Loading...

Thursday, March 8, 2012

taifa limegawanyika kuhusu mgomo wa madaktari?


"Sio haki kwa madaktari kumuamuru Raisi wetu wa nchi kutoa maamuzi kutokana na matakwa yao. LAKINI Dr Mponda na mama Nkya wenyewe kwa utashi wao wenyewe lazima wafanye maamuzi magumu kwenya jambo hili. Raisi mtaafu Mwinyi alifanya maamuzi magumu bila kushurutishwa na mtu yeyote. Lazima wafuate mfano. Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi" - Nickson Ngajilo
---


"Huu ni uchumi wa soko huria na madaktari ni bidhaa adimu; ukiwafukuza vile wamesema tu fukuza mawaziri wawili, vile eti wewe ni mkuu wa kampuni huwezi kushinikizwa; na huku wao ni bidhaa adimu kokote watakapokwenda watapata soko...Hivi kweli tangu Januari madaktari wanasema mawaziri wale wawili waondoke watu bado mnanunua propaganda eti madaktari wamempa saa 72 Rais? Hivi kweli Rais heshima na hadhi yake ya Urais itatetereka na kupotea vile ametangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kunusuru wananchi wake wasife? Eti madaktari walikula viapo wasiwaache wagonjwa wafe bila kuwasaidia hivyo waache mgomo, je, Rais kwa nini naye asiambiwe kuwa alikula kiapo kutokuacha wananchi wafe na hivyo awawajibishe mawaziri wale wawili ili kuonesha nia ya kuwasikiliza hawa madaktari adimu badala ya kuwasikiliza washauri wanaosema Rais ajali zaidi eti hadhi na heshima yake badala ya kujinyenyekeza kwa madaktari ili wananchi wake wasife? Hivi kweli serikali inadhani wananchi walio wengi watashawishiwa wawachukie madaktari badala ya kuichukia serikali yenyewe inayoonekana kufanya propaganda na kuchezea shere madaktari kwa kauli zinazokanganya za Waziri Mkuu? Tusubiri tuone" - Azaveli Lwaitama
---


"Mara ngapi madaktari hawa hawa wanashindwa kutuhudumia kwa sababu ya kufanya kazi zao binafsi na Serikali hii hii imeacha kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria leo hii eti wanataka wengine wajiuzulu. Kama wao wenyewe ni wazembe wanapaswa kujirekebisha ili wakati wakinyooshea wengine vidole wao wabaki wasafi bila ya hivyo utabaki unafiki tu na kujikosha. Lazima tuangalie pande zote siyo Serikali kuonekana haitekelezi madai ya wananchi kumbe wananchi na wenyewe wana matatizo ambayo walipaswa kuyarekebisha kwanza" - Bariki Mwasaga
---

"Kweli kabisa, hawa wanaoitetea serikali kwenye mgomo huu watueleze, Dk Nkya na Dk Mponda wanaolindwa na serikali ni bora kuliko maelfu ya wagonjwa wanaoteseka hospitalini? Mgomo huu wa madaktari umeonyesha sura halisi ya kushindwa kwa utawala wa JK. JK huyu aliyeingia kwa kishindo mwaka 2005 kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Leo anakimbia matatizo na kumwachia Pinda ambaye hana mamlaka ya kumwajibisha mtu, kazi yake ni kuongea tu. Namsikitikia sana. Hiki ndicho kipimo cha urais, ni vema sasa JK ajitokeze ashughulikie matatizo haya mwenyewe. Mbona 2010 alipambana mwenyewe na Tucta?" - Elias Msuya
---


"Madaktari, manesi, polisi, watu wa fire, na waongoza ndege ni watu wanaotakiwa kugoma baada ya njia zote zimekwisha na wagome kwa utaratibu usiohatarisha maisha ya binadamu wenzao. Hawa waligoma kwa hasira za kujibiwa hovyo na watendaji wa wizara. Serikali nina hakika wangeweza kushinikizwa kupitia wabunge wakasikilizwa na kama nilivyosema hapo awali, wakagoma kuhudumia mfano wagonjwa wa nje, au walio na nafuu progressively wakifanya mazungumzo!" - Tony PT
---


"Nitaendelea kuunga mkono kwa sababu huu mgomo upo ili kuboresha si tu maslahi ya madaktari bali mazingira ya matibabu ya wagonjwa na sisi tukiwa miongoni. Tanzania mazingira ya matibabu imekuwa ni kero kubwa na sisi ni mashuhuda wa hospitali zetu kama Mwananyamala, Ilala n.k. Wagonjwa wanalala chini au watatu kitandani, ukitembelea sehemu za huduma ya mama na mtoto utashangaa! Idadi kubwa ya wagonjwa wanaokufa kutokana na haya mazingira ni kubwa lakini Serikali haioni. Uchaguzi wa Igunga umetumia pesa kubwa ambayo kama ingepelekwa Mwananyamala wote tungeliona mabadiliko. Hivyo hivyo itakayopelekwa Arumeru sote tutajua ni kwanini madaktari wanagoma! Elimu waliyoipata madaktari imewafanya wasiwe wanafiki na hivyo kugoma kweli kweli tofauti na walimu ambao wako katika mgomo baridi wa miaka mingi na madhara yake tunayaona katika matokeo ya mashule ya Serikali ya hivi karibuni. Naogopa madhara yatakayotokea kama madaktari pia wataamua kuingia katika mgomo kama huu. Najua wanasiasa wanafurahi kuona madaktari wakiwa ofisini hata kama hawafanyi kazi yao ipasavyo kama ilivyo kwa walimu, lakini ni vema wakagoma waziwazi ili wakirudi makazini wafanye kazi. Taifa letu linakuwa masikini kwasababu Serikali yetu imewatupa mkono wasomi na kuwalaki wanasiasa. Sishangai kuona wasomi na madaktari bingwa wakipigana vikumbo katika kura za maoni. Hivi ndivyo taifa letu limeamua tuishi na ndiyo maana taasisi zote za utafiti zimekufa. Taifa linaloendeshwa bila taasisi za utafiti ni sawa na taifa mfu" - Jones Nyakwana
---


"Kuwaondoa mawaziri hakutaleta mishahara bora maana matatizo haya ni ya kimfumo yapo tangu mwaka 1992 wakati wa Mzee Mwinyi. Katika utendaji huwezi kumpa mkuu wa nchi shinikizo tena la masaa 72 la kufukuza wateule wake au la mnagoma. Bahati sana kwamba wanaweza kufanya hivyo na bado wakasikilizwa. Kimsingi tunakubaliana na madai yao lakini njia wanayotumia ni ya kinyama" - Richard Mgamba
---

"Kinachonishangaza ni jinsi watu walivyo na mshipa wa kujadili vitu ambavyo inaelekea wazi kwamba hata hawajaviangalia kwa karibu, ikiwemo matamko ya madaktari na hata serikali. Ni dalili kwamba hili taifa letu linaumwa; tena linaumwa kweli..


"Ukitaka kupata jawabu la jambo gumu, anza na kupekua ukweli uliopo kabla ya kuchambua chochote. Mfano rahisi: Madaktari hawakusema kwamba hawawapendi waziri na naibu wake, bali walisema kwamba hawa ni kikwazo cha kufikia muafaka na hivyo majadiliano hayawezi kufanyika na watu hawa wakiwa kwenye nafasi zao. Kama mtu hulielewi hili, basi waulize ili wakueleze lakini usiwalaumu hata kwa ambacho hawakukisema.


"Hali kadhalika, WM Pinda hakuwafukuza akina Mtasigwa na Nyoni bali aliwasimamisha. Na pia hakufanya hivyo ili kuitikia mwito wa madaktari bali kutokana na orodha ya tuhuma ambazo zinafanyiwa uchunguzi hivi sasa. Kwa hiyo tusiseme tu kirahisi kwamba aliwafukuza kutimiza masharti ya madaktari. Tuangalie matatizo yaliyopo wizarani pale, ni zaidi ya hivi wanavyolalamikia madaktari. Ile wizara ina matatizo na ndiyo msingi wa madaktari kufikishana hapa na serikali. Chunguzeni.


"Lakini pia, kudai kuwa eti madaktari wana akili za kitoto huenda ni dalili kwamba huelewi hata kinaendelea nini. Januari na Februari ilifikia mahali mpaka madaktari mabingwa nao wakagoma ingawa ngoma nzima ilianzia na wale waliokuwa mazoezini. Sasa naomba watu mjifunze kuna ngazi ngapi za udaktari kuanzia na pale kwenye Internship hadi kuwa bingwa. Mkishaelewa hiyo, ndiyo mjiulize iwapo kuna tatizo la ujana au utoto hapo.


"Ndiyo, kugoma kutibu wagonjwa ni jambo baya lakini waziri na naibu wake kugoma kuachia ngazi katika mazingira haya ni jambo baya zaidi. Madai ya madaktari yanahusu pia maslahi ya wagonjwa kama mmesoma vema. Ni madai ya maslahi ya taifa. Hawa si watoto wadogo au watu wajinga. Kwa watu ambao hamjawahi kujishughulisha na kufuatilia matatizo ya sekta ya afya nchini ama shida za madaktari na wahudumu wengine wa sekta hii, naomba mchunguze kwanza. Mwaka 2001 nilifanya kazi hii hadi kushinda tuzo ya uandishi na nilichogundua kilinishangaza.


"Hii ni moja ya sekta zinazodharauliwa kupita kiasi nchini na ili mambo yabadilike ni lazima zitumie hatua zisizokuwa za kawaida. Tanzania hivi leo imo katika orodha ya nchi taabani 20 duniani kwenye sekta ya afya na hali inazidi kutisha. Ilifikia mahali mpaka G8 waliamua kwamba wazisaidie baadhi yake ikiwemo Tanzania. Niliwahi kuhudhuria mkutano wa Waziri wa Afya wa Tanzania (siyo huyu Mponda), pale New York alipokutana na wawekezaji wa sekta ya afya, na nilipigwa na butwaa. Someni taarifa za vyombo kama WHO, UNICEF, miradi kama MDG, mashirika kama USAID, na NGO kama Save the Children, mtaona jinsi nchi yetu ilivyo hohe hahe.


"Hivi leo Tanzania ina wafanyakazi wachache zaidi wa sekta ya afya kuliko ilivyokuwa mwaka 1985 licha ya kuwa idadi ya watu imeongezeka karibu mara mbili. Tatizo liko wapi? Ndiyo maana wale madaktari walipoagana na WM Pinda ile Feb 9 walisema kwamba watakutana Machi 3 kufanya tathmini kwa sababu wanaijua serikali yetu. Siyo hii ya sasa tu, zote ziko hivyo. Wanajua wanachokifanya; tusiwadharau ingawa kweli kabisa kugoma kutibu wagonjwa ni hatua ngumu sana."Tusitumie akili zilizochakaa kuchambua matatizo makubwa yaliyokomaa. Hivi inaingia akilini kwamba daktari alipwe posho ya siku nzima ya masaa 24 ya sh. 10,000 anapokuwa wodini lakini mbunge alipwe sh. 70,000 kwa masaa yasiyofikia 12 (halafu adai zaidi) na mtumishi wa serikali alipwe sh. 80,000 akisafiri? Jamani haya mataifa yaliyoendelea hayakufikia hapa yalipo kwa akili hizi mbovu mbovu hivi.

...Kwa wasiojua hali yetu ya sekta ya afya..........Angalia picha ya kwanza iliyomliza Naomi Campbell - Hospitali ya Temeke. Hawa akina mama wamekosa kwa Mola? Hawa watoto wamekosa nini kwa Mungu? Halafu Watanzania mliosoma, watu wenye akili timamu, mnashindwa kuelewa vita iliyopo kati ya madaktari na serikali? Unataka kusema miaka yote hii serikali haijui kwamba kuna shida kwenye sekta ya afya? Mbona magari ya kifahari yamejaa kila kona? Mkuu wa Wilaya anapewa fungu la sh. milioni 10 kwa mwezi za kuchezea tu ofisini wakati hospitali zetu hazina bajeti za kutosha. Wabunge wanaziongelea fedha kama utani na wanadai zaidi lakini manesi wetu kwa mwezi wanalipwa pesa ambayo haitoshi hata kushonea suti moja ya waziri kama Mponda. ANGALIENI HIZI PICHA. Hawa akina mama wamelikosea nini taifa? Na kumbuka hawa wote wako mjini, je, vijijini hali ikoje? Madaktari wamefikia hapa baada ya serikali kufanya unyama na mzaha mkubwa kwa muda mrefu. Kumbukeni wakubwa wanatibiwa huko kunako huduma nzuri. Hawataki kabisa kutibiwa Tanzania.


" Hawa ni watoto wa Watanzania wenzetu (Picha na SAVE THE CHILDREN).

" Hapa ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (Picha na New Hope Ministry).

" Hospitali zetu Tanzania. Hii ni Amana. (Picha na The Globe and Mail) "

- Mobhare Matinyi


---"Ushauri unaotoa wewe [Tony] ulishazingatiwa na walimu. Ndiyo, walisitisha mgomo, wakarudi shuleni, lakini hawafundishi. Umeona matokeo ya mitihani? Unadhani inatokea kwa bahati mbaya? Tujivune kwa kuwa walimu wanaihurumia, wanaisikiliza serikali, wanaingia darasani?


"Kama madaktari watasikiliza ushauri wako, watarudi kazini. Lakini nakuhakikishia, wagonjwa watakaokufa ni wengi zaidi.


"Wanachopigania sasa, si maslahi binafsi. Twende mbali zaidi. Wanapigania uhai wa wagonjwa wetu. Hicho wanachodai ndicho kitakachowezesha ufaniSi wa kazi yao, na kuokoa maisha ya wagonjwa wetu.


"Si haki kabisa, kutumia sensitivity ya taaluma yao kuwanyanyasa. Si haki kabisa kuitetea serikali inayo-frustrate madaktari wetu. Ni makosa makubwa kujiingiza kwenye biashara ya kutetea wenye mabavu dhidi ya wanyonge. Serikali inayokusanya kodi (kwa wagonjwa) ndiyo inayolazimika kuwaokoa.


"Kama kweli mna huruma na wagonjwa, ilazimisheni serikali itumie kodi zao kunusuru maisha yao. Hivi ni nani anajali maslahi yake binafsi, kati ya madaktari, rais, na mawaziri husika? Dk. Mponda, kwa mfano, ana faida gani kwa taifa kukalia cheo hicho wakati maisha ya wananchi yanateketea? Uwaziri wake leo unaokoa wagonjwa wangapi? Yaani cheo chake ni bora kuliko maisha ya madaktari na wagonjwa?


"Wagonjwa kama kweli tunajali uhai wa watu hawa, kwa nini tuone kwamba rais, waziri na naibu wao wana haki ya kufanya haya wanayofanya? Madaktari hawatangulizi maslahi badala ya uhai, bali wanataka wawezeshwe kuwa katika hali nzuri ya kuokoa uhai wetu.


...


"Naona wengine mnasema eti sasa kuna watu wameanza kuingiza siasa! Kwani siasa ni nini? Nani kakwambia kuwa mgogoro huu si wa kisiasa? Nani kakuambia kwamba sehemu ya ufumbuzi haipaswi kuwa ya kisiasa? Kwa hiyo, tukinyanyapaa siasa ndio ufumbuzi unapatikana? Na mbona hata huyo aliyehoji, amehoji kisiasa? Tuache utani jamani. Anayenyanyasa madakatari ndiye anaua wagonjwa" - Ansbert Ngurumo


---


"Usisahau ni katika hospitali ya Temeke hii hii wakati Mh. Lyatonga Mrema ni mbunge kupitia chama cha NCCR Mageuzi alikusanya misaada kutoka kwa watu mbali mbali ili kusaidia hospitali hii. Misaada ya kwanza mganga mkuu wa hospitali aliipokea. Alipokuja mara nyingine watu wote ikiwa ni pamoja na mganga mkuu wa hospitali walikimbia na kuziacha ofisi zimefungwa. Walipoulizwa na waandishi wa habari nakumbuka walisema wamepewa maelekezo kutoka juu wasipokee misaada ile. Baada ya miaka kadhaa Naomi Campbell anaikuta hospitali ile ile ikiwa iko taabani na katika hali ya kutisha. Masikini nchi yetu.


"Kijijini hali nako siyo nzuri. Kuna kijiji kimoja kwetu kule nilikuwa likizo mwaka 2010. Niliugua nikaenda kwenye zahanati ya kata. Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Ijumaa. Cha ajabu niliambiwa kwamba dawa hazipo huwa zinakuja Jumatano. Kwa hiyo nirudi Jumatano inayofuata. Nilibaki hoi" - Peter Lwegasira

---


Ndugu zangu wadau wa afya tuuangalie huu mgomo kwa jicho la tatu. Naomba msinielewe vibaya silazimishi watu au watumishi wa afya wasigome. Lengo la mgomo huu halikuwa Mawaziri kujiuzulu bali ni Maslahi ya watumishi wa afya, mazingira bora ya kazi na vifaa vya kutolea huduma.


Hicho kinachofanyika sasa ni hasira za watu kutokana na maisha mabovu yaani ndio inaonekana nafasi nzuri ya kuisulubisha serikali iliyoshindwa kutimiza wajibu wake kwa muda mrefu.
Mfumo wa serikali hii umeoza tangu zamani na kuna safari ndefu ya kubadilisha mfumo huo ikiwa ni pamoja na kubadilisha katiba na serikali iliyopo madarakani. Kwa sasa kuendelea kugoma na kusema mawaziri wajiuzulu sio jambo la busara hata kidogo, asipojiuzulu tunagoma na kusababisha vifo vya wananchi wasio na hatia ambao wana matatizo kama sisi wenyewe hatuwatendei haki wananchi hao. Hata kama mawaziri wakijiuzulu au wakifukuzwa na raisi hatuwezi kubadlisha hii nchi kutoka kwenye umasikini tulionao kwa haraka kama tunavyofikiri.


Jichukulie wewe unapewa uwaziri wa afya kwa sasa kwa mfumo huu wa serikali je utaweza kukamilisha matakwa ya madaktari na watumishi wa afya hawa? Lazima tukubaliane kwa sasa nchi ni maskini au kwa uzembe wetu au kwa kutojua au kwa tamaa za viongozi wetu. Tutumie busara, turudi kazini kuwahudumia wananchi wasio na hatia wanaopoteza maisha ambayo yangeweza kuokolewa. Tutafute njia mbadala na sahihi kutatua mgogoro huu. Mawaziri sio baba zangu wala mama zangu lakini wakijiuzulu sio mwarobaini wa tatizo letu.


Tukumbuke Mwl. alisema unaposomeshwa ni sawa na kupewa chakula chote kilichopo kijijini ili uchukue ule na upate nguvu ya kwenda nchi za mbali kwenye chakula cha kutosha na kuleta kijijini kwetu je sisi tunawarudishia nini wanakijiji waliotuchangia chakula chao?" - Mlingwa

---

"Tatizo sisi Wadanganyika wengi, kama ulivyosema [Matinyi] hatuutafiti ukweli, na pengine kutokana na kuendekeza wavivu na ubinafsi. Hatuendi kwenye hospitali za umma kuona wagonjwa kwa vile wagonjwa wetu hawatibiwi huko! Utajifunzaje bila kuona, bila wewe mwenyewe kuwa sehemu ya waathirika wa hali?


"Mimi nilimfuatilia mgonjwa mmoja aliyekuwa anasubiri kupata operesheni hapo Muhimbili na akawa anapigwa tarehe karibu mwaka si kwa sababu madaktari wa kumfanyia upasuaji walikuwa hawapo, la hasha, bali kwa vile tu vifaa vidogo vidogo vya kuwezesha operesheni ifanyike ikiwa ni pamoja na gauze inayoweza kutengenezwa kwa pamba inayozalishwa Tanzania havipo! Wanaweza kupangiwa operesheni watu watano kwa siku lakini kutokana na ukosefu wa vifaa vidogo vidogo tu, wakafanyiwa wawili au mmoja siku imekwisha, madaktari wanarudi nyumbani si kwa sababu wamemaliza kazi bali kwa sababu hakuna vitendea kazi!


"Niseme tu kwamba hata tukijidai tuna makengeza au kuziba masikio, au mafundi wa kuyumbisha ukweli kuwa uongo, ukweli utabaki pale pale-nchi yetu inayo matatizo makubwa katika hospitali za umma; matatizo ambayo watawala wetu wengi hawayafahamu kwa sababu wao na familia zao hawatibiwi huko.


"Tuseme tusemavyo, kama hatua hazitachukuliwa, badala yake tukatukana madaktari kwamba wana utoto, tutakuwa tunajidanganya wenyewe kama taifa, na tatizo litabaki pale pale na tena likizidi kukua na watakaoendelea kuumia zaidi ni sisi watawaliwa wa taifa hili, hasa wanawake na watoto wa familia maskini.


Je, wakifa maskini wengine tutaishi milele? Leo mama mmoja mwenye mtoto aliyelazwa pale Muhimbili baada ya kuona madaktari hawapiti wodini ameuliza “serikali ina mpango wa kupunguza watu?” Hawa wagonjwa wakimlilia Mungu kwa uchungu taifa linapata baraka?
0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP