Loading...

Friday, March 23, 2012

MJADALA WA UJANA NA URAIS WAZIDI KUPAMBA MOTO

WANAOPINGA KUONDOLEWA KWA KIKWAZO CHA UMRI WA URAIS WATOE HOJA

Sabatho Nyamsenda

Labda nitaje mapema kabisa kuwa mimi naupinga mjadala huu kwa lengo na namna unavyoendeshwa, aina ya watu wanaoushadadia, na baadhi ya hoja zinazotolewa. Lakini sipingi kuondolewa kwa vikwazo vya watu kugombea nafasi za kisiasa vikiwemo vigezo vya vyama na umri.

Mimi si shabiki wa nadharia za kibwanyenye. Lakini wananadharia wa kiliberali wanasema kuwa binadamu kwa asili yake amezaliwa na uhuru kamili ambao haupaswi kuingiliwa na mtu ama taasisi yoyote. Binadamu anapaswa kuwa mwamuzi wa maisha yake mwenyewe na kuzitumia fursa alizo nazo pasi na kuingiliwa. Mtu anayenyimwa uhuru ama fursa, haijalishi kama anaitumia ama la, anashurutishwa na kuonewa [‘she or he is being coerced’]. Hivyo, yule anayemnyang’anya mtu uhuru na fursa alizonazo anapaswa kujitetea na kuthibitisha uhalali wa kufanya hivyo.

Katika nchi yetu, tulikuwa na kiongozi mahiri na shupavu, lakini ambaye mara nyingi aliziminya fursa na uhuru wa watu kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kujenga umoja wa kitaifa na hata kujiimarishia mamlaka ya kuwa Rais mfalme. Mtu huyo ni Mwalimu Nyerere. Na kila mara alipowanyang’anya watu uhuru wao alijenga hoja juu ya kwa nini amefanya hivyo. Alifuta vyama huru vya wafanyakazi, akafuta vyama vya upinzani, akafuta ushirika, akawanyima watu fursa za kutajirika na kuwanyonya wenzao, akaminya uhuru na fursa za kuiba fedha za umma na kula rushwa, n.k. Lakini alijenga hoja ambazo waliozipinga waliishia tu kusema, “Ah! Hana lolote huyo, anataka tu kujiongezea madaraka.” Na baadae alikiri kuwa baadhi ya vitu alivyofanya vilikuwa na makosa ikiwemo kufuta ushirika.

Historia ya dunia inatufundisha kuwa binadamu amenyimwa uhuru kwa namna mbalimbali. Kuna wakati wanawake hawakutambulika kama binadamu. Hata walipotambulika hawakupewa fursa za kupiga kura, achilia mbali kugombea na kumiliki mali. Lakini baada ya ‘mapambano’ sasa dunia inakiri kuwa wanawake ni binadamu na wanapaswa kuamua hatma zao kwa namna mbalimbali ikiwemo kupiga kura na kugombea. Watu weusi vivyo hivyo. Lakini sasa dunia inatambua [hata kama ni kwa unafiki] kuwa nao ni binadamu. Masikini vivyo hivyo, lakini sasa japo wanaruhusiwa kupiga kura na kugombea, haijalishi kama wana uwezo wa kushinda.

Hoja niijengayo hapa ni kwamba waliowanyang’anya – na wanaotetea – Watanzania wenye chini ya miaka 40 fursa ya kugombea urais sharti wajenge hoja zenye mantiki na zenye kushawishi. Kwa nini ni 40 na si 39 ama 25? Ni katiba gani inayotaja umri wa kuanzia lakini haiweki kikomo? Kuna vigezo gani vya kisayansi, kihistoria ama kimantiki vinavyoweza kuthibitisha kuwa mtu mwenye miaka 40 atafaa zaidi kuwa Rais kuliko mwenye 37 au 29?

Ukizipitia kwa umakini hoja za wapingao umri kupunguzwa utagundua namna zilivyojaa chembechembe za uhafidhina. Kwanza wapo wasemao chini ya miaka 40, mtu anakuwa bado ni mchanga, kijana, n.k. Lakini hawatuambii kama mtu akifikisha 40 ndio anakuwa amekua na kukomaa. Wala hawaikemei Katiba kutoweka kikomo, kiasi kwamba hata ‘kikongwe’ mwenye miaka 120 ana haki ya kugombea urais, lakini si ‘kichanga’ mwenye miaka 39.

Wapo wanaotumia jina la Mwalimu kuthibitisha ‘uharamu’ wa hoja zao. Kuna mtu alitolea mfano wa mwaka 1995, Mwalimu alipomwambia mmoja wa wagombea wa urais kupitia CCM, kuwa, ‘Wewe bado ni mdogo. Subiri kwanza ukue’. Lakini mtu huyo [tumwite ‘Bwana Mdogo’] alikuwa na miaka 45 wakati huo. Mwalimu mwenyewe hakuzuiliwa kugombea urais wa TAA na baadae TANU na kuongoza harakati za ukombozi licha ya udogo wake kiumri. Nijuavyo mimi, sina hakika kama Mwalimu angebadili mawazo yake, iwapo angekuwa hai, mwaka 2005 pale ‘Bwana Mdogo’ alipojitokeza tena, akiwa na uzoefu mkubwa zaidi na umri wa miaka 55. Angalau karibu nizungumzaye nae ananiambia udogo na uchanga wa ‘Bwana Mdogo’ huyo si wa umri, ni wa uwezo.
Lakini Mwalimu alimshabikia mgombea fulani, ambae alikuwa ni mwanafunzi wake na baadae kafanya nae kazi kwa ukaribu, akimpa nafasi mbalimbali ikiwemo ile nyeti kwa wakati huo, ya uwaziri wa mambo ya nje [tumwite ‘Bwana Msafi’]. Kuna ushahidi wa wazi kuwa kati ya watu waliomsoma na kuonekana kumshiba Mwalimu ni huyo ‘Bwana Msafi’. Sote tumeshuhudia alikoipeleka nchi na jinsi alivyogeuza nchi shamba la bibi: kila aliyehitaji kujifunza kuiba kwa namna mbalimbali, ikiwemo wizi uliohalalishwa kisheria [ubinafsishaji na uwekezaji] na ule ulioharamishwa kisheria [EPA, Radar, Kiwira], alipata fursa katika kipindi cha ‘Bwana Msafi’. Ni katika kipindi hicho pia tulipojifunza kuwa Ikulu ni mahali pazuri na kuanzishia biashara, kuombea mikopo, kujiuzia bure migodi na ardhi na kumfungulia bibie kaserikali kake ka pembeni – ‘kaenijioo’.
Lakini ‘Bwana Msafi’ na ‘Bwana Mdogo’ wote ni watu waliolelewa katika Chama, tena angalau wakati ule ambapo Chama kiliwajali na kuwasikiliza wanyonge wake. Wote ni watu walioingia madarakani wakiwa na zaidi ya miaka 50! Wote ni watu waliopata fursa ya kufanya kazi, kuzungumza, kucheka, kula, kushikana mikono na kukumbatiwa na Mwalimu; baadae wakamwona alivyougua na kufariki, hatimaye akazikwa. Kwa maana hiyo, wanajua kabisa kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu wa kawaida [aliyezaliwa, akakua, akazeeka, akaugua, akafariki] na si malaika aliyeshushwa toka mbinguni. Hivyo, historia inatuthibitishia kuwa hoja ya ukubwa wa umri, uzoefu na kulelewa katika Chama haina mashiko. Na je, kuna chama gani hapa Tanzania kiwaleacho, kwa nadharia na vitendo, watoto na vijana ili wawe viongozi baadae? Bado tunazungumzia suala la makuzi ya kichama hata katika zama hizi ambazo watu wanadai uhuru mpana wa kugombea urais na ubunge bila dhamana ya vyama?
Wanaotaka kuondolewa kwa vikwazo vya umri wanatutaka tusome historia ya Afrika, toka DRC hata Libya: Je, Ghadafi aliingia maradakani na miaka mingapi? Tazama jinsi alivyoibadili nchi ile akiwa kijana mdogo tu mwenye umri wa miaka ishirini na ushee. Lakini Ji-Ghadafi zee lilikuwa tayari limeanza kulewa madaraka na kuurejesha mfumo wa kifalme lililoupindua. Wapo wanaotutaka kulinganisha hawa wafuatao na kusema yupi alikuwa bora zaidi, kama tunafuatilia historia zao: Komredi Yoweri K. Museveni wa miaka ya 70 na Mhe. Dk. Yoweri K. Museveni wa miaka ya 2000.

Lakini mjadala huu una hatari kubwa sana kama wanavyodai wanaopinga namna hoja ya akina Zitto inavyopenyezwa. Ni mjadala unaogusa hisia na kujaribu kuwafanya vijana wajione wao ni kundi moja, kundi linalounganishwa na umri. Ni kipi kimfanyacho kijana mlalahoi wa Nyamitwebili ajione kuwa yeye si sawa na walalahoi wenzake wenye umri wa zaidi ya miaka 40, eti kisa ni wazee? Halafu ajione yuko sawa na Januari na Zitto, eti kisa ni vijana?

Ukweli ni kwamba vijana waliobebea hoja hii hawaishi maisha ya vijana wa mtaani, wala hawayasikii machungu yao, zaidi tu ya kubeba hisia zao. Kwangu mimi, sidhani kama ni sahihi kutumia kigezo cha umri kutengeneza kundi. Kijana mwenye umri wa Zitto Kabwe au Januari Makamba ana kipi kinachofanana nao? Januari ana chimbuko la tabaka la walala-heri. Mahali alikosomea, maisha aliyoishi na fursa alizopata zinadhihirisha wazi jinsi tabaka la walala-heri linavyoweza kujizalisha na kujiimarisha kwa namna mbalimbali. Nitaeleza.

Tuchukulie mfano wa Zitto, ambae ana chimbuko la familia ya kilala-hoi, lakini sasa, kwa sababu ya elimu na nafasi yake, alishaliaga tabaka hilo. Ana utangamano upi na yule kijana waliyemaliza wote darasa la saba, ambae sasa ni mvuvi wa kutumia mtumbwi? Je, wakikutana wana kipi kinachofanana? Nadhani wanatofautiana kila kitu: namna na idadi ya lugha wanazozungumza, nchi walizotembelea, aina ya vyakula walavyo, mavazi wavaayo, nyumba waishizo, n.k. Hata ndoto waotazo na mawazo wawazayo ni tofauti. Wakati mmoja akiwaza juu ya jinsi atakavyomalizia shahada yake ya uzamivu huko Uropa, [...], safari yake nje ya nchi na Rais, [...]; mwingine anawaza juu ya nyavu zake zilizokamatwa na kuchomwa moto na Magufuli (wakati huo), mtumbwi wake uliotoboka, nyumba yake ya tope na nyasi inayokaribia kuanguka, kijishamba chake alichoporwa kupisha mwekezaji-papa au mtoto wake aliyefukuzwa shule kwa kukosa ada ya elfu kumi. Hawatangamani kamwe. Mmoja akiugua kichwa analazwa wodi ya ‘very important person (V.I.P.)’ na kesho yake kupelekwa nje kwa matibabu zaidi; mwingine huishia katika kijituo cha afya cha akina ‘poor innocent victim (P.I.V.)’ ambacho hakina hata ‘panadol’. Hakuna utangamano. Mmoja akijisikia kuchoka anaweza kuamua kupanda ndege kwenda Afrika Kusini kwa mapumziko, mwingine ataishia chini ya mwembe kusinzia.

Ipo hoja ya pili, vijana hawa wana ndoto za kuwania urais. Angalau Januari amekwisha sema kuwa, kwanza hana ndoto hiyo, na pili, hata angekuwa nayo, mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 41. Hivyo, kama hiyo ndiyo ingekuwa nia yake, basi asingekuwa na haja ya kuanzisha mjadala huu. Lakini si ajabu kusikia watu wakikana ama kusema hawagombei lakini baadae wakagombea kwa sababu wananchi au wazee ‘wamewalilia’. Zitto, alikwishanukuliwa zamani kuwa angegombea urais ifikapo 2015. Alipoulizwa itakuwaje, wakati utakuwa na umri ‘mdogo’ wa miaka 39 alijibu kuwa anategemea katiba itakuwa imebadilishwa na kuondoa kikwazo hicho.

Mdogo wake Januari aitwae Thuwain, aliwahi kuandika waraka [upo kwenye mtandao] akiwalaani Watanzania kwa kumdharau Rais Kikwete na kumtupia lawama kila kukicha. Alimsifu Rais kuwa ni kiongozi shupavu na amefanya maendeleo mengi, ambayo aliyashuhudia kwa siku 90 tu alizokaa hapa nchini kwa kipindi chote cha awamu ya kwanza ya Rais Kikwete (2005 - 2010). Na akawapa Watanzania dawa ya matatizo yao: chanzo cha matatizo yao ni kizazi kilichozaliwa kabla ya uhuru. Hivyo, suluhisho pekee ni kuhakikisha kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2015, mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya 1961 asipate nafasi yoyote ya uongozi. Kijana aliyekaa nchini kwa siku 90 katika kipindi cha miaka mitano, kipindi ambacho baba yake na kaka yake walikuwa wateule wa Rais, angewezaje kuona ubovu wa utawala uliopo, achilia mbali kufahamu machungu ya walalahoi hadi kuwapa suluhisho?

Hoja hii ya Thuwain ndiyo inayopenyezwa na akina Zitto na Januari katika mjadala. Wala haikuanza leo. Januari alianza kuipenyeza hoja hiyo hata kabla ya 2010. Zitto pia. Wanadai kuwa sasa ni wakati wa vijana. Wazee ndiyo chanzo cha matatizo, waiachie nchi kwa vijana. Ndani ya UVCCM pia wapo vijana, akina Salum, wamebeba bango hilo: Rais awateue wao vijana kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, na Chama kiwateue kuwa makatibu wa wilaya na mikoa kwa sababu wazee wameshindwa!

Kwa namna yoyote kinachopandikizwa hapa ni sumu ya ubaguzi – ubaguzi wa umri. Katika mfumo wa kandamizi na wa kinyonyaji tulionao, uliowafanya watu kupoteza matumaini, ni rahisi sana kupandikiza sumu ya aina hiyo na ikafanya kazi. Kama hoja ya leo ni umri, kesho itakuwa ni dini. Tuna hoja gani ya kumjibu atakayetushawishi kuwa nchi hii imetawaliwa na wakatoliki wawili na waislam wawili katika kipindi cha miaka 50 na hakujawahi kuwa matumaini? Kisha akituambia kuwa chanzo cha matatizo yetu ni hizo dini mbili, na kwamba ni wakati sasa wa kuwajaribu waprotestanti au wapagani, tutakataa? Akija mwingine akatuambia chanzo ni makabila yaliyotawala na kwamba sasa ni wakati wa kuwajaribu wahaya, wasukuma, wanyakyusa au wachagga tutakataa? Na, je atakayetuambia chanzo ni kutawaliwa na watu wasio na Phd za darasani? Na, vipi atakayesema kuwa chanzo ni kuwa marais wote walikuwa wanaume, na kwamba sasa ni wakati wa kumjaribu mwanamke?

Mjadala ulioasisiwa na Zitto na Januari una lengo la kununua hisia za wanyonge na kuwafanya wasihoji chanzo cha ufukara wao na kudadisi sababu za utajiri wa wenzao; waendelee kutawaliwa na kunyonywa na kijitabaka kilekile ambacho kinazidi kujizalisha; na wasiweze kujenga umoja ili kukipindua kijitabaka hicho kinachokumbatia mfumo kandamizi wa uliberali mambo-leo.

Kama nilivyosema, binafsi sipingi kuondolewa kwa vikwazo vya watu kugombea nafasi za kisiasa vikiwemo vigezo vya vyama na umri. Lakini si uhaini kuasisi mjadala wa aina yoyote ule kwani sasa ndio wakati wake hasa. Tunaojiita ‘watetezi’ wa maslahi ya wanyonge tunapaswa kuonyesha sura halisi za mijadala hiyo, na kuitetea au kuipinga kwa hoja!

Sabatho Nyamsenda,
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

CHANZO:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP