Tuesday, May 22, 2012

Ihefu hadi Ikwiriri: Majuto ni Mjukuu?

TUTASHUGHULIKIA MATOKEO TU HADI LINI?


Sijasoma yote yaliyoandikwa katika mjadala huu wa Wanabidii lakini nina
 machache ya kuchangia kuhusu suala la Ikwiriri kwa kuwa ni eneo ambalo
 nimekuwa nikifanya kazi za utafiti kwa muda mrefu sasa.Takriban miaka mitano mpaka kumi iliyopita hakukuwa na mfugaji wa
ng'ombe hata mmoja. Wengi wa wafugaji ni wa kabila la wasukuma ambao
 wamehamia toka Ihefu. Tukumbuke serikali iliwafukuza/kuwahamisha Ihefu 
kinyume cha taratibu na kuwanyang'anya mifugo baadhi yao waliochelewa 
kuondoka. Walitakiwa kwenda maeneo tengefu ya Lindi na Mtwara na kwingineko. Maeneo tengefu mengi hayafai kwa ufugaji kwani hayakutengwa kwa kuzingatia mahitaji ya wafugaji: maji, malisho na
huduma za kijamii. Hivyo wafugaji wamelazimika kubuni mbinu zao za
kuweza ku-survive in the absence of effective structural,
infrastructural and institutional support systems from the State.
Hali ikoje:
 Kwa kuwa hakuna kanuni nzuri za kuhakikisha kuishi kwa pamoja baina ya 
wakulima na wafugaji na kwa kuwa shughuli zao haziendani, kwa maana ya
 kwamba wanyama wa wafugaji wanaharibu mazao ya wakulima, hitilafu
 zilipotokea, wananchi (wakulima na wafugaji) walikimbilia ofisi za
 serikali za vijiji na polisi kuweza kupata usuluhishi. Kesi 
ziliongezeka mno. Polisi wetu na viongozi wetu wa vijiji, kata, tarafa
 na wilaya tunafahamu kuwa hawalipwi vizuri na serikali. Wafugaji ambao 
huwa wana uwezo bora kimaisha na kifedha kuliko wakulima katika maeneo ya 
Ikwiriri walianzisha mchezo mchafu wa kuhonga polisi na kuwabambikia
 kesi wakulima kuwa wao ndio wavurugao amani.
Nina mifano kadhaa kutoka kwa wananchi wengi niliopata kuongea nao.
 Mfano: Mzee XX amekuta mifugo shambani kwake na kuanza kujibizana na
 mfugaji YY kufikia hatua ya kutaka kupigana. Mkulima XX anatamka kuwa
 ni lazima suala hili alifikishe kunakohusika. Mfugaji YY anachukua
 pikipiki na kuwahi Ikwiriri police post. Mkulima XX anafika polisi,
anakamatwa kuwa ametishia uhai wa Mfugaji YY na mifugo yake. Anawekwa
 ndani kwa muda ambao polisi wameamua wenyewe.
Nikitumia taarifa halisi ambazo si rasmi kwa kuwa hazijatolewa na
vyombo vya usalama (polisi) lakini nimezipata toka kwa jamaa zangu
waishio Ikwiriri:Mapigano ya juzi ni kilele cha ugomvi ambao umekuwa ukiendelea kwa
 miaka kadhaa sasa na wakulima ndio wamekuwa waathirika wakubwa. Huyu
 Mzee alieuawa Ijumaa aliwahi kutoa taarifa kuhusu wafugaji kuingiza
 mifugo shambani kwake mwaka jana. Alikamatwa na kuwekwa ndani. 
Alipotoka aliendelea kudai haki yake kwa kwenda mahakamani. Alishinda 
kesi mahakamani na mfugaji mhusika alitakiwa kuondosha mifugo yake 
mara moja. Lakini hakufanya hivyo kwa kuwa mahakama si yenye kusimamia 
migogoro ya wakulima na wafugaji on a daily basis but ni polisi, hivyo
 mfugaji aliendelea kuhonga polisi.
Siku ya tukio, mkulima mzee wa miaka 60 alikuta mifugo shambani kwake
 na kuanza kujibizana na wenye mifugo. Wafugaji walipiga kelele na 
kuchukua marungu, mapanga na silaha nyinginezo wakampiga mpaka kumuua 
yule mzee. Ina lillah wa in illaih rajiun! Wananchi wakaenda kutoa
 taarifa polisi Ikwiriri. Kwa mujibu wa wananchi, hawakupendezwa na
 namna polisi walivyolishughulikia suala hili. Waliona kuwa polisi
 wamechukulia kana kwamba kimekufa kiji-mnyama tu kidogodogo na si
 binadamu tena wa miaka 60 ambaye alishinda kesi mahakamani kuhusu
 mgogoro uliopelekea mauti yake. Wananchi wakulima wakasema "enough is
enough".
Wakazifunga barabara za kutoka Lindi na Dar na kuanza kushambuliana na 
wafugaji. Kwa kuwa wafugaji waliompiga na kumuua yule mzee ni wa
kabila la kisukuma, wakulima walilenga kuwashambulia wasukuma
 irrespective ya kuwa ni wafugaji ama la. Maduka, magari, nyumba na
 mali nyinginezo zinazomilikiwa na wasukuma zimechomwa moto. Polisi
 mmoja wa kabila la kisukuma amechomewa nyumba yake kubwa yenye
 wapangaji kadhaa kwani wananchi walimtuhumu kuwa huwa anawasaidia
 wasukuma wenzake.Wakulima wa Ikwiriri nilioongea nao kwa simu wanahoji kwamba: kwa nini
 vyombo vya habari na jeshi la polisi wametoa takwimu za wafugaji
 waliojeruhiwa na kuharibiwa mali zao lakini hawajasema kuhusu WANANCHI
 WAKULIMA WA KABILA LA WANDENGEREKO WAWILI WALIOUAWA KWA RISASI NA MFUGAJI
 WA KABILA LA KISUKUMA SIKU YA MACHAFUKO? Kwao wao, wanadai kuwa hii
 bado inalenga kumkandamiza mkulima hasa wa kabila la kindengereko (nimetaja makabila kwa kuwa wao walioniambia wamesisitiza katika maandiko
 nifanye hivyo ili ichangie kuonesha ukandamizaji wa kabila la
 wandengereko. Mimi si mndengereko wa silazimishwi kufanya wanavyotaka
 wao, bali nimeona nifanye hivi kujibu hoja ya mmoja wa wachangiaji
 aliyehoji kwa nini ukabila umekuwa "issue" katika suala hili.)
Sasa hivi hali bado ni mbaya kwani Wandengereko wamedai hawawezi
kuendelea kuishi kwa kuonewa na wasukuma, hivyo wasukuma waondoke. Hii 
ndio hali halisi kwa vyanzo nilivyoweza kuvifikia mimi.
Maswali ambayo yameulizwa kuwa
 wafugaji waende wapi na ni nani mwenye haki zaidi ya ardhi, mkulima au 
mfugaji? Majibu yangu ni kama ifuatavyo:


Serikali ilipaswa itambue mahitaji ya wafugaji kama vile kutenga
maeneo yenye malisho na maji ya kutosha na kuweka miundombinu ya
kukidhi mahitaji hayo. Namna ambavyo serikali inaachia suala hili liwe baina ya 
wakulima na wafugaji ndicho chanzo kikubwa cha migogoro. Vijiji vingi 
vya Ikwiriri, Lindi na Mtwara vimeshurutishwa na serikali kutengeneza 
mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwemo kutenga maeneo ya wafugaji.
 Wananchi hawa hawana uzoefu na ufugaji na hivyo hawajui mahitaji
 maalum ya wafugaji. Kwa mfano, katika Kijiji cha Mavuji wilayani Kilwa,
 wananchi wametenga eneo la malisho ambalo liko milimani ambao mifugo
 haiwezi kutembea kwa urahisi. Mipango hii ya matumizi bora ya ardhi
 imetengenezwa bila ushiriki wa wafugaji kwa kuwa hakukuwa na wafugaji
 katika vijiji husika. Halmashauri za Wilaya husika zilikuwa na jukumu la
kuhakikisha kuwa mipango ya matumizi ya ardhi iliyotengenezwa imekidhi
 vigezo vya kitaalam ili kuepusha migogoro kama hii tunayoiona sasa.
 Kwa hali ilivyo sasa, tutegemee migogoro mingi kama hii kuibuka.Tutaendelea kushughulikia matokeo mpaka lini ilihali vyanzo twavijua?


Mwandishi: Baruani Mshale

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP