Sunday, May 13, 2012

Toa Kitabu Kisomwe-Utata wa Uhuru wa Kifikra

``TOA KITABU KISOMWE``-Utata wa `Uhuru wa Kifikra`

Hii ni kampeni ya msingi sana. Kusoma ndio msingi wa kupata maarifa na kukua kifikra.Ni wazi kua upatikanaji wa vitabu ni hatua ya msingi sana katika mchakato wa kutoa elimu ambayo ndiyo humuwezesha mtu kupata maarifa na kukua kifikra. Mbali na ukweli huu, taarifa hii ya Ndugu Mnyika(na hivyo kampeni hii kwa ujumla) imekosa kuangazia mambo kadhaa ya msingi.


La kwanza ni mahusiano kati ya kupatikana kwa vitabu na kusomwa kwa vitabu. Ingawa kampeni inasisitiza ``TOA KITABU KISOMWE`` haisemi ni kwa jinsi gani itahimiza, kushawishi na kusaidia kujenga tabia ya kusoma katika jamii husika. Ukosefu wa tabia ya kupenda kujisomea katika utamaduni wetu ni jambo linalolalamikiwa na wengi na lenye kuathiri uelewa na uwezo wa kifikra wa watanzania. Hili pia linaathiri ushindani wa watanzania katika Nyanja za kimataifa. Pale UDSM kuna maktaba kubwa tu na yenye vitabu vingi(vya kisasa?), lakini kuna wanafunzi wanamaliza mwaka bila kusoma hata kimoja. Hasomi kitabu labda aambiwe kitatumika kujibu mtihani. Hawa ni wanafunzi wetu wa elimu ya juu ambao, kwa kawaida, walitakiwa wawe ndio vinara katika kupenda na kusaka maarifa yaliyo katika vitabu (lakini wapi!). Hivyo kupatikana kwa vitabu hakumaanishi kusomwa kwake. Kupatikana kwa vitabu bila kuwa na mpango-mkakati wa kutatua tatizo la ukosefu wa tabia ya kujisomea kwa kiasi kikubwa vitaishia kwenye makabati na kuwa maficho ya mende, mazalia ya panya  na hifadhi ya vumbi.


Katika kuelezea lengo la hii kampeni ya ``TOA KITABU KISOMWE``, mwandishi Mnyika anaandika:


Neno `Uhuru wa kifikra` linarudiwa mara kadhaa na Mnyika ingawa bila ufafanuzi. Je, kumpa mtu elimu ni kumpa uhuru wa fikra au kumuongezea uwezo wa kufikiria? Kimsingi, na kwa mtizamo wangu, hakuna mtu asiye na uhuru wa kifikra. Ila hoja ni unafikiria nini? Je, unachofikiria ni cha manufaa na kinachoendana na muktadha hata kukidhi ushindani? Nani alishaweza kumpokonya mfungwa uhuru wa fikra? Kujaribu na hata kufanikiwa kwa mfungwa kutoroka ni ishara kuwa alinyimwa uhuru mwingine wowote ila sio wa kifikra. Hata wakati wa biashara ya utumwa, watumwa, watu ambao hawakuwa na elimu na walioonekana kutostaarabika walipinga kunyanyaswa kwa kujaribu na hata kufanikiwa kumuua mmiliki wao, familia yake au kujiua wenyewe. Walijaribu kutoroka pia. Hii ni ishara kuwa walipokonywa vyote isipokua `uhuru wa fikra`. Kwangu mimi, Uhuru wa Fikra ni haki ya kufikiria. Haki ambayo hauwezi kumpokonya mtu yeyote, kwa njia yeyote mbali na kumuua.
 
Niliwahi kuandika shairi kuelezea `Uhuru wa Kifikra`. Nililiita `Uhuru wa Mateka`. Nimeliweka hapa kwa ajili ya tafakuri. Nalo ni hili hapa:

Uhuru wa Mateka

Hawakupokwa vyote
Sikiza, hili ni tete
Sitaandikia mate
Simulizi naweka kidete

Uhuru wa mateka
Daima ni kunung`unika
Hupokwa maamuzi, inafahamika
Bahati, hubaki na fikra.Tutafika?

Waulize waliobwaga mioyo
Watasimulia, hawana choyo
Toka bagamoyo mpaka oyo
Waliimba, walilaani – ndiyo

Hata sasa-tunaimba, tunalaani
Loh! Hawatusikilizi asilani
Bahati, tunazo fikra kibindoni
Sisi sote tuingie mtaani

Tuingie  tukafanye fumanizi
Sikia kamaradi, fikra ndo wetu uzi
Tuukaze, tusilete makuzi
Amini tuu mateka-tunahitaji ukombozi

© Dastan Kweka

Hivyo kampeni hii inachanganya kati ya `Uhuru wa Kifikra` na wigo wa kufikiria. Mbali na hayo,nampongeza mbunge kwa kuja na huu mpango. Hizi ni changamoto katika kumkumbusha pale ambapo ama hakupaona au alipitiwa. Sote tunataka Tanzania iliyo bora.
---------------------

asante Dan kwa hoja nzuri na kwa utenzi wako, asante Mh. Mnyika kwa fikra zinazotekelezwa kwa vitendo, asante Dalali kwa kutujuza... ninachoweza kushauri ni kuwa kusambaza vitabu yafaa kuendane na mfumo wa kuvitumia kwa pamoja na mchakato wa kushawishi usomwaji wavyo. ziko taasisi na watu kadhaa wanaowiwa na suala hili na kwa namna moja au nyingine wanafaya juhudi zinazoweza kukopeshana au kuungana mkono na hiyo. Taasisi yetu ya Soma ni mojawapo. kauli mbiu yetu ni 'soma: burudani, utamaduni maarifa'. ina vipengele kadhaa: utafiti--1) watu wanasoma nini, wanataka kusoma nini, wanapata wapi cha kusoma, wanafanya nini kutimiza mahitaji yao, wana changamoto gani tunazoweza kushirikiana nao kuzikabili. 2) upatikanaji: wa vitabu na matini mengine--kwa kupitia maktaba za jamii/vituo vya maarifa, maduka ya vitabu, kusambaza taarifa za vitabu, kuibua na kuhuisha vyanzo vingine vya maarifa hata vilivyo vichwani na vinywani mwa watu hususani wenye elimu ndogo ya darasani au wasiokuwa nayo kabisa (kutokujua kusoma na kuandika si sawasawa na ujinga) kwa kupitia  amali za utamaduni na fasihi ili kurahisisha dhana ngeni/ngumu kueleweka ambazo zaweza kuwa ndizo zinahitajika kuwapa watu ufahamu na stadi za kukabiliana na changamoto za maisha yao.3) kuhimza mijadala na mitandao ya kuhimiza usomaji na shughuli za kifasihi, utamaduni na kianazuoni zinazochochea udadisi, uchambuzi na ari ya kutaka kujua zaidi na zaidi ili kuchukua hatua stahiki. 4) kuendeleza vipaji na stadi za uandishi, uibuaji na usambazaji wa maarifa. 5). kuendesha majukwaa na fursa za majadiliano ya kifasihi na kianazuoni yanayoambatana na burudani ili kufungamanisha maisha ya kawaida ikiwa ni pamoja na burudani na utamaduni wa kujifunza.


- demere kitunga

PICHA:

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP