia


Barua yako ya wazi ulomrushia


Uonjo mkali wa kalamu yako katili


'Ewe kamaradi wangu wa prolitari


Usikubali kupigwa teke na siasa za jemadari'Kamwe sitosahau unyekekevu na utulivu wako


Kiburi uliepuka kama tauni, jazba zilikuwa geni kwako


Nilipotunga hadithi ya Amina na kijana mwanafalsafa


Nilikuwa nakuwazia wewe na usawa wa yako falsafaShati nje ya suruali, na ndara za kanda mbili


Ukiishi katika risachi fleti namba mbili


Yenye kuta pasi picha wala pambo


Isipokuwa Mzee Maksi na madevu yake ya majigamboNdugu yangu, rafiki yangu, Kamaradi Henry – mbele sitaenda


Nakuachie salamu za kamaradi chipukizi Sabatho Nyamsenda:


'Afrika imepoteza mmoja wa makamanda muhimu


katika vita dhidi ya mfumo huu dhalimu ...'.Issa bin Mariam


02/02/2011

Ndugu zangu,

Henry Mapolu ameaga dunia, juzi Jumapili jioni.

Ni kati ya waanzilishi wa Chama cha USARF na jarida la Cheche katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 60. Kwa mliopata kitabu cha "Cheche" mtakuta makala / taarifa zake.

Kwa mliosoma kitabu cha Walter Rodney "How Europe Underdeveloped Africa", mtakuta ametoa shukrani kwa watu wawili: Karim Hirji na Henry Mapolu.

Prof. Shivji anamwelezea Henri Mapolu kama ifuatavyo:-

Henry alichagua kuwa upande wa wanyonge mapema katika maisha yake tukiwa sote Chuo Kikuu, na kushiriki katika vuguvugu la mwamko wa nadharia na itikadi ya Ujamaa kwa mtazamo wa Kimaksi. Baada ya kufuzu shahada ya uzamili, bila kusita, Henry akaacha kazi yake ya uhadhiri chuoni na kujiunga na Kiwanda cha Urafiki kama Afisa Elimu ili aweze kutoa mchango wake kwa kuamsha uelewa wa wafanyakazi na wavujajasho juu ya hali yao halisi. Mimi binafsi ninafarijika kwamba niliwahi kufanya kazi naye kuandika, kukusanya na kuhariri makala ambayo yalichapishwa katika kijitabu kiitwacho 'Vuguvugu la wafanyakazi Nchini Tanzania'. Maandishi ya Henry Mapolu yataendelea kuwa nyenzo mojawapo katika mapambano ya wavujajasho dhidi ya mfumo katili wa ubepari.
Issa Shivji
30/01/2010

Hakika Afrika imepoteza mmoja wa makamanda muhimu katika vita dhidi ya mfumo dhalimu wa ubepari / ubeberu.

MAPAMBANO YA KUBOMOA NGOME YA UBEBERU YANAENDELEA

Sabatho Nyamsenda

1 comments:

Mbele February 2, 2012 at 11:25 PM  

Nimeshtuka kupata taarifa hii. Nilipoingia Chuo Kikuu Dar kama mwanafunzi, mwaka 1973, ndipo nilipoanza kumwona na kumsikiliza Henry Mapolu. Alikuwa mmoja wa wanaharakati waliotupa changamoto sisi vijana. Wanaharakati wengine walikuwa akina Issa Shivji, Mahmoud Mamdani, Yash Tandon, Dan Wadada Nabudere, Walter Rodney, Grant Kamenju, Josaphat Kanywanyi, Frank Mbengo, Gilbert Gwassa, Haroub Othman, Walter Bgoya, Kingunge Ngombale Mwiru, na wengine zaidi, kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Uganda, na kadhalika. (Kwa vile nimemtaja Kingunge, napenda tu kusema kuwa Kingunge Ngombale Mwiro wa leo si yule wa miaka ile, alipokuwa Kivukoni)

Tulijifunza mengi kutoka kwa wote hao. Henry Mapolu alibobea sana kwenye suala la wafanyazi na uongozi wa wafanyakazi. Kazi aliyoifanya, pamoja na wanaharakati wenzake, ilitupa motisha sisi vijana wa TANU Youth League, na baadhi yetu tulikuwa tulijiunga na naendesha jarida la "Maji Maji," ambalo lilikuwa ndio mrithi wa "Cheche." Kuondoka kwake kunatuachia pengo kubwa, ila mchango aliotoa ni hazina itakayoendelea kuwepo.

Natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki. Mungu awape nguvu ya kustahimili kipindi hiki kigumu, na amweke marehemu mahali pema Peponi. Amina.

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP