Saturday, April 21, 2012

HITIMISHO lA HOTUBA YA SAHIHI 70!

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho. Tatizo kubwa la Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutokutekelezwa ni ukosefu wa uwajibikaji; na kama nchi hii tunataka tuendelee, kama tunataka tupigane kwa dhati kabisa dhidi ya ubadhirifu, dhidi ya udokozi, dhidi ya uzembe, dhidi ya uvivu ni kuhakikisha tuna misingi sahihi ya uwajibikaji. Accountability, niliwahi kuwaambia vijana fulani kwamba kama kutakuwa kuna neno moja linalotakiwa liandikwe kwenye Katiba mpya, neno moja; ni ‘accountability,’ uwajibikaji na ndicho kinachokosekana. Taarifa hizi zinatolewa kila mwaka, nashukuru sana safari hii Wabunge mmekuwa wakali sana. Lakini bila kuhakikisha Executive inawajibika katika haya mwaka kesho tutarudia haya haya na tutakuwa wakali hivi hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,  napenda kutoa taarifa kwamba; mimi na Bunge hili halina mamlaka ya Mkurugenzi wa Shirika, Katibu Mkuu wa Wizara au Mkurugenzi wa Halmashauri. Mawaziri ambao wametajwa kwa njia moja au nyingine kutokuwajibika ipasavyo na kuliingizia hasara taifa wamekuwa wagumu sana kuwajibika, wanampa kazi Rais ya kuwafukuza.

Lakini sisi hatuwezi kuwaazimia hapa ila sisi tuna mamlaka na mtu mmoja tu humu ndani ya Bunge; na naomba mnisikilize kwa makini sana. Tuna mamlaka na mtu mmoja tu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa Mawaziri waliotajwa hawatatoka na wasipotoka madudu haya yatarudia. Kwa hiyo Mbunge yoyote mwenye uchungu na ubadhirifu, Mbunge yoyote ambaye anakereka na watoto kwenye Jimbo lake kukaa chini, Mbunge yoyote anayekereka na madawa kuharibiwa na MSD na MSD kushindwa kupeleka madawa kwenye vijiji vyetu, nampa taarifa kwamba kuanzia kesho tunakusanya sahihi za Wabunge 70, ili siku ya Jumatatu tutoe hoja hapa Bungeni ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.  (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kipindi hiki tunakitoa Mawaziri wote ambao wapo implicated kwenye taarifa hizi waweze kuona ama wao, au wamtoe rehani Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wabunge wote wenye uchungu kuanzia kesho tutakuwa pale mlangoni, sahihi zinazohitajika ni 70 tu, kwa ajili ya kuleta hapa Bungeni na Wabunge wanahitajika kupitisha hilo azimio ni nusu tu ya Wabunge, 50 plus one. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewapa heshima wananchi wetu, wataona kweli tumewatendea haki badala ya kupiga kelele bila ya kuchukua action. (Makofi)

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP