Tuesday, June 19, 2012

Kupotea Njia Ndio Kuijua?

Tumepotea njia

Pendekezo la kitabu cha mkusanyiko wa mashairi
Na: demere kitunga, juni 19, 2012

1. Utangulizi

Kwa kipindi cha miongo miwili hivi, nchi yetu inapita katika msukosuko mkubwa. Kuanzia nyakati tulizoahidiwa kufunga mikanda kwa miezi 18 katika miaka ya 80, baadhi ya watanzania hawakuifungua tena na si ajabu wasiifungue kabisa wakati wa uhai wao. Lakini ingekuwa ni kufunga mikanda kwa miaka 18 ukiwa na matumaini kuwa madhila yako ni sadaka kwa vizazi vyako vya sasa na vijavyo, labda mzigo huo ungekuwa mwepesi kuubeba. Lakini yale tuliyoambiwa na wanazuoni wenye uzalendo wakati tunakubali sera za utandawazi ili angalau tupate bidhaa madukani, kuwa sera hizo hazitaifanya  hali kuwa nzuri kwa watu masikini kwani ufunguaji milango ulioshinikizwa utawafanya wapoteze hata kile kidogo walichonacho inajidhihirisha vema sana. Historia inatudai tuchukue hatua katika kila nyanja, ili kuinusuru hali hii, kama si leo hata iwe kesho, keshokutwa au mtondogoo. Nasi kama watu wa kalamu na fikra, hatuna budi kuutoa mchango wetu kwa njia moja au nyingine. Watafiti na waandishi wameshaandika sana na wanaendelea kuandika. Lakini haitakuwa ziada mbaya kama tutaweza kutoa juzuu moja la ushairi unaokijadili kipindi hiki cha historia. Siku moja, siikumbuki tarehe, tuliongea haya na Profesa Shivji kuhusiana na mkusanyiko wa ‘Summons’ uliohaririwa na Richard Mabala, kwamba mfululizo wake haujapatikana. Alinichagiza niongoze mchakato wa kupata mkusanyiko mwingine kama ule katika muktadha wetu wa sasa. Imenichukua muda kutafakari pa kuanzia, na leo nimeona pa kuanzia ni hapa. Kutuma mwaliko, na kuomba mrejesho na maboresho.

2. Jina: Tumepotea njia
Kwa kuanzia nimelipendekeza jina hilo lakini linaweza kubadilika. Wengi, pamoja na mimi, tunapenda majina yenye mwelekeo chanya, yanayotoa matumaini. Lakini katika lugha yangu ya kwanza, Chasu, tuna msemo usemao ‘kupotea njia ndio kuijua’. Nami naamini kuwa hali iliyopo sasa hivi ni ishara wazi kuwa tumepotea njia kama jamii, kama kizazi, na kama taifa. Labda tukilikubali hilo, tutatumia fursa hiyo vilevile kuitafuta, kuifuata na kuionyesha.

3. Utanzu: ushairi
Napendekeza ushairi kwa kuwa ni utanzu unaoweza kubeba mawazo mazito kwa maneno machache kuliko utanzu mwingine ukiacha methali. Vilevile ni utanzu uliokita mizizi katika fasihi na utamaduni wa mtanzania kwa miaka mingi. Utanzu huu pia hupokea na hupendeza unapokuwa na sauti nyingi ndani ya juzuu moja.

4. Lugha: Kiswahili
Japo maongezi yetu yalilenga ushairi kwa lugha ya Kiingereza, napendekeza tuanze na Kiswahili kwa makusudi. Mkusanyiko huu utakuwa mchango wetu katika mijadala na vitendo vya kupinga hali inayoendelea kujitokeza miongoni mwa makundi ya watanzania ambao wengi wao lugha yao ya mawasiliano ni Kiswahili. Hii ndiyo lugha ya umma wa mtanzania hivyo kama hatua ya kwanza katika ‘mradi’ huu, napendekeza Kiswahili.

5. Idadi, uwiano: [nakaribisha maoni]
6. Dhamira kuu na ndogondogo: [nakaribisha maoni]
7. Washiriki: Washairi wazalendo [rika na jinsia zote, waliobobea na chipukizi]

Kwa kuanzia kufikiri, itategemea na idadi ya mashairi na kama itabidi kuzalisha majuzuu mawili na iwe hivyo. Naamini baadhi yetu tuna mashairi tayari na mchakato huu unaweza kutupa hamasa ya kuongeza mengine. Labda tuweke ukomo wa juu wa mashairi tutakayochangia: napendekeza kila shairi lisizidi kurasa mbili na kwa kila mchangiaji ukomo wa juu uwe mashairi 5 ambayo yanaweza yasichapishwe yote kulingana na maoni yatakayojitokeza katika mchakato wa uhakiki na uhariri.

8Muda:
Uandishi—kukusanya: Juni/Julai; Uhakiki na Uhariri: Agosti; Usanifu na Uchapishaji: Septemba/Oktoba—lengo liwe kuchapishwa kabla ya Disemba

9. Njia:
i) Ukusanyaji: Michango itumwe kwa mhariri ambaye atapendekeza mpangilio na kutoa maoni ya kiuhakiki, na kuyakabidhi kwa kamati ya uhariri.
ii) Uhakiki na uhariri: Mhariri ataomba wachangiaji kupendekeza majina matano ya washairi na wahakiki wa ushairi kuwa wajumbe wa kamati ya uhariri. Kila mwanakamati atapatiwa mkusanyiko mzima aupitie na kutoa maoni ya uhakiki na kushauri kuhusu mpangilio na mapengo yanayohitajika kujazwa. Kila mchangiaji atapewa maoni binafsi kuhusu mashairi yake na mrejesho wake utazingatiwa katika hatua ya mwisho ya uhakiki/uhariri. Kisha mswada wa juzuu la kwanza utasambazwa kwa wachangiaji wote ambao mashairi yao yameingia ili kupata maoni yao. Mhariri ataratibu mirejesho na kamati itapitia mirejesho yote kabla ya kuupitisha mkusanyiko kuwa mswada.  
Uiii) Uchapishaji: Wachapishaji rafiki na wapenzi wa fasihi watakaribishwa kuupokea mswada kwa uchapishaji kwa masharti kuwa wataweza kuuzalisha kwa wakati uliopangwa—na kama ndivyo mkataba utafanyika wenye kuzingatia makubaliano hayo.

11   Mrabaha:
Wachangiaji watakubaliana jinsi watakavyogawana mrabaha. Mapendekezo ni kuwa tuwe na jambo fulani ambalo tutataka fedha zitakazopatikana zichangie[maoni zaidi yanakaribishwa].

Demere Kitunga < demeredye@gmail.com >
Mkahawa wa Vitabu Soma

0 comments:

Karibu kwenye ulingo wa kutafakari kuhusu tunapotoka,tulipo,tuendako na namna ambavyo tutafika huko tuendako/Welcome to a platform for reflecting on where we are coming from, where we are, where we are going and how we will get there

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP