Loading...

Thursday, February 23, 2012

UHARIBIFU WA KISWAHILI MITANDAONI

UHARIBIFU WA KISWAHILI MITANDAONIZAVARA MPONJIKANimefurahishwa sana na waraka wa "Watanzania Tunavyokiharibu Kiswahili Twitter"na namna mwandishi anavyokabiliana na hili tatizo. Nimefurahi kuona kuna watu wengi wanaguswa na tatizo hili linaloanza kupevuka. Watu wengi wanaoingia humu kwenye hizi baraza za kijamii(Facebook, Twita) kiukweli wana zile athari za ulimbukeni.Ugonjwa wa ULIMBUKENI ni mbaya yaweza kuwa pengine kuliko UKIMWI na SARATANI, ila unaweza kupona. Inasikitisha kuona hadi leo watu wanadhani eti kuongea kikoloni ndo' ujanja. Bahati mbaya pamoja na kulundikana kwa mashule yanayoitwa English Medium hicho kikoloni bado hakina nguvu. Nimeshakaa na wanafunzi kibao wa vyuo vikuu ambao hawawezi kuongea lugha hii wanayoinyenyekea. Ni aibu kweli wanachokinyenyekea hawakiwezi na cha kwao kinaanza kuwaponyoka.Nilitarajia kwenye makala yako ungegusia kuhusu huu mtindo wa kuingiza herufi C (inatamkwa CHE kwa kiswahili) na kuingiza namba 2 na 4 kwa kujifanya kama mtu anaandika kikoloni, mtindo ulioanzia kwenye kuandika ujumbe wa maandishi kwenye simu. Kuna wanaohadaika kudhani eti ni ubunifu kuandika vile, wakati ukweli ni kwamba ni UJINGA wa hali ya juu. Maandishi na herufi hizo haziendani na lugha ya kiswahili hata kidogo. Ukiandika "m2" kwa kiswahili inasomeka "mmbili" - kitu ambacho unakuwa umeondoka kabisa kwenye mantiki. Kwanza hairahisishi lolote kwa vile inabidi utafsiri mara tatu ili kupata maana. Kwa hiyo kusudio la msingi linapoteza maana yake. Hii inadhihirisha watu hawajui kusoma na wana utata kwenye kuandika. Hili jambo limeanza kukomaa sana. utaona mtu anaandika "cina" akimaanisha sina ambapo kwa Kiswahili inasomeka C"chena". Je, hapo unawasilisha nini na kupunguza herufi gani? Kwa huo uandikaji ulikusudiwa na lugha ile kupunguza urefu wa maneno. Hapo ule ujinga niliousema unajidhihirisha.Sasa ina maana gani kwa neno kama hilo hapo juu iwapo idadi ya herufi inakuwa ileile?Inafaa tufanye juhudi za dhati wadau wa kiswahili hasa wa kizazi hiki kukemea na kufanya mambo mbali mbali kuonyesha madhara ya kudharau lugha na tamaduni zetu na kuendekeza vya wengine. Nimewahi kuwa na mijadala na watu wengi kuhusiana na suala hili, kuna wanaojitetea eti ndio usasa. Nilicheka sana na kuwaambia sio usasa bali ni ULIMBUKENI na kama hao wanaojaribu kuwanakili mbona hawachanganyi Kiswahili? Usasa iweje uwe unaathiri upande wetu tu?Hongera sana kwa kukemea hili, kwa wote wanaokemea tuko pamoja kwenye mapambano haya. Nahitilafiana tu kidogo na mwandishi wa makala kule Tanganyikan pale usemapo Kenya Kiingereza ndio lugha yao ya kwanza, hilo sio sahihi lugha ya kwanza haimaanishi lugha unayokutana nayo shule. Wapo watu wengine pia wanosema na kudhania kuwa Kiingereza ndio lugha ya kwanza. Nigeria hilo pia sio sahihi. Lugha ya kwanza ni ile unayoongea ukizaliwa, unayokuta mama akiongea nawe. Kule Kenya lugha za kwanza mara nyingi ni zile asilia na Kiswahili ni ya pili kwa mantiki hiyo, ila kiswahili ni lugha ya taifa ya Kenya pia kama ambavyo ni ya taifa hapa Tanzania. Huu mjadala ni mrefu tuendelee kujenga ili tunusuru taifa letu kuangamia kwenye dimbwi la maangamizi. Upendo na amani.Twitter: @Rhymson


Facebook: Zavara Mponjika

4 comments:

Shagihilu February 23, 2012 at 10:55 AM  

Nakuunga mkono kwa asilimia zote. Tumepotoka sana hasa kudhani kwamba kwa kuwa tunatumia mitandao ya kijamii ilotengenezwa na 'wadhungu' basi kila kitu tukiweke kwenye 'kidhungudhungu'!
Tujitahidi kuboresha lugha yetu katika mitandao. Hebu tuwe mabalozi sote hata kama maneno ya kiswahili hayatoshelezi.
Sote tuwajibike

Anonymous February 23, 2012 at 11:23 AM  

Kuna ulimbukeni mwingine ambao umeingia siku hizi wa kuandika herufi x badala ya s. Mfano mtu anaandika xana akimaanisha sana

siku4saa4 February 25, 2012 at 12:04 PM  

Huu ujinga lazima upigwe vita! Nimeshangazwa sana kusoma kwamba kuna ujinga wa namna hii! Ucku badala ya usiku!? Tunaelekea pabaya sana kwa mtindo huu

siku4saa4 February 25, 2012 at 12:08 PM  

Huu ni ujinga uliopitiliza yaani Xana badala ya Sana? Sasa hapo herufi na silabi ni sawa kwahiyo hata kama ni kujaribu kuokoa zile 160 za sms hakuna namna. Hii ni hatari sana kwa lugha kuharibika na watoto kushindwa kusoma na kuandika huko tuendako. Je taasisi za serikali zinaonaje hii? Usiku sasa itageuka Ucku? Huu ni upumbavu mkubwa

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP